UTATA mkubwa umegubika idadi halisi ya watu waliopoteza maisha kwenye mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam. Wakati serikali ya mkoa ikisisitiza kuwa idadi ya waliopoteza maisha ni 38, zipo taarifa kuwa idadi hiyo inafichwa na serikali kwa sababu isizopenda kuzitaja. Akizungumzia kuhusu suala hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadik, alisema idadi ya watu waliokufa mpaka jana kwa mujibu wa takwimu za serikali ni watu 38. Alisema kama kuna watu wanazo taarifa zaidi juu ya vifo vilivyosababishwa na mafuriko wazipeleke sehemu zinazohusika. “Hatuna sababu ya kuficha vifo vya watu, sisi tunatangaza idadi ya maiti tulizoziona si vinginevyo,” alisema. Aliongeza kuwa ni jukumu la kila mmoja kushirikiana na serikali kuwahudumia waathirika wa mafuriko hayo ambao mpaka sasa wamefikia 5,000. Wakati utata ukigubika juu ya maiti hizo, baadhi ya wananchi wa maeneo ya Jangwani wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili, kuwa wameanza kusikia harufu za kuoza kwa vitu, na wameweka bayana kuw...