ATHARI ZA KUJITOA KATIKA FAO LA UZEENI

Makala hii imejumuisha mawazo ya wale wote waliochangia kwenye hoja ya haja juu ya dhana ya mifuko ya hifadhi ya jamii, niliyoiweka kwenye blog hii tarehe 31.07.2012. Asante kwa mawazo ya kujenga na kwa paomoja tuijenge Tanzania yetu.

Natumaini tunaweza kukubaliana kuwa sera yoyote hupimwa ufanisi wake kwa kuzingatia inatekelezwaje mkabala na mahitaji ya uanzishwaji wake.Hakuna sera isiyokuwa na lengo, lengo likitimia ndipo tunapoweza kubaini  kuwa sera imefaulu au imeshindwa. Dhana na lengo la mifuko ya hifadhi ya jamii ni kuwakinga wananchi (wafanyakazi wa umma, binafsi, walioajiliwa na waliojiajili) dhidi ya matukio yasiyo tarajiwa  maana ambayo ni bayana. Lakini tukumbuke kuwa, neno “jamii” katika sera hii linatuvuta kuangaliazaidi ya mteja wa mifuko ya hifadhi ya jamii, lakini pia watu na taasisi zinazowazunguka ambazo  kwa njia moja au nyingine huweza kuathiriwa na matendo ya mteja  wa mifuko ya hifadhi ya jamii, hii ndio maana mifuko mingi ya hifadhi ya jamii hutoa mafao kadhaa kwa ndugu wa karibu wa mteja kama watoto na warithi wengine wa mteja huyu. Je, wajua kuwa tasisi za kifedha hutoa mikopo kwa wafanyakazi kwa kutegemea mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwa mteja atapatwa na janga lolote lenye uwezo wa kumfanya  ashindwe kulipa deni lake kwa kukatizwa kipato chake au kifo?
Ni muhimu kutambua kuwa, mifuko ya hifadhi ya jamii ina jukumu kubwa la kumlinda mteja na waanga wake dhidi ya matukio yanayoweza kusababisha umaskini  kwa sababu ya uzee au kutojiweza . Kuna mifuko ya hifadhi ya jamii tofauti kulingana na uhitaji wa mteja au aina ya ajira ya mchangiaji (mteja), ikimaanisha kuwa kuna mifuko ya wafanyakazi wa umma, binafsi, hata wale waliojiajili pia wanaweza kujiunga na  mifuko ya hifadhi ya jamii kwa mfano: LAPF (Mfuko wa hifadhi wa wafanyakazi wa serikali za mitaa) umetoa fursa kwa watu wa kada mbalimbali kujiunga na mfuko huo kwa kuchagua kiasi wanachoweza kumudu kuchangia. Ifahamike kuwa hifadhi ya jamii ni haki ya kila mtu kwa mujibu wa matamko mbalimbali ya ulimwengu ikiwemo katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,(kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara), hii ni kwa wote, wawe wameajiliwa au wamejiajili, tuzingatie kuwa kujiajili si suluhisho la uzee, vilema au aina nyingine za kutojiweza. Changamoto pekee kwa watu waliojiajili ni uhakika wa uchangiaji kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kiasi husika kwa mda muafaka, lakini pia ukosefu wa elimu ya kutosha  juu ya hifadhi ya jamii, maana yake, umuhimu wake na jinsi inavyofanya kazi, jambo ambalo huibua hisia na mitizamo tofauti juu ya huduma zinazotolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii.
Fao la kujitoa (withdrawal pension), ni malipo ambayo hufanywa na mfuko husika kwa mtu ambaye awali alikua mteja wa mfuko huo na baadae kujitoa kwa sababu ya kuacha kazi, kubadili kazi au muajili.
Zifuatazo ni athari za fao la kujitoa
1.      Kupunguza au kufuta kabisa fao la uzeeni
Ni dhahili kuwa mtu nanapolipwa fao la kujitoa au fao jingine lolote lile, rekodi hutunzwa na hufanyiwa makato wakati wa majumuisho ya fao la uzeeni. Hivyo mtu aliyepewa fao la kujitoa hawezi kupata fao la uzeeni. Pia kwa mtu ambaye amepatiwa huduma yoyote ile na mfuko wa hifadhi ya jamii kabla ya kustaafu hupata mafao tofauti na Yule ambaye hajapata huduma yoyote ile. Lakini hii haiwezi kubadili jukumu la mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa huduma kwa mtu mwenye uhitaji kwa mujibu wa taratibu na kanuni za mfuko husika.
2.      Kupata fao finyu kwa mteja anayejitoa
Mteja anayejitoa kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii mda mfupi mara baada ya kujiunga hupata fao finyu sana kwa sababu pesa yake inakuwa haijazalisha sana kama ilivyotarajiwa na mfuko husika. Hii ni kwa sababu kiwango cha pesa huongezeka kulingana na mda ambao pesa zimekaa kwenye mfuko husika. Mfano: Kiasi cha pesa ambacho kimetolewa baada ya mda wa miaka 5 hadi 10 ni tofauti sana na kiwango ambacho kimetolewa baada ya mda wa miaka 25 hadi 30.
3.      Kukosa kabisa matunzo ya uzeeni ya mwezi hadi mwezi
Ikumbukwe kuwa mteja aliyejitoa hukosa kabisa matunzo ya uzeeni ambayo hufuatia fao la kustaafu (kiinua mgongo), hii huturejesha kwenye matatizo ya umaskini usababishwao na uzee, maradhi au hali nyingine ya kutojiweza kama maradhi na mengineyo, jambo ambalo sera ya hifadhi ya jamii imedhamilia kulipunguza au kuliondoa kabisa.
4.      Kuathiri  malengo ya mfuko husika
Michango itolewayo na mifuko ya hifadhi ya jamii huwekezwa katika miradi mabalimbali ambayo huweka riba kwenye hela ya  mteja. Hivyo kujitoa kwa mteja mara tu baada ya kujiunga usababisha mfuko husika kukaa na hela mteja huyu mda mfupi kabla ya kuzalisha ipasavyo hivyo huathiri miradi ya mifuko husika iwapo wateja wengi zaidi watajitoa,hii uathiri zaidi hasa miradi ya mda mrefu kama majengo na miradi mingineyo ambayo uzalishaji wake ni wa mda mrefu.    
Ni muhimu kutambua kuwa kujitoa kwa kada fulani ya wafanyakazi, hasa wale wenye ajira za mikataba kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ni sawa na kumaanisha kuwa maana halisi ya mifuko ya hifadhi ya jamii haiwajumuishi kitu ambacho ni kinyume na uhalisia. Naamini hakuna anayepanga na Mungu, tujue kuna kupanga kuishi sana na ukaishi kidogo na kujua utaishi kidogo ukaishi kupita kiasi. Suala hapa ni kwamba ukijaliwa kupita hatua moja utamuduje hatua nyingine na ukishindwa , wale wanaokutegemea watabaki katika hali gani.
Kipi tunatakiwa kufanya.
Tukubaliane kuwa sisi wote tunapenda kufaidi matunda ya jasho letu tukiwa pamoja na ndugu, jamaa na marafiki zetu, japokuwa hakuna anayejua kesho, kwa maana tungejua tungeweka bajeti kufikia pale tutakapokoma kuishi. Yafuatayo ni muhimu ili kuhakikisha ufanisi wa mifuko yetu ya hifadhi ya jamii.
1.      Kuhamishika kwa mafao kutoka mfuko hadi mfuko.
Watafiti wengi pamoja na ripoti zinaonyesha kuwa kuna tatizo la uhamishikaji wa mafao kutoka mfuko hadi mfuko. Hii ni muhimu pale mtu anapobadilisha ajira, kazi au muajiri ikiwa ni pamoja na kujiajiri: kwamba, kama ajira au muajiri fulani alifanya muajiliwa kuchangia katika mfuko wa PPF na baada ya kubadili kazi anatakiwa kuchangia katika mfuko wa LAPF, basi kuwepo na uwezekano kuhamisha mafao ya mteja kutoka mfuko wa awali kuja mfuko mpya zikiambatana na taarifa zote za marejesho ya mchangiaji ili imuwezeshe kuendelea kuchangia kwa ajili ya manufaa yake ya baadae ya uzeeni pindi atakapopoteza nguvu za kufanya kazi kuliko kukimbilia kujitoa  jambo ambalo ni tofauti na Lengo kuu la mifuko ya hifadhi ya jamii.
2.      Mamlaka ya udhibiti wa mifuko ya hifadhi ya jamii iweke taratibu mahususi ya kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii kuhakikisha kuwa huduma tajwa zinapatikana kwa wateja bila usumbufu wa aina yoyote ile na kwa muda muafaka. Hii itaongeza imani na kupunguza malalamiko dhidi ya mifuko ya hifadhi ya jamii.
3.      Pesa zinazotolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa taasisi mbalimbali za serikali na za binafsi zifuate taratibu na kanuni za mikopo na zirejeshwe kwa riba  ndani ya muda muafaka bila kuathiri hali ya kifedha ya mifuko ya hifadhi ya jamii.
4.      Mifuko ya hifadhi ya jamii ianzishe miradi yenye kunufaisha wateja wake, kama vile kujenga nyumba na kuwauzia wateja wake kwa bei nafuu kwa mfumo wa mikopo yenye masharti nafuu na miradi mingine kama hiyo.
5.      Pawepo na utaratibu wa kutoa mafao kwa wateja kwa hawamu mbili, yaani kwa umri wa kati wa kustaafu (kwa hiari au lazima) tangu mteja alipoanza kuchangia katika mfuko husika na pindi anapotimiza umri wa kustaafu(kwa hiari au kwa lazima)
6.      Pawepo na taratibu rahisi na za kueleweka  za kupata mafao, ili kumwezesha mteja kupata huduma husika kwa urahisi pindi awapo na uhitaji na anapostahili kupata mafao ya uzeeni.
7.      Lakini pia Huduma za mifuko ya hifadhi ya jamii ziboreshwe zaidi ili kuvutia wateja wake kwa kutoa huduma bora.
Kwa kumalizia naomba kila mmoja atambue wajibbu wake kuanzia kwa muajiliwa, muajiri kwa kuchangia kwa wakati kiasi tajwa kwenye mifuko husika. Lakini pia mifuko ya hifadhi ya jamii itoe huduma stahiki kwa wateja wake pindi wanapokuwa na uhitaji huku wakitambua kuwa hiyo ni nguvu yao, ni hela yao na ni haki yao, Mamlaka zenye dhamana ya kudhibiti mifuko ya hifahi ya jamii zikiwemo za kutunga sheria, zitunge sheria na kuandaa sera inayonufaisha mteja na si kundi fulani la watu au wanasisa,  hii italeta ufanisi katika sekita hii ya hifadhi ya jamii na itaondoa manung’uniko kwa walaji.    
Ninapenda pia kutoa ushauri wangu wa dhati kwa wale wanaofanya kazi kwa mikataba, kuwa pindi wasitishapo mikataba yao wasikimbilie kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, ila watafute jinsi ya kuendelea kuchangia ikiwa ni pamoja na kuhama mifuko kwenda kwenye ile mifuko inayohusika na aina ya kazi au waajili walionao , kwani ni muhimu kwa ajili ya maisha yao ya baadae. Tukumbuke kuwa hifadhi ya jamii ni zaidi ya pensheni. Ukweli ni kwamba hata aliyejiajiri anahitaji na anastahili hifadhi kutoka kwa jamii. Ni muhimu kutambua kuwa hela inakuwa salama zaidi inapokuwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, kinachohitajika ni kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi thabiti wa mifuko hiyo ili kuwepo na ufanisi. “mifuko ya hifadhi ya jamii kwa manufaa yetu, tuisimamie kwa kwa ajili ya maisha yetu ya baadae

Kwa  maoni na maswali zaidi, wasiliana na:
Davis Muzahula,
Mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya sheria (mwaka wa nne),
Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania
Simu: +255756829416
Barua pepe: davismuzahula@yahoo.com

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA