Majina ya waliofariki kwenye ajali ya boti ziwa Tanganyika Januari 2013


IMETHIBITIKA kuwa watu tisa wamekufa na wengine 12 hawajulikani waliko huku wengine 64 wakiokolewa baada ya boti ya abiria waliyokuwa wakisafiria katika Ziwa Tanganyika kuzama baada ya kukumbwa na dhoruba.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Fraiser Kashai aliyekwenda eneo la tukio, alithibitisha jana kwamba boti hiyo iitwayo Tunusuru Yarabi iliyokuwa ikitoka Kirando, Rukwa kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Rumonge, Burundi, ilikuwa na shehena ya dagaa, vyakula na bidhaa za viwandani.

Kamanda Kashai alisema hadi jana mchana miili ya watu wanane kati ya tisa iliyokuwa imeopolewa ilikuwa imetambuliwa na kati yao, saba ikiwa ya wanawake na miwili ya watoto wa kiume ambayo imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa ya Maweni.

Aliwataja marehemu hao kuwa ni: Shani Baba wa Kirand, Mzinga Kandoro, Mwalimu wa Shule ya Msingi Filbert Bayi ya Dar es Salaam, Wamjini kutoka Burundi na Sarah Joseph wa Karundu, Nkasi, Rukwa. Wengine ni Nuru Hassan wa Kirando, Rukwa; Sewa Seba wa Karungu, Rukwa; Shadrack Amnyasi wa Malindi, Rukwa, na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Asha. Mwingine hakuwa ametambuliwa hadi jana.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kigoma chini ya Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya, nahodha wa boti hiyo Akilimali Seif na baadhi ya abiria walionusurika ajalini, walisema boti hiyo ilizama baada ya kupigwa na wimbi kali ikapasuka na kuzama.

Nahodha huyo alisema boti yake haikuwa na hitilafu za kiufundi au mbovu, bali wimbi kubwa walilokumbana nalo ndilo lilisababisha kuzama na kusababisha vifo hivyo.

Alisema baada ya kupigwa na wimbi la kwanza, injini ilizima na wakati akifanya jitihada za kuwasha mashine nyingine alizidi kupigwa na dhoruba na ikapasuka vipande na kuzama.

Baadhi ya abiria walionusurika waliokuwa wakisafiri kwa boti hiyo, Mariam Saidi na Mohammed Shaaban walisema pamoja na dhoruba kusababisha ajali hiyo, shehena kubwa ya vitu mbalimbali vilivyokuwa vimebebwa katika boti hiyo vilichangia kuzama.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Herembe, Jack Mpapi alisema jitihada za wananchi wa kijiji hicho katika uokoaji hazikufanikiwa kutokana na hali mbaya ya hewa na mawimbi makubwa yaliyokuwa ziwani wakati huo.

Machibya na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wilaya ambao walifika eneo la tukio walitoa pole kwa walionusurika katika ajali hiyo.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa alilaumu upakiaji wa mizigo kupita kiasi unaofanywa na boti hizo na inapotokea dhoruba inakuwa kazi kubwa kuokoka.

---
Taarifa kwa mujibu wa gazeti la HabariLeo


Source: http://www.wavuti.com/#ixzz2HAZ9lSEp

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA