MAKALA MAALUM KUTOKA KWA MDAU KUHUSU MIFUKO YA JAMII
IMEANDALIWA NA
Davis
Muzahula,
Mwanafunzi
wa shahada ya kwanza ya sheria (mwaka wa nne),
Chuo
Kikuu Cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania
Simu:
+255756829416
Barua
pepe: davismuzahula@yahoo.com
UTANGULIZI
Kwa
mujibu wa Shirika la Kazi Duniani, Mfuko wa hifadhi ya jamii ni mfumo ambao
jamii husika imejiwekea kwa lengo la kuwakinga watumishi wa umma au binafsi (waajiriwa) dhidi ya matukio yasiyotarajiwa
(Contingencies). Matukio hayo ni kama
maradhi, ulemavu, kupoteza kazi, kuacha kazi kwa sababu ya uzee (kustaafu) aidha kwa hiari au kwa lazima,
na mengineyo ikiwamo huduma za matibabu, ghalama za msiba ikiwa mteja atafariki
au kufiwa na mtu ambaye mfuko husika huchangia. Vile vile iwapo mteja atafariki
kabla ya kustaafu basi mafao yake hulipwa kwa warithi wake ambavyo huweza kusaidia
kusomesha watoto wa mhusika.
Hifadhi
kutoka kwa jamii ni haki ya kila mtu kama ilivyotajwa na katiba ya jamhuri ya
Muungao wa Tanzania, 1977 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara) katika
ibara ya 11, ibara ndogo ya (1) kwamba:
“Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu
unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekerezaji wa haki ya mtu kufanya kazi,
haki ya kupata elimu na haki ya kupata msaada kutoka kwa jamii wakati wa
uzee, maradhi au hali ya ulemavu, na katika hali nyinginezo za mtu kuwa
hajiwezi...”
Hivyo
hivyo, ndivyo inavyotaja ibara ya 22 ya Tamko la Ulimwengu la haki za Binadamu
la mwaka 1948, ambayo pia inataja kuwa ni haki kwa kila mtu kupata hifadhi ya
kijamii kupitia utaratibu uliowekwa.
KWA
NINI KUNA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
Kutokana
na hali ya maisha kutotabilika, wafanyakazi wengi hujikuta wakiishi maisha
magumu mara baada ya kumaliza muda wao wa utumishi (kustaafu). Lakini pia hata kabla ya kustaafu, wafanyakazi hujikuta
wakipitia hali ngumu za maisha kutokana na maradhi au ulemavu ambavyo huweza
kusababisha kupungukiwa au kukosa kabisa kipato hivyo kushindwa kumudu ghalama
za matibabu na za kimaisha kwa ujumla. Hiki ndicho kipindi ambacho umuhimu wa
Mifuko ya hifadhi ya jamii huja, kwani baada ya kuridhika kuwa mteja anastahiri
huduma kutoka kwenye mfuko husika, huweza kupatiwa ghalama za matibabu na
matunzo kutoka katika mfuko huo kulingana na taratibu zilizowekwa. Ila
inatakiwa iwe imetajwa kuwa mfuko husika hutoa huduma husika na mteja amekidhi
sifa za kupata huduma hiyo (pensionable
fund) kwa maana ya kutabulika kama mteja na kuchangia kwa utaratibu
uliowekwa.
WAKATI
AMBAO MTU ANAWEZA KUPATA MAFAO YAKE AU HUDUMA KUTOKA KWENYE MFUKO HUSIKA
Ifahamike
kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ni maalum kwa ajili ya kumsaidia
mfanyakazi kumudu mahitaji yake ya
uzeeni pindi anapostaafu kama si mahitaji mengine yaliyotajwa hapo mwanzo. Sababu kubwa iliyopelekea kuwepo kwa mifuko
wa hifadhi ya jamii ni baada ya kubainika kuwa wakati wa ujana, wafanyakazi
wengi hushindwa kujiwekea akiba ya kutosha kukidhi mahitaji yao ya uzeeni au
kumudu ghalama za maisha yao pindi itokeapo hali yoyote ya kutojiweza.
Tofauti
na benki au taasisi nyingine za kifedha, mifuko ya hifadhi ya jamii hutoa mafao
kwa mteja wake pindi awapo na uhitaji wa kidharula (mfano: Maradhi, ulemavu au hali nyingine ya kutojiweza ), au
kustaafu kazi kwa misingi ya uzee kwa mujibu wa sera za kazi na utumishi na si
vinginevyo. Kwa mantiki hiyo mteja wa mfuko husika hawezi kudai mafao yake kwa
misingi yoyote ile tofauti na ile iliyowekwa na mfuko husika (mfano: kuhitaji pesa kwa ajili ya kuanzisha
biashara, kununua vyombo vya starehe kama gari, pikipiki na vinginevyo) kama
kustaafu kazi au kupoteza kazi. Kwa hiyo bila uhitaji wa namna hiyo mteja hawezi
kulipwa mafao yake ya aina yoyote ile mpaka pale atakapofikia umri wa kustaafu
aidha kwa hiari au kwa lazima ambao kwa Tanzania ni miaka 55 hadi 60, mtawalia*.
Mifuko
ya ifadhi ya jamii ni kama ilivyo sera ya bima yaani mtu hulipwa pale
anapopatwa na janga, na ni mahususi kumsaidia mfanyakazi kununua vitu vya
thamani kama vile viwanja au kujenga nyumba anapostaafu au anapoelekea
kustaafu. Kwa hiyo, hiyo ndiyo maana halisi na lengo la mifuko ya hifadhi ya
jamii.
Kabla
ya kuhitimisha makala hii, tukizungumzia kidogo kuhusu pensheni ambayo
hujulikana kama (Kiinua mgongo), ni
kiasi cha pesa ambacho hulipwa na
serikali au kampuni binafsi kwa mtu ambaye ameacha kufanya kazi kwa sababu ya
uzee au maradhi. Kwa maana hiyo mtu hawezi kupata pensheni mpaka ule umri wa kustaafu
ambao umewekwa na serikali (miaka 60).
Ieleweke na ndivyo ilivyo, ya kwamba mtu hawezi kupewa pensheni katika umri wowote tofauti na umri uliotajwa
kuwa ni umri wa kustaafu kwa lengo la kufanya biashara au kwa ajili ya lengo
jingine lolote lile. Hii ni kwa sababu hela ya mteja husika hutumika kuanzisha
vitega uchumi na taasisi husika na ndio maana mteja hupata mafao manono zaidi
kuliko alivyochangia. Hii ni kama alivyo wahi kusema Mheshimiwa Irene
Isiaaka ambaye ni mkurugenzi mkuu wa mamlaka
ya udhiti wa mifuko ya hifadhi ya jamii (SSRA),
kuzitaka taasisi za mifuko ya hifadhi ya jamii kubuni miradi endelevu na
kuanzisha vitega uchumi mbalimbali ili kuziwezesha taasisi hizo kutoa huduma
bora kwa wateja wake. Hii ndio sababu kubwa ambayo huipasa mifuko ya hifadhi ya
jamii kukaa na pesa za wateja wake kwa mda mrefu zaidi ili kuwa na uhakika wa
mafao bora wakati ambapo mteja huacha
kuchangia kwa sababu ya kuacha kulipwa mshahara na badala yake kuanza
kulipwa mafao yake na mfuko husika kutokana na uzalishaji wa hela yake.
Ni
muhimu kutoa pongezi kwa mamalaka ya udhibiti wa mifuko ya hifadhi ya jamii kwa
kutoa nafasi kwa wafanyakazi wanaokaribia kustaafu kupata sehemu ya pensheni
zao kupitia sheria iliyopitishwa na bunge mwezi April mwaka 2012. Nafasi hiyo
itawapa watumishi wa umma uwezo wa kujiandalia mazingira mazuri ya kustaafu
ikiwa ni pamoja na kukununua viwanja, kujenga nyumba bora za kuishi na
kusomesha watoto wao.
Napenda
pia kuonesha kusikitishwa kwangu na watu wanaobeza hatua hiyo iliyofikiwa na mamlaka ya udhibiti
wa mifuko wa hifadhi ya jamii, huku wakidai ya kuwa umri wa miaka 55 hadi 60 ni
mkubwa na kuwa una dalili za kibaguzi hivyo kuwa kinyume na haki za binadamu.
Naweza kusema ya kuwa ni kuhoji mambo tusiyoyafahamu yanaendaje napengine kuigiza
siasa hata kwenye mambo ambayo si ya kisiasa ambavyo ni hatari kwa maendeleo ya
jamii yetu. Zaidi natambua kuwa wamo wanasheria na mashirika ya kutetea haki za
binadamu wanaopanga kuzuia sheria hiyo kwa kigezo cha umri wa pensheni kuwa
mkubwa. Ningependa kuwakumbusha kwamba penshion siyo mshahara, siyo mkopo na
wala sio kama pesa iliyowekwa benki kwamba mtu anaweza kuidai pindi
anapojisikia, kufanya hivyo ni kopotosha maana halisi ya dhana ya pensheni ambayo
hata kamusi zote zinalitaja kuwa ni mafao ya uzeeni baada ya kuacha kazi,
kupatwa na maradhi au kupata kilema kiasi cha kushindwa kuendelea na kazi
ambazo ndio sifa za mtu kupata pensheni (pensionable)
na si vinginevyo.
Ushauri
wangu ni kwamba kama kuna mtu anahisi kuwa umri uliowekwa kwa mtu kupata
pensheni ni mkubwa aombe serikali kubadili sera ya umri wa kustaafu na si
kubadili maana ya pensheni kuwa kama mishaara au mifuko ya hifadhi ya jamii
kuwa kama benki. Ijulikane kuwa ndio maana kuna benki na kuna mifuko ya hifadhi
ya jamii.
HITIMISHO
Ni
muhimu tukielewa kuwa kulalamika pale tunapohisi kuwa haututendewi haki ni haki
ya kila mmoja wetu kama watanzania. Lakini ni muhimu kuelewa na hata kutafuta
kuelewa jambo ambalo hatulielewi vizuri. Hii itatusaidia kujikosoa pale
tunapojikuta kuwa jinsi tulivyoelewa jambo ni tofauti na uhalisia wa jambo
husika na si kukimbilia kulalamika kwa ushabiki wa kisiasa kwa mambo
yasiyostaili kuingiziwa siasa. Mamlaka za mifuko ya hifadhi ya jamii ziandae
elimu maalum kwa ajili ya wadau wake ili kuwawezesha kufahamu mfumo na jinsi
mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii invyofanya kazi. Hii itaondoa malalamiko yasiyo
ya lazima kutokana na kutofahamu jinsi mifuko hii inavyotoa huduma zake.
Natanguliza
shukrani
*Mtawalia:
maana yake- Respectively- a kufuatana katika mpangilio
Davis
Muzahula,
Mwanafunzi
wa shahada ya kwanza ya sheria (mwaka wa nne),
Chuo
Kikuu Cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania
Simu:
+255756829416
Barua
pepe: davismuzahula@yahoo.com
Comments
Post a Comment