Hakuna shaka kuwa Rais John Magufuli anatimiza ahadi yake ya kutumbua majipu aliyoitoa katika hotuba yake ya kwanza bungeni baada ya zaidi ya watumishi 152 wa Serikali kutimuliwa hata kabla ya siku 100 kutimia. Hao ni watumishi waliotimuliwa kwa majina au vyeo vyao, lakini ukijumlisha na wengine waliosimamishwa au kufukuzwa kwa matamko bila kutajwa majina, idadi ni kubwa zaidi. Watumishi hao wamesimamishwa na baadhi wamefukuzwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali za kukiuka Sheria ya Ununuzi wa Umma, Rais kutoridhishwa na utendaji wao, wizi kwenye taasisi zao, ukwepaji kodi, tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma na utovu wa nidhamu. Hatua hizo ni utekelezaji wa ahadi ambazo Rais Magufuli alitoa kwenye hotuba yake ya kwanza bungeni Novemba 2, mwaka jana mjini Dodoma, alipoahidi kupambana na rushwa bila kigugumizi wala haya yoyote. “Dawa ya jipu ni kulitumbua na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine,” alise