Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Muhongo akabidhi gari la wagonjwa, Akerwa Ufaulu Duni wa Wanafunzi
Makabidhiano hayo yamefanyika hivi karibuni kituoni hapo na kushuhudiwa na wananchi mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya wilaya hiyo baada ya gari hiyo kukaguliwa kwa kina na Daktari Bingwa wa huduma za dharura na Majanga, Dkt. Christopher Mnzava na kujiridhisha kwamba lipo tayari kwa kuanza kutumika kutoa huduma husika.
Akizungumza kabla ya makabidhiano hayo, Profesa Muhongo alisema gari hilo limetolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya wananchi wa jimbo la Musoma Vijijini lengo likiwa ni kusaidia wananchi hao kuondokana na usumbufu waliokuwa wakiupata.
Alisema kwamba Serikali hiyo ya Japan kupitilia Balozi wake nchini Tanzania, imeahidi kwamba endapo gari hilo litatunzwa na kutumika kwa lengo lililokusudiwa ndani ya kipindi cha miezi sita, wananchi hao wataongezwa gari lingine la aina hiyo.
Profesa Muhongo aliwaagiza wananchi wa jimboni humo kuwa walinzi wa gari hilo ili kuhakikisha linatunzwa vizuri na vilevile linatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Ninamuomba Dkt. Mnzava awe anakuja huku mara kwa mara kwa ajili ya kuligakua. Nyie tutakaowakabidhi endapo mtatatizwa na jambo kwenye gari hilo muwasiliane nae ili awapatie maelekezo ya nini cha kufanya.”
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Dkt. Mnzava alimpongeza Mbunge huyo kwa juhudi zake za kuhakikisha anamaliza kero mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa jimboni humo hususan katika suala la afya.
Alisema kuwa amelikagua gari hilo na kwamba ni gari la kisasa na ni tofauti na magari mengine ya wagonjwa ambayo yapo katika hospitali mbalimbali nchini.
Aliongeza kuwa vifaa vilivyomo ndani ya gari hilo ni adimu na hivyo inapasa watakaokabidhiwa walitunze. “Kwa hapa Tanzania gari la aina hii lipo hospitali ya Muhimbili peke yake; hivyo kwa sasa yapo mawili moja ni hili la Murangi na lingine ni la Muhimbili,” alisema.
Alisema wananchi wa Musoma Vijijini wanayo bahati kubwa kuwa na Mbunge ambaye anajitahidi kushughulikia kero zao kwa kuwatafutia ufumbuzi wa kudumu.
Aidha, kwa upande wa wananchi waliojitokeza kushuhudia makabidhiano hayo, walimpongeza Profesa Muhongo kwa juhudi zake alizozionyesha tangu amechaguliwa za kuwaletea maendeleo.
Nyanjiga Mgeta ambaye alikuwa Kituoni hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu alizungumza na mwandishi wa habari hii na kueleza kuridhishwa kwake na kasi ya maendeleo ya mbunge huyo.
Mgeta alisema hapo awali iliwalazimu wakodi magari ili kufikisha wagonjwa mahututi hospitalini jambo ambalo ni gharama kubwa na vile vile upatikanaji wa magari jimboni humo ni mgumu.
Mwananchi mwingine aliyefahamika kwa jina la Eliza Chilyamkobi alimpongeza Profesa Muhongo na kueleza kwamba gari hilo ni mkombozi kwao na vilevile alimuahidi ushirikiano zaidi na ulinzi wa gari hilo.
Aidha, Profesa Muhongo alisema ifikapo tarehe 6 mwezi huu timu ya madaktari bingwa wapatao sita kutoka China itawasili kituoni hapo kwa ajili ya kutoa huduma ya uchunguzi wa afya na kutoa tiba kwa maradhi mbalimbali.
Alisema madaktari hao vilevile wanakuja na madawa ambayo watayakabidhi kwa wahusika kituoni hapo na huku akiwataka wananchi hao kujitokeza kwa wingi ili kupatiwa tiba bila gharama yoyote.
Katika hafla hiyo, Profesa Muhongo alichangia bati 50 na mifuko ya saruji 234 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Wadi ya kina mama na watoto.
Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akifungua mlango wa gari la wagonjwa kabla ya kulikabidhi rasmi.
Daktari Bingwa wa huduma za dharura na Majanga, Dkt. Christopher Mnzava (kulia) akizungumza jambo wakati wa hafla ya kukabidhi gari la wagonjwa la Kituo cha Afya cha Murangi. Kushoto ni Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
Gari la wagonjwa la Kituo cha Afya cha Murangi ambalo limekabidhiwa hivi karibuni. Gari la namna hiyo na la pili nchini na huku lingine lipo Hospitali ya Muhimbili.
Vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa katika gari la wagonjwa la Kituo cha Afya cha Murangi.
Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akilikagua gari la wagonjwa kabla ya kulikabidhi.
Muhongo akerwa na ufaulu duni wa wanafunzi jimboni kwake
Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema amesikitishwa na matokeo ya Kidato cha Nne katika jimbo lake na kusisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka ili kukomesha hali hiyo.
Aliyasema hayo hivi karibuni katika kijiji cha Murangi, Mkoani Mara kwenye hafla ya kukabidhi gari la kisasa la wagonjwa la Kituo cha Afya cha Murangi.
Alisema shule za Serikali jimboni humo zimetia aibu kwani matokeo yao hayaridhishi na sio ya kujivunia na huku akisisitiza hatua za haraka zinahitajika ili kubaini chanzo cha tatizo hilo la wanafunzi wengi kufanya vibaya kwenye mitihani yao.
Kufuatia hali hiyo, Profesa Muhongo aliagiza wasaidizi wake watano ambao waliajiriwa mapema mwaka huu maalum kwa kafuatilia shughuli za jimbo kutembelea shule zilizopo kwenye maeneo yao na kuzungumza na wakuu wa shule hizo na kumpatia taarifa.
Aliagiza wakutane na wakuu wa shule zote zilizomo jimboni humo na kila mkuu wa shule aeleze sababu za kuwa na matokeo mabaya ya mitihani iliyopita ya kidato cha nne.
“Hawa vijana nimewaajiri kufuatilia shughuli za jimbo na kwa kawaida kila wiki wananiletea taarifa za masuala mbalimbali ya kimaendeleo ambayo ninatekeleza ili kuelewa kuhusu utekelezaji wake,” alisema.
Alisema binafsi anaelelewa baadhi ya sababu zinazochangia wanafunzi kufanya vibaya lakini ametoa agizo hilo la kupata maelezo ya wakuu wa shule ili kujiridhisha zaidi.
Mbali na hilo, Profesa Muhongo aliwalaumu madiwani jimboni humo kwa kushindwa kufuatilia suala la elimu. “Madiwani hii ni kazi yenu, haiwezekani tumepata matokeo mabaya na hadi leo hii hamjaitisha kikao kujadili.”
Aliagiza kwamba taarifa husika ikamilike ndani ya mwezi mmoja na baada ya kupatiwa taarifa hiyo alisema ataitisha mkutano maalum wa elimu ili kuijadili.
Alisema endapo kutathibitika kuna wanaosababisha hali hiyo ya matokeo mabaya kwa namna yoyote ile watu hao itabidi wapewe adhabu.
Alisema inawezekana baadhi ya wazazi pia kwa namna moja ama nyingine wanachangia vijana kupata matokeo mabaya. “Hadi sasa kwa taarifa nilionayo kuna vijana 224 wamefaulu kujiunga na kidato cha kwanza lakini hadi hivi sasa hawajajiunga; na madiwani mpo tu mnatazama bila kuchukua hatua na mnaona ni kawaida,”
Aliagiza kupatiwa majina ya wazazi wote waliogoma kuruhusu watoto wao kuendelea na masomo na vilevile yapelekwe kwa Mkuu wa Wilaya. “Nataka hili lifanyike ndani ya wiki moja na watoto wote wawe wameenda shule.”
Vilevile Profesa Muhongo alisema suala alilogundua ni kwamba wanafunzi wengi hawana mazoea ya kujisomea vitabu ili kuongeza uelewa baada ya kutoka shule.
Alisisitiza umuhimu wa kusoma vitabu badala ya kukariri madaftari ya darasani. “Unakuta motto anatoka shule halafu anasoma daftari aliloandika darasani badala ya vitabu. Ndiyo maana nimewaletea vitabu ili kuwa na uelewa mpana zaidi.”
Alisema awamu ya kwanza alipeleka vitabu 7,110 vya Sekondari na vitabu 12,800 vya msingi na awamu inayofuata vitabu vitakavyoingia vitakua zaidi ya 25,000 vingi vikiwa ni vya sayansi, hesabu na kiingereza.
Mbali na hilo, Profesa Muhongo alihoji utendaji wa Halmashauri na kueleza kutoridhishwa na utendaji wake na hivyo aliagiza kufuatiliwa kwa karibu kwa Afisa Elimu wa Halmashauri hiyo.
“Inashangaza Halmashauri nao wanalalamika sasa kazi yao nini?; Afisa Elimu hafai, tutamfuatilia kwa karibu,” alisema.
Profesa Muhongo vilevile aliagiza madiwani wote jimboni humo kuacha kuingilia shughuli za watendaji hususan kwenye suala la ukusanyaji wa kodi.
“Hakuna diwani kukusanya kodi, nyie ni wa kupokea taarifa kujadili na kufanya tathmini; ni utendaji wa hovyo diwani kujihusisha na ukusanyaji kodi. Mliomba udiwani kuleta maendeleo na siyo kutumbua maisha,” alisisitiza.
Hafla hiyo ya makabidhiano ilihudhuriwa na wananchi mbalimbali wa jimboni humo, wataalamu wa afya wa kituo cha Murangi, wadau wa maendeleo na watendaji wa Halmashauri husika.
Comments
Post a Comment