ALICHOKISEMA FID Q TZ HipHop!



Fid Q.

Miaka 11 ya “FidQ.com”
Kitu chochote kile kinaweza kuchukuliwa kama kazi ya sanaa, ila inategemea mtazamo wa hadhira ukoje juu ya kitu au kazi husika. Kwa upande mwingine, historia — hasa za jamii au vikundi vya jamii vilivyokuwa na vinavyoendelea kukandamizwa kwa namna moja au nyingine — husema vingine.
Sanaa imekuwa ni mojawapo ya zana zinazotumiwa kufungua macho na fikra za watu kwenye jamii mbalimbali, katika vipindi tofauti. Mfano mzuri ni ndugu zetu wa Afrika Kusini. Wakati wa utawala wa kibaguzi (herufi ndogo zimetumiwa kwa makusudi), watu waliokuwa wanaangaliwa kama viongozi walikuwa hawaruhusiwi kukutana au kuongea na mtu zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja. Lakini harakati zao hazikugota; waligeukia sanaa — wakatumia kazi za sanaa kuamsha watu.
Kwa hapa nyumbani, historia sio tofauti sana. Wazazi wetu waliokuwa kwenye harakati za kuusaka Uhuru walitumia mpaka ngonjera za mashuleni kuwasilisha sera za TANU, ASP na vyama vingine vya siasa.
Kizazi chetu, cha vijana wa sasa, kina changamoto zake. Na bahati nzuri Fid Q analitambua hilo. Yeye aliamua kutumia sanaa kuwaamsha vijana, tangu alipoingia kwenye Hip Hop takribani miaka 15 iliyopita.
Tulifanikiwa kulonga naye, na hakusita kuongelea jinsi alivyoanza, kazi zake kwa ujumla na mipango yake ya hapo baadae.
1. Miaka 11 tokea mitaa izinduliwe na ‘FidQ dot com’, na bila shaka unaipa ‘dot com’ uzito na heshima ya kipekee. Kwa nini hasa — ni sababu binafsi tu au kuna zaidi?
‘Fid Q dot com’ ni wimbo ambao ulinifungulia njia kwa roho safi na kunifanya nipewe heshima iliyoniendeleza mpaka hapa nilipo. Kabla ya ‘Fid Q dot com’ nilitoa ‘Huyu na Yule’ ambayo nilimshirikisha Mr. Paul na Squeezer, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama nitasita kusema hii ilinitambulisha vyema kwenye medani ya muziki wetu.
Tofauti iliyopo kati ya ‘dot com’ na ‘Huyu na Yule’ ni kuwa, ‘dot com’ ilikuwa ni kama kitu kipya zaidi masikioni mwa watu, na kitu kipya mara zote husisimua! Ni wimbo ambao nitatumbuiza kwenye tamasha la kesho na kesho kutwa, na bado watu wakaruka nayo utadhani imetoka jana tu. Ngoma hii ilinipa, na bado inanipa, heshima kwa wapenzi wa muziki, hata emcees niliowakuta na mpaka waliofuatia…  Ni moja kati ya nyimbo chache ambazo zimebahatika kutochuja, na kama tukisema zinazeeka basi sio vibaya kama nikiifananisha na muwa. Namaanisha, itazeeka na utamu wake. Ninasherehekea miaka 11 ili kuwakumbusha wasanii wenzangu tofauti iliyopo kati ya “bubble-gum music”… na “pure music”!
2. Una zaidi ya mlongo mmoja kwenye gemu, na inaonekana kadri muda unavyozidi kwenda unazidi kupata watu wanaokutegea sikio. Kwa kuwa wasanii chipukizi, hasa wa Hip Hop, wanajaribu kufuata nyayo zako, una lipi la kuwashauri?
Siku zote mi’ hupenda kuwaambia wasijaribu kuwa mimi, kwa sababu hata hapa nilipo sipo ninapohitaji kubakia. Na kinachonifanya niendelee kuwepo ni kile kiburi changu cha kutohofia kupitwa ilimradi muda usiniache! Na pia Paul Robeson ameshawahi kunena haya: “Sanaa kazi yake si kuonesha tu hali ya dunia ilivyo sasa tu; bali inavyopaswa kuwa na itakavyokuwa baadae.”
Sababu hiyo ya msingi imenipelekea kuamini ya kwamba wanamuziki na wasanii wote kwa ujumla tuna jukumu la kuwa wajenzi wa ‘kesho njema’ kuliko hata wanaotutawala.

3. Changamoto zipi hasa ulikutana nazo wakati ndio kwanza unaingia kwenye gemu? 
Nilianza kisirisiri kwa kuwa mama’angu hakupenda niwe mwanamuziki. Nilipopata ruksa ya kutembelea studio nilikutana na vikwazo ambavyo kila msanii anayefanya hip hop yenyewe lazima atakuwa ameshakutana navyo. Vikwazo hivyo ni pamoja na kuambiwa ‘upunguze ukali wa maneno au kufanya mashairi mepesi yasiyoumiza vichwa vya wasikilizaji’.
Kwa kweli, kwa kupitia vipingamizi hivi, nilijifunza uandishi fulani hivi. Yaani kwa mfano hata kama ninakosoa jambo fulani, nitahakikisha linaruka kwa kasi ya kifaru aliyejeruiwa lakini linatua kiulaini kama sponji! Ndio maana naweza nikatoka na ngoma inayoongelea ‘matatizo’ na bado watu wakaiimba na kucheza wakiwa vilabuni na kwenye madisko mbalimbali.
4. Katika tungo ulizoandika, hebu tuambie nyimbo tatu ambazo zina sehemu ya pekee kwenye moyo na fikra zako…
Najua wengi watashangaa, lakini ile siku niliyosikia mama yangu mzazi akisema anaipenda ‘Usinikubali Haraka’ ilinilazimu nitenge masaa matatu ya kujiuliza nilifikiria nini mpaka nikaandika ule wimbo? Na pili, je ni kweli mama yangu kaliona hilo? Unajua siku zote unapofanya kazi yenye malengo ya kuigusa dunia, huwa inafikia kipindi ile dunia nayo huwa inataka kukugusa wewe mhusika mkuu.
Fid Q ni msanii kama wasanii wengine, hivyo na mimi huwa nakutana na mikasa mbalimbali katika maisha, lakini pale linapokuja suala la kutafuta mwenza wa kuishi naye kwenye raha na shida, ndipo huwa najikuta “nina-moonwalk”… Kwa kuwa tuna tabia ya kuhukumu vitu kama tulivyo na sio kama vilivyo, hivyo basi nimegundua hiyo tabia ipo kwenye mapenzi pia. Hawakupendi for who you are but for what you are. Na hicho kinapelekea wapendanao wengi kuuziana kanyaboya. Nilitaka tukumbushane ule msemo wa haraka haraka haina baraka, ili muda zaidi upate kutengwa kwa ajili ya kitu chenye manufaa.
Wimbo wa pili ni Propaganda… hili wazo liliniijia baada ya kughairi kutoka na Darwin’s Naitmea, na nilipenda kwa jinsi nilivyoweza kucheza karibu na mada ya kwanza kabisa.
Wa tatu ni Fei. Ukiusikiliza vizuri utagundua upendo nilionao juu ya mwanangu, na pia historia fupi ya mahusiano yaliyopo kati yangu na baba yangu mzazi.
5. Ndani ya hiyo miaka 10 au 11, tumeona wasanii wa Hip Hop wakibadili mwelekeo na wengine kufikia hata hatua ya kukacha (Hip Hop) kabisa na kufanya aina nyingine za sanaa. Lakini wewe umeendelea kuwepo na kukua. Nini mtazamo wako na maoni yako? 
Maslahi ndio kitu pekee kinachowaumiza watu wengi lakini kama alivyosema Hasan Salaam kwenye FidStyle Friday, ‘Its one thing to live for the cause and another to die for it.’
6. Ukiangalia mwelekeo wa Hip Hop ya Bongo, unadhani miaka 10 ijayo itakuwaje, au ungependa iweje? 
Miaka kumi ijayo hip hop ya Bongo itakuwa kubwa zaidi ya vile ilivyo hivi sasa, na ningependa ipewe kipaumbele zaidi kwa sababu ni hii hii hip hop ndio ina uwezo wa kupunguza au kuondoa ujinga kwa asilimia 50 au hata 70, kama wanafunzi walioko mashuleni wataendelea kulega kwenye masomo yao ya kila siku.
7. Vipi upande wa albamu, una mbili tu sokoni. Huoni kama unawanyima vitu mashabiki wako?
Unajua album mimi huwa naichukulia kama “audio book”… Yaani sio suala la ku-compile au kukusanya nyimbo tu.
Kinachotokea mara nyingi sana ni hiki; unakuta mtu anatoka na album, ngoma ya kwanza inasema ‘Umeniacha’, ya pili ‘Sikutaki Tena’ ya tatu ‘Nataka Mpenzi’, ya nne ‘Unanichosha’. Halafu unakuta album labda inaitwa ‘Toba’!… Ha ha ha! Hapo unakua unachanganya madawa mzee!
8. KitaaOLOJIA tuitegemee lini? Unafikiri soko la Tanzania lipo tayari kuipokea? 
KitaaOLOJIA is the completion of the tril (triology)… Yaani kuanzia album ya kwanza ambayo ni ‘Vina Mwanzo Kati na Mwisho’ na ya pili ambayo ni ‘Propaganda’, sasa Kitaa inakuja kukamilisha ule uprofesa wangu wa chuo kikuu cha ghetto, kwa kuwaletea simulizi na mafunzo niliyokutana nayo mitaani… kwa kupitia mambo yaliyonipatia uzoefu katika maisha yangu binafsi. Natarajia kuipakua Aug 13.
Naaam, soko la Bongo lipo tayari na lishakaa mkao wa kula.
9. Upande wa mradi wa CheusiDawaTV, inaoenekana imepokelewa vizuri ila watu wamekuwa wakiuliza kunani sasa hivi, mbona kimya. Kuna mikakati au mambo yanayoendelea nyuma ya pazia? 
FidStyle Friday itaanza kurushwa kwenye kituo kimoja cha televisheni hapa nyumbani. Na pia tupo katika maongezi na mmiliki mmoja wa televisheni ya kujitegemea iliyopo Ujerumani kwa kuwa hata na wao wamevutiwa na yaliyomo kwenye FidStyle Friday na wapo tayari ku-join the revolution.
10. Kuna lolote unalotaka kuwaambia mashabiki wako na Hip Hop kwa ujumla? 
Waendelee kusikiliza kwa umakini, wawe wadadisi ikiwezekana wafanye utafiti wa kila kauli itakayowavutia kwenye tungo za hip hop kwa sababu hiyo ndio njia pekee ya ku-relate kwa sauti na sense.
11. Kwa kumalizia, tupe Top 5 emcees (wako) kutoka Bongo. Na kwa nini hao watano!?
1. Prof. J… Mpaka leo bado ninajivunia kununua ile album yake ya ‘Machozi, Jasho na Damu‘. Huwa hainichoshi kuisikiliza na nimeridhika nayo kabisa. Kiasi kwamba huwa sioni kama jamaa anakosea kwa kunata kwenye midundo ya kapuka na mingineyo. Tayari ameshaachia classic, mwacheni akusanye senti zake!
Prof. Jay — Machozi, Jasho na Damu:
2. Hasheem Dogo. Huyu hajatoa ngoma muda mrefu, lakini zile alizozitoa zamani bado zinasumbua hizi mpya zilizotoka leo na zitakazotoka kesho.
3. Nikki Mbishi. Mc pekee ambaye ananishangaza kila siku kwa ubunifu wake, uandishi na jinsi anavyotema madini, hasa pale ninapolinganisha umri wake na sanaa yake.
3. One The Incredible. Napenda jinsi anavyotumia Kiswahili fasaha na ule uandishi wake wa kugushi kushoto kisha anaelekea kulia. Uandishi kama huo kitaalamu huwa unaitwa ‘Unorthodox literary’…
4. Stereo. Nasubiri atoke na album ili nimpe namba moja. Sijawahi kuona Mc mwenye akili na kazi yake, na isitoshe yupo humbled..
5. Jay Mo… huyu jamaa anajua ku-spit. Na ni kweli huwa ana techniques na flava nyingi. Mchopanga kama unasoma hii, naomba utuambie lini utaiachia ‘Mocumentary’.
Amani!

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA