MAFURIKO YA DAR..............

UTATA mkubwa umegubika idadi halisi ya watu waliopoteza maisha kwenye mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam. Wakati serikali ya mkoa ikisisitiza kuwa idadi ya waliopoteza maisha ni 38, zipo taarifa kuwa idadi hiyo inafichwa na serikali kwa sababu isizopenda kuzitaja. Akizungumzia kuhusu suala hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadik, alisema idadi ya watu waliokufa mpaka jana kwa mujibu wa takwimu za serikali ni watu 38. Alisema kama kuna watu wanazo taarifa zaidi juu ya vifo vilivyosababishwa na mafuriko wazipeleke sehemu zinazohusika. “Hatuna sababu ya kuficha vifo vya watu, sisi tunatangaza idadi ya maiti tulizoziona si vinginevyo,” alisema. Aliongeza kuwa ni jukumu la kila mmoja kushirikiana na serikali kuwahudumia waathirika wa mafuriko hayo ambao mpaka sasa wamefikia 5,000. Wakati utata ukigubika juu ya maiti hizo, baadhi ya wananchi wa maeneo ya Jangwani wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili, kuwa wameanza kusikia harufu za kuoza kwa vitu, na wameweka bayana kuwa wana hofu kuwa kuna baadhi ya miili ya watu imezama kwenye tope na mingine imechanganyika na takataka zilizonasa kwenye maeneo mbalimbali. Amos John, anayeishi nyuma ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alisema kuwa kwenye miti ya mikoko kuna uchafu mwingi ambao mpaka sasa haujafukuliwa. Alibainisha kuwa jana aliwaona baadhi ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiwa na machela iliyobeba maiti. “Nina imani kuwa idadi ya watu waliokufa kwenye mafuriko haya ni kubwa zaidi, ninaomba serikali iongeze jitihada kutafuta maiti,” amesema. Hashim Suleiman alisema uchafu ulioletwa kwenye maeneo yao na maji unaweza kuhifadhi miili ya watu ambao kadiri inavyoendelea kukaa ndivyo inavyozidi kuharibika. Aliongeza kuwa iwapo maiti hizo hazitaweza kupatikana haraka kuna hatari kubwa ya maeneo yao kukumbwa na harufu kali pamoja na magonjwa mbalimbali.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA