Serikali yapiga marufuku WOTE wanaojinadi kuponya/kuganga/kutibu UKIMWI



Serikali imewataka watu wanaojitangaza kutibu UKIMWI zikiwemo taasisi za dini na waganga wa jadi, kuacha mara moja kufanya hivyo kwa kuwa wanafifisha mapambano na kupotosha ukweli kwamba hakuna dawa ya ugonjwa huo kwa sasa.

Aidha wanaoishi na ugonjwa huo wanaotumia dawa za kukabiliana na makali yake (ARVs), wameshauriwa kuyapuuza matangazo hayo hasa yanayowataka kuacha kutumia dawa hizo kwa kuwa wakiacha, wanahatarisha maisha yao.

Mwenyeki Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk Fatma Mrisho aliwaambia waandishi wa habari jana katika mkutano wa kupitia mapendekezo ya kitaalamu na maboresho ya sera na huduma za UKIMWI nchini na kuongeza kuwa hatua kali dhidi ya wahujumu hao zinatakiwa.

“Jamii yenyewe inawaendekeza hao wanaojitangazia tiba, kwanza wanakwenda kinyume na Sheria ya UKIMWI ya mwaka 2008, wanafifisha mapambano, mpaka sasa hakuna tiba ya Ukimwi bali kuna dawa za kupunguza kasi ya kuzaliana virusi, wanaojitangazia tiba wanapaswa kushitakiwa,” alisema Dk Mrisho.

Aliwatahadharisha watumiaji wa ARVs kutoacha kutumia dawa hizo kwa vigezo vya kuwepo kwa tiba na kuwashauri wanaodhani wana tiba, waende Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuthibitisha tiba zao.

Kuhusu mkutano huo, Dkt. Mrisho alisema lengo lake ni kuongeza kasi ya mapambano ambayo imefanikiwa katika Mpango wa Maendeleo ya Sekta wa miaka miwili uliomalizika mwaka huu na mkakati mpya wa kitaifa wa miaka mitano (2013-2017) ili kudhibiti maambukizi mapya.

Awali Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa TACAIDS, Dk Raphael Kalinga alisema takwimu zinaonesha kwa sasa maambukizi kitaifa ni asilimia 5.7  kutoka 7.5 na mpango ni kuwa na sifuri tatu ambazo ni kusiwe na maambukizi mapya, kusiwe na vifo na kusiwe na unyanyapaa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Vitalis Makayula akizungumzia maboresho, huduma na changamoto za mapambano ya UKIMWI nchini, alishauri serikali kuendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa na kuiomba jamii kupinga unyanyapaa kwa wenye VVU.

“Naomba jamii ifahamu kwamba Ukwimi hauna tiba mpaka sasa, viongozi wa dini wasaidie hili, tusipotoshe umma kuhusu tiba bali tueleze ukweli ili watu wajilinde,” alisema Makayula.

Awali akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo alitaka taasisi zinazopambana na ugonjwa huo kutumia rasilimali ndogo zilizopo vizuri badala ya kubaki kulalamika kila siku kuwa ni finyu.

Lyimo aliwasihi vijana, ambao wanashambuliwa zaidi na ugonjwa huo, kubadili tabia na kutambua kuwa tiba ya kisayansi dhidi ya ugonjwa huo haipo hivyo wajitunze na wasaidiwe kujilinda.


Source: http://www.wavuti.com/#ixzz2C4iGh4ep

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA