Madaktari waipa serikali siku 14 baada ya wenzao kupigwa na kusimamishwa kazi
Akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari katika hosptali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es salaam, rais wa chama cha madaktari Dk Billy Haonga amesema vyombo vinavyohusika, kama jeshi la polisi na serikali, visipochukuwa hatua stahiki kwa muda wa siku 14 chama hicho kitaitisha mkutano mkuu wa dharura kujadili usalama wao na hadhi ya tasnia ya udaktari katika kutoa huduma.
Aidha, Dk Haonga amesema kuwa katika sekta zinazofanya kazi chini ya kiwango kwa asilimia kubwa kwenye sekta zake zote hapa nchini ni sekta ya afya kutokana na uhaba wa raslimali watu, vifaa tiba na madawa. Ameeleza kuwa mapungufu hayo yanatokana na bajeti ndogo ya sekta ya afya inayotengwa na serikali, jambo linaloathiri kwa kiasi kikubwa utoaji na upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi. Amewataka wanasiasa kuwaeleza ukweli wananchi badala ya kutupa lawama kwa wahudumu wa afya.
“Hali inayojijenga kwa sasa inamwondolea daktari utu na huruma na kutokuaminiana kati ya mtoa huduma na mpokeaji huduma jambo ambalo litapelekea kuumia hata kusababisha vifo kwa wagonjwa,” amesema Dk Haonga.
Comments
Post a Comment