UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA WAANZA AFRIKA KUSINI

Raia wa Afrika Kusini wanapiga kura katika chaguzi za serikali za mitaa ambazo huenda zikawa pigo kwa chama cha ANC ambacho kimeiongoza nchi hiyo tangu kumalizika kwa enzi ya ubaguzi wa rangi miaka 22 iliyopita.
Jana saa moja asubuhi Wapiga kura walianza kupanga foleni katika vituo vya kupigia kura kukiwa na hali ya baridi kali. Takriban wapiga kura milioni 26.3 wamesajiliwa kushiriki katika chaguzi hizo.
Kulingana na kura za maoni, chama cha ANC kiko katika hatari ya kupoteza viti katika miji muhimu nchini humo ukiwemo mji mkuu Pretoria, mji mkuu wa kibiashara Johannesburg na mji wa pwani wa Port Elizabeth ujulikanao pia kama Nelson Mandela Bay.
Maendeleo nchini Afrika Kusini yamekuwa sio ya kasi iliyotarajiwa tangu Hayati Nelson Mandela aliposhinda katika uchaguzi wa kihistoria mwaka 1994 ambapo enzi ya ubaguzi rangi ilikoma nchini humo. Bado raia wengi weusi hawana maakazi mazuri, elimu bora na nafasi za ajira.
Je ANC kitastahimili kishindo?
Benki kuu nchini humo imesema uchumi utatuwama kwa asilimia sufuri mwaka huu na vyama vya upinzani Democratic Alliance na Economic Freedom Fighters EFF kinachoongozwa na Julius Malema vimeishutumu serikali ya Rais Jacob Zuma kwa kuurejesha nyuma uchumi wa taifa hilo imara zaidi kiuchumi barani Afrika. Upinzani umeahidi kuuboresha uchumi iwapo utashinda katika chaguzi hizo.
Kiongozi wa kwanza mweusi wa chama cha DA Mmusi Maimane amesema Afrika Kuisni iko katika nafasi ya kujipatia kitu cha kipekee na cha kihistoria katika chaguzi hizo akikitaja chama tawala cha ANC kuwa fisadi, badhirifu na kuondoka kutoka ndoto waliyokuwa nayo waafrika Kusini ya demokrasia.
Rais Zuma ana uungwaji mkono mkubwa nchini humo hasa katika maeneo ya vijijini na ANC kimekita mizizi miongoni mwa raia wa nchi hiyo na kina fedha za kuwashawishi wapiga kura ili kiendelee kuwa na wingi wa viti 278 vya mameya na madiwani.
Uchaguzi kipimo cha umaarufu wa Zuma
Lakini umaarufu wa Zuma umeingia dowa kutokana na kashfa chungu nzima za ufisadi, kesi mahakamani, kuzorota kwa uchumi wakati wa uongozi wake na viwango vya wasio na kazi vikiwa asilimia 27. Kati ya watu wanne nchini humo, mmoja hana kazi.
Mlungiseleli Kwanini mwenye umri wa miaka 60 ambaye anafanya vibarua katika mji wa Port Elizabeth amesema ANC kimeshindwa vibaya katika kuteleza ahadi zake ilizotoa kilipoingia madarakani 1994 na kinachoshuhudiwa ni ukosefu wa ajira, viwango vya juu vya uhalifu na ufisadi na ukosefu wa huduma muhimu kama maji na umeme.
Matokeo ya chaguzi hizo zinazotajwa kuwa kipimo cha umaarufu wa Rais Zuma yanatarajiwa siku ya Alhamisi na huenda yakaongeza shinikizo kwa kiongozi huyo kujiuzulu kabla ya muhula wake kukamilika mwaka 2019.
Zuma hata hivyo amesema ana imani watashinda viti vingi. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Afrika Kusini Judith February amesema iwapo ANC kitashindwa katika mabaraza muhimu, yaliyo na watu weusi wengi kama Johannesburg na Nelson Mandela Bay, itamaanisha hali ngumu kwa Rais Zuma. Hata hivyo February ameongeza kuwa ANC huenda kikawashangaza wengi matokeo yatakapotangazwa.DW

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA