UTEJA WA DAWA ZA KULEVYA UNACHANGIWA NA UNYANYAPAA TOKA KWA JAMII
UTEJA WA DAWA ZA KULEVYA UNACHANGIWA NA UNYANYAPAA TOKA KWA JAMII
Na: Edwin soko
Mwanza
Tabia ya jamii kuwanyanyapaa watumiaji wa dawa za kulevya imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa wateja wa dawa za kulevya waliacha kurejea matumizi ya dawa hizo na matokeo kuthidi kuathirika kimatendo kiroho na kimwili.
Makala hii ilijikita kutazama mtazamo wa jamii juu ya waliokuwa wateja wa dawa za kulevya baada ya kupata program maalumu toka kwenye Nyumba za utimamu (Sober Houses) na wanaopata tiba ya methadone toka kwenye kiliniki za Muhimbili, Mwanayamala na Temeke.
Ni imani yangu kuwa, tiba hizo mbili ni msaada mkubwa kwa wateja wa dawa za kulevya, endapo mtu atajitambua na kujikubali ni wazi kuwa ataachana na maisha ya uteja wa dawa za kulevya na kuishi maisha huru bila kuwa mtumwa wa dawa za kulevya.
Jamii ina wajibu mkubwa kwa waliokuwa wateja wa dawa za kulevya katika kuhakikisha kuwa hawanyanyapaliwi ili wasiweze kurudi tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa kupata upendo mkubwa toka kwa familia, ndugu na marafiki. Suala hili limekuwa gumu sana kwa jamii, kwani watu wengi wamekuwa hawana imani tena kwa mtu aliyekuwa akitumia dawa za kulevya na baadaye kuamua kuacha.
Bwana Novatus William mtumiaji wa dawa za kulevya anayepata tiba ya utimamu wa mwili ya Pili Missanah Mwamza alisema kuwa mazingira ya awali yana nafasi kubwa sana ya kumrudisha mtu aliyekuwa mteja wa dawa za kurejea tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa kuwa jamii inayomzunguka ina baki na picha ile ile ya uhalifu kwa mtu yule yule. .
Naye Bwana Nicholus Manota toka Nyumba ya utimamu ya pili Missah alisema kuwa familia za watu waliokuwa wakitumia dawa za kulevya zinakosa kurudisha imani kwa ndugu zao wanapoacha kutumia dawa za kulevya baada ya kutoka kwenye nyumba za utimamu na hali hiyo inapelekea walioacha dawa kukosa imani ya kuheshimiwa na jamii zao na hali hizo zinapelekea mtu kurudi katika matumizi ya dawa kwa lengo la kupata faraja.
Pia Manota aliongeza kuwa, hata jamii inayozunguka nyumba za utimamu (Sober Houses) imekuwa haina imani kabisa kwa kudhani wao ni wahalifu wakati ilibidi watambue kuwa wao ni watu wenye matatizo ya kiafya kama walivyo wagonjwa wengine na sio wahalifu.
Naye meneja wa nyumba ya utimamu ya Pili Misanah kata ya Ilongazala , wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza Bwana Mohammed Mohammed alibainisha kuwa, tatizo kubwa la wateja wengi walioacha dawa za kulevya kurejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya ni kukosekana kwa ushirikiano toka kwa jamii, kwani jamii imekuwa haitaki kuamini kwamba mtu anayetumia dawa za kulevya anaweza kupona na kurejea katika hali yake ya kawaida. Kitendo hicho kimekuwa kikiwabagua wateja walioacha dawa za kulevya na hatimaye kujikuta wametengwa na jamii nzima na hapo ndipo urudi kwenye kwenye matumizi ya dawa za kulevya ili kupata faraja.
Athari za matumizi ya dawa za kulevya zinaweza kuwa, kimwili, roho na akili |
Nyandidi aliongeza kuwa wateja wa dawa za kulevya upendo wa kijamii ili waweze kuimarika kimwili na kiroho na kujiona ni sehemu ya jamii licha ya maovu waliyokuwa wakiyafanya.
Naye Bibi Rehema Abdallah aliyeacha dawa za kulevya kwa kuhudhuria Kiliniki ya Methadone ya Muhimbili alimwambia mwandishi wa makala hii kuwa, dawa za kulevya zinauwezo wa kuachwa cha msingi ni elimu kwa jamii juu ya ukweli huu, kwani jamii bado inamchukulia mteja wa dawa za kulevya sawa na muhalifu.
Bwana Leonard Cyprian mkazi wa Mabatini ,Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza alisema kuwa jamii inaishi na ndoto za vitendo viovu vilivyokuwa vinafanywa na wateja wa dawa za kulevya hasa za wizi na unyang’anyi hivyo inakuwa vigumu sana kwa mara moja kuamini kuwa mtu aliyekuwa mwizi anaweza kuwa mwema.
Ni wazi kuwa jamii inabidi ibadilike na kuamini kuwa mtumiaji wa dawa za kulevya anaweza kupona na kurejea katika maisha yake ya kawaida, cha msingi jamii iwe na upendo na wale wote walioacha kutumia dawa za kulevya, kwani kuzidi kuwanyanyapaa ni kuzidi kukuza tatizo badala ya kupunguza tatizo, iwachukulie watu hao kama wagonjwa wengine wa malaria au Virusi vya Ukimwi/AIDS.
Kwa ushauri wasiliana na Mwandishi wa makala hii kwa simu 0754551306
Makala hii imedhaminiwa na Mfuko wa Kuvisaidia Vyombo vya Habari Tanzania(TMF)
Comments
Post a Comment