Emmanuel Makaidi Mwenyekiti wa chama cha siasa NLD, Dk Emmanuel Makaidi (74) amefariki dunia hii leo Oktoba 15, 2015 mchana katika hospitali ya Nyangao mkoani Lindi kwa kile kilichotaarifiwa kuwa ni shinikizo la damu. Kifo cha Makaidi kimethibitishwa na viongozi wa NLD ambao wanadai kupata taarifa kutoka kwa mjane wa marehemu, Modesta Ponera-Makaidi. Dk Makaidi ambaye alikuwa ni Mwenyekiti Mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unaoundwa na vyama vya NLD, CHADEMA, CUF, na NCCR Mageuzi, pia alikuwa akiwania Ubunge wa Masasi Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Marehemu Dk Emmanuel Makaidi, mhandisi aliyebobea, alizaliwa Aprili 10, 1941 huko wilayani Masasi mkoani Mtwara. Baba yake mzazi alikuwa ni katekista wa Kanisa la Anglikana. Alianza elimu katika Shule ya Msingi Namalenga wilayani Masasi kati ya mwaka 1948 – 1952, mwaka 1953 – 1954 alisoma katika Shule ya Kati (Middle school) iitwayo Luatala hukohuko Masasi. Baaday...