Wenye kupata pasi za Kidiplomasia Tanzania ni pamoja na: Wake, Waume wa Viongozi na Wabunge

Serikali imesema wake au waume wa viongozi waandamizi nchini pamoja na wake ama waume wa wabunge wana haki ya kupatiwa pasi za kusafiria za kidiplomasia.

Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Pereira Ame Silima, alibainisha hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo (CCM) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Katika swali hilo, Chilolo alitaka kujua ni watu gani ambao wanastahili kupatiwa pasi za kusafiria za kidiplomasia na kama wake ama waume wa viongozi hao wakiwamo wabunge wanaruhusiwa kupatiwa pasi hizo.

Akijibu swali hilo, Silima alisema kwa mujibu wa makubaliano kati ya serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu cha 3(a) yaliyosainiwa jijini Arusha, inaelekeza viongozi hao kupatiwa haki zao, ikiwa ni pamoja na pasi za kusafiria za kidiplomasia.

Alisema wanaotakiwa kumiliki pasi hizo ni viongozi waandamizi wakiwamo makatibu wakuu, wabunge, mawaziri ikiwa ni pamoja na viongozi wa ngazi ya juu kwa kulingana na vyeo vyao.

Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Joyce Mukya (CHADEMA), alitaka kujua serikali inawaeleza nini Watanzania wenye sifa, lakini wanakataliwa kupewa pasi za kidiplomasia na kuwapo usumbufu wakati wa kuomba viza.

Aidha, alihoji kama serikali haioni kuwa Jumuiya kuwanyima pasi hizo kunawadhalilisha Watanzania hao wanaofanya kazi huko na pia kutengeneza mikataba miongoni mwa wanachama.

Silima alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki haitoi pasi za kusafiria kwa wafanyakazi wake wa ngazi yoyote.

Alieleza kuwa pasi za kusafiria za wafanya kazi wa Jumuiya hiyo hutolewa na nchi wanazotoka kuendana na matakwa ya kisheria ya nchi hizo.
Taznania Daima

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA