KUMBUKUMBU YA KIFO CHA MZEE A. MUTARAGARA CHIRANGI


MAREHEMU MZEE A. MUTARAGARA CHIRANGI

Pamoja na Mwanafalsafa Friesrich Nietzsche (1844 - 1900) kuona na kusema kweli kwamba, kuwa na subira au uvumilivu ni ngumu sana, hata kwa Washairi Wazamivu kushindwa kuzuia hasira zao kutoa dhamira ya ushairi wao au kwamba shauku haitasubiri!,

Tulimsikia na kumwona baba Mzee Mutaragara Chirangi (RIP), akionyesha uvumilivu katika anga za Siasa kwa hali isiyotegemewa.

Ni siku nyingine tena leo, ikiwa imetimia takribani miaka minne tangu atutoke duniani, tunaendelea kupata kumbukizi la changamoto toka maisha ya huyu mzee wetu.

Katika anga za ki- Siasa hususan baada ya chaguzi, uwezo wa Binadamu wengi kuweza kuvumilia au kunyenyekea au kuonyesha subira au kujizuia kusema au kufanya jambo ambalo halina tija wala maendeleo ya mwanadamu kwa leo na kesho, ni mdogo sana.

Dhamira ya uvumilivu aliyoitangaza mzee Chirangi kwa vitendo, kamwe haikumaanisha kushindwa kudai haki au kupigia debe maisha ya kukosa misimamo, la hasha; bali uwezo wa kutulia baada ya uchaguzi na kuchambua hali halisi na kuchukua hatua muafaka pasi jaziba, husuda wala chuki zisizo na maana.

Wenye kumbukumbu, wanaelewa ni mara ngapi mzee huyu aliwahi kugombea nafasi mbalimbali katika njanja kadha wa kadha, akashindwa na miitikio yake ilikuwaje na hata pia ilipotokea akashinda alisema na kufanya nini kwa waliokuwa washindani au hata wapinzani wake.

Hebu tusome sehemu tu ya moja ya Hotuba zake aliyoitoa Agosti 1977,baada ya kutoa huduma kwa mfululizo wa miaka 15 kama Mwenyekiti wa CCM Musoma mjini. Nanukuu:

“Kama ambavyo nimekuwa nikisema na kutenda, ieleweke wazi kuwa kiongozi achaguliwaye kwa kutoa fedha, ataongoza kwa kuchukua fedha, vilevile achaguliwaye kwa kufuata ukabila, atasimamia kabila, naye yule achaguliwaye kwa kampeni moto toka juu huenda akaondolewa kwa kampeni baridi kutoka chini.

Aidha, ni kitendo cha kutokukomaa kisiasa, kujenga chuki na hasira kwa mtu yeyote eti kwa sababu ya kutokupigia kura, kukushinda kwenye uchaguzi au kuazimia kugombea nafasi uliyodhani umetengewa wewe pekeke”.

Japo umelala baba, sauti na maisha yako yataendelea kutufunza milele na milele.

Kwa kila jambo kuna majira yake.....!

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA