MAKALA: TABIA ZINAZOWEZA KUKUFANYA UFANIKIWE


Watu wote wanapenda kufanikiwa maishani haijalishi ni wa umri gani, anatokea wapi, anafanya nini kujipatia kipato. Kila mmoja amebeba maana tofauti ya “mafanikio” kuna ambao huelezea mafanikio ni kuoa/kuolewa na mtu muaminifu anaejali familia na watoto, wakati wengine wanaona mafanikio ni kuwa na Mali, Mamlaka/Madaraka na Kujulikana. 

Wote tunataka kufanikiwa ili tuishi maisha ya furaha na Amani, Uhuru wa Kiuchumi, kuendesha magari mazuri, kuishi nyumba nzuri n.k ingawa mafanikio haya tunayoyatamani tutayapata lakini hayatakuja kirahisi, tunahitaji kuweka juhudi katika shughuli zetu za kila siku pia tunatakiwa tutambue tabia ambazo zitatufikisha kwenye mafanikio tunayoyataka:-

      Nguvu ya Fikra
Tunatambua kwamba tunaishi maisha ya kuchagua, kuamua na kupanga. Chaguzi hizo mara nyingi zinatoka katika mawazo yetu. Watu waliofanikiwa hufikiri vyema na kupanga vyema kutokana na mawazo yao. Ili tuweze kufanikiwa ni vyema kujua namna ya kutawala fikra zetu, tufanye chambuzi yakinifu katika fikra zetu, tuwe makini na fikra zetu. Kuna msemo unaosema “Aliwazalo mtu ndilo linalomtokea” mara nyingi wanatumia Aliwazalo “mjinga”kwa maana kwamba unapojiwazia mabaya basi wewe ni mjinga na fikra hizo hizo zitakutokea. Hivyo basi kwa mjasiriamali unayetaka kufanikiwa hakikisha unatawala fikra zako kwa mawazo mazuri, iwazie mema biashara yako, wawazie mema wateja wako. Ukiwaza kudhurumiwa basi itakuwa kwasababu hautachukua hatua za kuhakikisha unalipwa deni lako, ukiwaza kushindwa katika biashara au na washindani wako ndivyo itakuwa kwani hautaweka fikra nzuri za kuhakikisha unapata mbinu bora za kuleta ushindani na mafanikio.

      Jiwekee Malengo na uyatimize
Unaweza kujiwekea malengo ya muda mrefu au ya muda mfupi, yaandike malengo yako sehemu nzuri kwa ajili ya ufatiliaji wa mara kwa mara. 

Hakikisha unafatilia kutimiza malengo yako, kila lengo ulilojiwekea hakikisha linatimia katika muda uliojiwekea, weka mikakati itakayosaidia kuhakikisha unatimiza lengo lako. Mfano:-Unataka kufungua tawi linguine kwa ajili ya biashara yako, orodhesha lengo hilo na muda unaotaka litimie, likifuatiwa na mikakati kuhakikisha lengo hilo linakamilika na kila mkakati utatumia muda gani na nani atakaehusika kuhakikisha huo mkakati unakamilika. 

Lengo hilo litakapotimia unaweza kuweka alama ya vema, na kama halitatimia basi inabidi uangalie upya ni nini kimekwamisha lengo hilo kutimia na uanze upya tena. Usijiwekee malengo usiyoweza kuyatimiza. Jifunze kusimamia malengo yako usiyumbishwe na maneno au mitazamo ya watu wengine juu ya malengo yako.

      Kuwa na Imani juu ya Ndoto zako
Watu waliofanikiwa wanaimani kubwa, wanaamini kila jambo wanalotarajia katika maisha yao linawezekana. Haijalishi watu wengine watasema nini au wana mtazamo gani au kuna changamoto gani zinazohusiana na ndoto yako, 

kikubwa ni kuweka imani katika ndoto hiyo kwamba itawezekana. Imani hii inaenda na matendo huwezi kuamini huku ukikaa kusubiri muujiza unaamini huku ukitafuta namna ya kuweza kuikamilisha ndoto yako. Tukumbuke kwamba hata simu tunazotumia leo hii, zilianza na wazo na ndoto za mtu alieamini kuwa siku moja itakuwa, lakini mtu huyu hakukaa kusubiri muujiza alitia juhudi kuhakikisha anachokiamini kinafanikiwa.

     Chukua Hatua
Ukiwa na ndoto bila matendo ni sawa na kazi bure, ni sawa na kuwa na gari huku haujui kuendesha na wala hauna dereva. Watu waliofanikiwa wanafanyia kazi ndoto zao, japo tunasisitiza kuwa na imani na ndoto yako ili ifanikiwe lakini hakuna kitu kitatokea kwa miujiza “Imani bila matendo ni kazi bure” watu wanaofanikiwa/waliofanikiwa hawaachi muda wao upotee bure bila kutenda jambo. 

Hawasubiri kesho ndio waanze kutenda, muda sahihi wa kutenda ni sasa na sio baadae. Kama wewe una ndoto ya kuwa Daktari ni lazima uifanyie kazi ndoto yako itimie kwa kuhakikisha unasoma kwa bidii na unafanyia bidii zaidi masomo ya sayansi ili yaweze kukufikisha kwenye ndoto yako.Huwezi kusema unataka kuwa Mfanyabiashara na wakati haufanyi juhudi hata za kuanzisha biashara unayoiota, 
hakuna mtu atakae kutimizia ndoto zako ni wewe mwenyewe unapaswa kuchukua hatua kuhakikisha unatimiza ndoto yako, hao watu wengine ni kukusaidia ushauri na misaada mbalimbali lakini msukumo unapaswa kuwa nao wewe na mtendaji mkuu ni wewe.

    Tumia muda wako vizuri
Watu wanaofanikiwa wanajua wakati ni mali. Muda unaopotea unalinganishwa na Uhai/Maisha kupotea. Kwa mtu anaetaka kufanikiwa ni vyema katambua umuhimu wa kupanga vipaumbele kwa majukumu yako. Tambua ni kipi kianze na kipi kifatie. Mara nyingi watu hulalamika kuwa muda hautoshi, lakini hatuwezi kuongeza muda kwa sababu Mungu ametupa masaa 24 kwa siku, Hivyo ni vizuri tutumie vizuri muda tuliopewa. Tunaweza kupanga vipaumbele vya shughuli zetu kwa kuangalia jedwali lifuatalo:

1.    Haraka na muhimu
Msiba, Ugonjwa,Ajali,Ukosefu wa Chakula,Ukosefu wa maji,Kufukuzwa mtoto shule n.k
2.    Muhimu si haraka
Kuzaa, kuoa/kuolewa, kusoma majarida n.k
3.    Haraka si muhimu
Kupiga na kupokea simu, kutuma ujumbe mfupi katika simu, kuingia facebook na instagrama, kuongea mambo ya watu wengine n.k
4.    Si muhimu Si haraka
Kumsubiri rafiki kwa masaa zaidi ya matatu kituoni, kuangalia picha za ngono mitandaoni, kusoma udaku, kuangalia tv kwa masaa mengi n.k
Hamua vyema shughuli zako za siku ili usipoteze wakati.
6.    
        Endelea Kujifunza
Watu wengi huacha kujifunza pale tu wanapomaliza masomo au mafunzo maalumu wakiamini kile walichokipata kinawatosheleza maisha yao yote. Ili uweze kufanikiwa penda kujifunza zaidi na zaidi. Watu waliofanikiwa wanajifunza kila siku kwa kusoma vitabu, kuhudhuria semina mbalimbali ili kujifunza mambo mapya yanayoendelea ulimwenguni hasa katika fani zao husika. 

Kwa unaependa kufanikiwa unaweza kufata tabia hizo, pia jifunze kuuliza maswali yenye kukujenga, jifunze kutoka kwa waliofanikiwa, soma historia zao na jinsi gani waliweza kufanikiwa ukiweza hata unaweza kuwaona ili uweze kujifunza kwa matendo kutoka kwao. 

Tumia mitandao ya kijamii vizuri kupata mambo mapya ya yanayoendelea katika kitu unachokifanya mfano: biashara ya magari, tafuta habari za magari mapya, gari gani lina mwendo kasi zaidi, bei zake nchini na nje ya nchi, gari gani halitumii mafuta zaidi kulingana na kipato cha mteja wako na mengine kadha wa kadha yanayoendana na shughuli unayoifanya, hii itakusaidia kuwa na taarifa zilizo sahihi na zenye kwenda na wakati halisi pia kumsaidia mteja wako kufanya maamuzi sahihi ya gari gani anunue kulingana na uchumi wake na mazingira aliyopo n.k.

    Mabadiliko huletwa na wewe mwenyewe.
Hakuna mtu anaeweza kukuletea mabadiliko, Kamwe usitarajie kwamba mafanikio ya maisha yako yataletwa na mtu mwingine,Sio mwanasiasa, mchungaji, mume/mke au watoto watakaokuletea mabadiliko bali wewe mwenyewe. (Changes begins with you) Ukijitambua na ukalitambua hilo basi utafanya juhudi binafsi ili kuleta mabadiliko unayoyataka katika maisha yako, kama unataka mabadiliko ya kiuchumi ni vyema ukachukua hatua binafsi kuhakikisha unafanya kazi kwa bidii, unafanya biashara kwa ufanisi ili kupata mabadiliko ya kiuchumi. 

Ukisubili mpaka uoe/uolewe, uajiliwe,mwanasiasa fulani arudi madarakani, mama apate kifuta jasho au mjomba akupe mtaji unajidanganya. Anza kuonesha mabadiliko mwenyewe hao watakukuta mbele ya safari kujazia pale utakapokwama, ndo maana hata benki hupewi mkopo kuanzisha biashara wanatoa mkopo kwa yule aliekwisha anza, Kama unataka kufanikiwa ni vyema kutumia msukumo wako wa ndani kufanya mabadiliko. Fikiri upya juu ya maisha yako katika mtazamo mpya na wa utofauti, utafika mbali.

    Epuka Uadui
Ili uweze kuwa mwenye mafanikio ni vyema kujenga urafiki na kila mtu (haimaanishi awe karibu yako) ila tu asiwe adui yako. Tunaona watu wengi wanashindwa kufanikiwa tu ni kwasababu anaweka uadui na watu wanaomzunguka. Jifunze kuishi na watu vizuri, watu hao hao unaoweka nao uadui ndio siku moja unataka wawe wateja wako, sasa kama hauna urafiki nao hata kama unauza bidhaa nzuri hawataweza kukuchangia kwa vile wewe ni adui yao. 

Kuna watu wengine ni wakorofi, wabishi, wanamatusi na ni ngumu kuishi nao katika jamii lakini haimaanishi na wewe uwe kama wao kwa sababu tu wanakuonesha tabia hizo. Katika kuweka uadui na watu kunaweza kuathiri maendelea yako hasa katika “maneno” hasa mabaya, maneno mabaya husambaa haraka na hivyo kuweza kuathiri biashara yako, mahusiano yako au hata sifa yako katika jamii na hivyo inakufanya usifanikiwe kwa sababu watu watakudharau au kukuweka chini kwa maneno yatakayoongelewa juu yako.

Kitu muhimu katika kufatilia tabia hizi ili kufanikia cha msingi kuliko yote ni “KUJITAMBUA”, Kujitambua ni kitu cha msingi katika kutafuta mafanikio yako. Pia ni vyema kutambua kwamba wewe unawajibika  katika maisha ya wengine na usisahau unawajibika katika maisha yako peke yako, ukitambua wajibu wako hautapoteza muda katika kutafuta mafanikio yako. 

Pia ni vyema kujiandaa kupokea yasiyotarajiwa katika maisha kama kukatishwa tamaa, kutofanikiwa haraka, kufirisika n.k lakini usiwape watu nafasi watu kukugandamiza katika yale ambayo hukutarajia kuyapitia nyanyuka chukua hatua na usonge mbele. Siku zote jiweke juu ya kiwango kinachotakiwa, washindwa washindani wako na utakapokuwa juu yao usiache ushindani shindana na wewe mwenyewe ili kulinda nafasi yako ya mafanikio.

Imeandaliwa na:
Nyakainja Manyama
TAPBDS Social & Business Consultant

Tell: 0652048022

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA