PPRA Yafungia Makampuni 7 Kwa Udanganyifu, Yatoa Ripoti ya Mwaka
Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Matern Lumbanga |
Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Matern Lumbanga (Kulia) akiongea na waandishi wa habari, Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Dk. Laurent Shirima. |
Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA),
imeyafungia makampuni 7 pamoja na wakurugenzi wake kutokana na vitendo vya
udanganyifu.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo katika makao makuu ya PPRA, Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Matern
Lumbanga amesema kuwa Mamlaka hiyo imeamua kuyafungia makampuni hayo kwa mujibu
wa kifungu cha 62 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma Na. 7 ya Mwaka 2011 na Kanuni
ya 98 ya Tangazo la Serikali Na. 446 la Mwaka 2013.
Aidha, Balozi Lumbanga alisema kuwa
kati ya makampuni hayo, Gagaja Contractors Company Limited, limefungiwa kwa
kipindi cha miaka 10 (kutoka tarehe 2 Oktoba,2015 hadi 1 Octoba, 2025) kwa kosa
la kuwasilisha dhamana za zabuni za kughushi wakati wa michakato ya zabuni.
Aidha, Balozi Lumbanga alisema kuwa
makampuni mengine Sita yamefungiwa kwa kipindi cha miaka miwili (kuanzia tarehe
2, Oktoba, 2015 hadi 1, Oktoba 2017 kwa kukiuka masharti ya mikataba.
Makampuni hayo sita ni pamoja na
Intersystem Holdings Company Limited,PEMA TECH Company Limited, Nyakire
Investment Limited, Kosemwa Prospects Company Limited, PERNTELS Company Limited
na Car and General Trading Limited.
Katika hatua nyingine, PPRA imetoa
matokeo ya ukaguzi ya mwaka wa fedha 2014/2015 ambapo imebainika kuwepo kwa
ongezeko kidogo la uzingatiaji wa sheria katika manunuzi ya umma.
“Matokeo yamebaini kiwango kidogo
cha ongezeko la uzingatiaji wa sheria kutoka wastani wa asilimia 65 mwaka jana
hadi kufikia asilimia 69 mwaka huu. Aidha, wastani huu bado uko chini ya lengo
lililowekwa la asilimia 75,” alisema Balozi Lumbanga.
Aidha, alibainisha kuwepo mapungufu
kadhaa ikiwa ni pamoja na malipo hewa ya kazi za ujenzi wa kandarasi katika
taasisi 9, malipo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 951.7.
“Malipo ya zaidi ya shilingi milioni
951.7 yalilipwa kwa wakandarasi kwa kazi hewa (non existing works). Kiasi hiki
ni sawa na asilimia 15 ya jumla ya thamani ya miradi yote ya kazi za ujenzi
iliyokaguliwa,”alisema.
Kadhalika, ripoti hiyo ilibainisha
uwepo wa viashiria vya rushwa katika baadhi ya taasisi na kueleza kuwa Mamlaka
hiyo itayapeleka majina ya taasisi hizo TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi.
Alizitaja taasisi hizo kuwa ni NEC
(29%), Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (21), Halmashauri ya Wilaya ya
Mpanda (22%), Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo (24%), Halmashauri ya Wilaya ya
Kigoma (28%), Agricultural Input Trust Fund (28%), Halmashauri ya Wilaya ya
Mbozi (20%) na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu (31%).
Comments
Post a Comment