Mbunge asitisha msaada wa "mabasi ya wanafunzi" kwa kushindwa uchaguzi


Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Mikindani, mkoani hapa, Hasnein Murji, amesitisha huduma ya usafiri kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Naliendele kufuatia kushindwa ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.

Murji aligombea jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alikuwa akitoa usafiri kwa wanafunzi wa shule hiyo tangu mwaka 2011 alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti shuleni hapo, wanafunzi hao walisema kuwa kitendo cha kutochaguliwa mbunge huyo kimewaathiri kiusafiri.

‘Tangu alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hili, alitoa magari mawili ambayo yalikuwa yanapokezana, tulikuwa hatulipi nauli, tulikuwa tunawahi vipindi kwa sababu tulikuwa na uhakika wa usafiri,’ alisema mmoja wa wanafunzi hao.

Walisema usafiri wa daladala ni mchache, lakini pia wanatozwa nauli ya Sh. 500 badala ya Sh. 200.
Walidai kuwa wakati mwingine wazazi wanashindwa kumudu gharama na kushindwa kufika shuleni kwa sababu ya kukosa nauli.

Walisema hivi sasa wanafunzi wanaofanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne wanalazimika kupanda mabasi ya Tandahimba na Newala ili kuwahi kufanya mitihani.

Kharim Mohamed, ni mwanafunzi wa kidato cha tatu, alisema kuwa ukosefu wa usafiri wa uhakika unawafanya wachelewe vipindi na hukaa kituoni kwa saa tatu wakingoja usafiri.

Awali Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Hittu Rashid, alisema shule hiyo ilianza mwaka 1997, na tatizo la usafiri kwa shule hiyo limekuwa la muda mrefu. ‘Miaka ya nyuma kabla sijahamia hapa, niliambiwa kwamba wanafunzi walikuwa wakitumia malori ya mchanga kama usafiri wa kuja shuleni, na mwanafunzi mmoja alipata ulemavu baada ya kuvunjika mguu wakati akipanda gari,’ alisema.

Alisema, tangu kuwepo kwa usafiri wa uhakika wanafunzi wake wamekuwa na mahudhurio mazuri darasani na utoro ukipungua.

‘Kutoka mjini kuja hapa shuleni ni kilomita 12, na kutokana na tatizo la usafiri kwa wanafunzi wangu aliyekuwa mbunge aliona tatizo hili akaamua kuwasaidia, zaidi ya wanafunzi 50 walikuwa wakipanda magari yake bure,’ alisema.

Alipoulizwa na Nipashe kuhusu kusitisha usafiri huo, Murji, alikiri kuchukua hatua hiyo tangu Jumatatu iliyopita kwa madai kuwa alikuwa akitoa huduma hiyo kama mbunge wao, lakini sasa sio mbunge tena ni mfanyabishara kama walivyo wengine.

Aliwataka wamuombe mbunge wao wa sasa awasaidie.

Hata hivyo, alisema atatoa magari kwa ajili ya kwenda Mikindani kwa wananchi wote na nauli yake itakuwa Sh. 200 bila kujali umri wa mtu.

Akizungumzia mpango wa kuwasaidia wanafunzi hao hata kwa kuwatoza nauli ili kupunguza makali ya usafiri, Murji alisema: ‘Kwa kuwa mimi sio mbunge wao tena nafikiria kama nitaweza huenda nitawapelekea, lakini sijajua itachukua muda gani kurejesha usafiri shuleni hapo,’ alisema.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA