Nguo fupi alias ‘vimini’ ni marufuku Vyuo vya KKKT

Habari imeandikwa na Yusuph Mussa - Majira, Lushoto, Tanga

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira kilichopo jijini Arusha, Profesa Joseph Parsalaw, amesema kuqanzia sasa ni marukufu kwa wanawake wanaosoma katika vyuo vikuu vyote na vile vishiriki vinavyomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuvaa suruali za kubana au vimini.

Prof. Parsalaw aliyasema hayo juzi katika mahafali ya tatu ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU), kilichopo Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga na kusisitiza kuwa, lengo ni kutoa wahitimu ambao watakubalika kwenye jamii kwa matendo yao pamoja na uvaaji wao.

“Chuo Kikuu cha Tumaini kipo mstari wa mbele kuwahimiza wanafunzi na wafanyakazi kuzingatia maadili  anayokubalika kwenye jamii ya Kitanzania.  Hivi sasa katika vyuo vyote vishiriki, tumeweka bayana aina ya mavazi ambayo yanastahili kuvaliwa na vijana ili kudumisha heshima na maadili mema,” alisema Prof. Parsalaw.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha SEKOMU, Mchungaji Dkt. Anneth Munga, alisema chuo hicho ambacho pia kinatoa elimu maalumu, kitaendelea kuongeza mahitaji ya jamii.

Aliwataka wanataaluma ambao ni wahitimu katika mahafali hayo, kuwa mabalozi wazuri katika maeneo ya kazi ili jamii ijiridhishe kama wametoka katika chuo cha kanisa, kupata upako wa Mungu, kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kuwanyenyekea watu.

Dkt. Munga aliwataka wasomi hao kukitangaza chuo hicho kwa mema, kuwa na moyo wa kuwakumbuka waliowashika mkono kwa mara ya kwanza, kupata mwanga wa maisha na kuweza kuonekana mbele ya jamii.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA