Leo tarehe 20 Machi 2013 ni siku ya mwisho ya wananchi kuwasilisha maombi ya kuwa wajumbe wa mabaraza ya katiba ya ngazi ya wilaya ambayo yana wajibu muhimu wa kupitia rasimu ya katiba na kutoa maoni iwapo imezingatia maoni ya wananchi yaliyokunywa katika hatua ya wananchi binafsi na makundi mbalimbali katika jamii. Nawakumbusha ambao bado hamjawasilisha maombi na mna dhamira ya kutimiza wajibu huu wa kiraia na kikatiba kwa kuwasilisha barua ya maombi kwa watendaji wa mitaa/vijiji. Kuna nafasi nane kwa kila mtaa kwa Dar es salaam, nne kwa maeneo mengine ya Tanzania Bara katika makundi yafuatayo; mwanamke, kijana, mtu mzima na mtu mwingine yoyote: kwa Zanzibar tatu kwa kila shehiya. Sifa ni raia, miaka 18 au zaidi mwenye kujua kusoma, kuandika, hekima, busara, uadilifu, uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo ambao najua wengi mnazo. Sifa nyingine ni kuwa mkazi wa kudumu kwenye mtaa au kijiji ambayo haimaanishi kwamba ni lazima uwe mwenye nyumba, hata wapangaji mnaruhusiwa kuomba. S...