Watu 17 wachinjwa kama kuku Musoma

WATU 17 wa familia tatu tofauti wakiwemo watoto wanane, wameuawa usiku wa kuamkia jana katika Kijiji cha Buhare, nje kidogo ya mji wa Musoma, mkoani Mara.

Miongoni mwa waliouawa ni wanawake 11 na wanaume sita, wakiwamo watoto wa kike watano na wa kiume watatu.

Wanane kati ya watu hao ni wa familia moja, akiwemo mume, mke, na watu wengine sita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Robert Boaz, amezitaja familia zilizokumbwa na maafa hayo ya kutisha kuwa ni za Kawawa Nyarukembe iliyopoteza watu wanane, Moris Mgaya watu sita na Mgaya Nyarukembe iliyopoteza watu watatu, akiwemo mke wa mwenye nyumba.

Akielezea tukio hilo, Kamanda Boaz alisema watu wasiofahamika walizivamia familia hizo juzi saa sita usiku, wakavunja milango ya nyumba zao na kuwashambulia wanafamilia kwa silaha zenye ncha kali, huku wengine miili yao ikitenganishwa na viwiliwili.

Aliwataja waliouawa katika tukio hilo la kutisha ni Nyambona Kawawa, Juliana Kawawa, Nyarukende Kawawa, Mengi Kawawa Nyanyama Kawawa, Kenguye Kawawa, Angelina Kawawa na Mzee Kawawa Kinguye.

Wengine ni Umbera Mgaya, Dorika Mgaya, Mzee Mgaya Moris, Magreth Moris, Aric Moris, Kado Moris, Maheri Moris, Nyasinde Moris pamoja na Joseph Sotereti ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mkirira iliyopo Manispaa ya Musoma.

Mbali ya watu hao 17 waliouawa, wengine watatu wamejeruhiwa vibaya na wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara, wakiendelea na matibabu.

Chanzo cha habari kiliiambia Tanzania Daima Jumatano kwamba siku ya tukio watu wasiojulikana wakiwa na silaha zenye ncha kali, walivamia kwa wakati mmoja familia hizo na kuvunja milango kwa kutumia mawe makubwa maarufu kwa jina la 'Fatuma'.

Mara baada ya kufanya unyama kwa wanafamilia hao, vilio vilitawala kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Baada ya askari polisi kupewa taarifa ya tukio hilo, walifika kwenye eneo la tukio na kuimarisha ulinzi huku wakiwa na silaha za moto aina ya SMG, na wengine wa Jeshi la Wananchi (JWT) ambao hawakuonekana kuwa na silaha.

Tanzania Daima Jumatano ambayo ilifika eneo hilo ilishuhudia miili ya marehemu hao ikiwa kwenye vyumba tofauti katika nyumba walizokuwa wamelala. Maiti moja ilikuwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.

Habari zaidi zilizopatikana katika eneo la tukio zilieleza kuwa ni tukio la pili kutokea. Tukio la kwanza lilitokea mwaka 2006, kwa kuihusisha familia moja ya Mzee Kawawa Kinguye, ambapo watu wawili waliuawa kwa mapanga.

Kamanda Boaz aliiambia Tanzania Daima Jumatano kuwa tayari watu watatu walikuwa wameshakamatwa hadi kufikia jana mchana na kwamba Jeshi la Polisi litatumia mbinu zote za kijeshi kuwanasa waliohusika na tukio hilo la kinyama.

Alisema mazishi ya marehemu hao yatafanyika siku yoyote baada ya taratibu za kifamilia kukamilika.

“Ndugu yangu hili ni tukio baya sana na ni tukio la kwanza kutokea tangu nihamishiwe hapa. Lakini hadi sasa (jana mchana), watu watatu tumeshawakamata kuhusiana na tukio hili na tutatumia mbinu zetu zote kuwakamata na wengine waliohusika,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Enos Mfuru, alisema chanzo cha mauaji hayo ni kulipiza kisasi cha uhasama uliokuwepo dhidi ya familia za koo hiyo na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi ambao baadhi yao waliuawa miaka minne iliyopita baada ya kupora mifugo ya wanafamilia hao.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mara, Benadictor Mwizarubi alisema watu waliolazwa kutokana na kujeruhiwa ni pamoja na Moris Mgaya, Maximilian Robert na Mariam Kawawa.

Hivi karibuni katika mkoa mwingine uliopo Kanda ya Ziwa, Mwanza, kulitokea mauaji ya kutisha ya watu 14, akiwamo jambazi mmoja waliouawa katika shambulio la kutupiana risasi kati ya majambazi na wananchi katika kisiwa kidogo cha Izinga, wilayani Ukerewe.

Katika tukio hilo watu wengine 17 walijeruhumiwa.

"chanzo cha habari hii ni kutoka gazeti la Tanzania daima"

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA