NAPE: HAKUNA NAFASI YA KUKATA RUFAA MAJINA YAKIKATWA

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakutakuwa na nafasi ya kukata rufaa kwa wanachama wa chama hicho walioomba ridhaa ya chama kupeperusha bendera ya CCM katika nafasi ya Urais iwapo majina yao yatakatwa.
Kauli hiyo imetolewa mjini Dodoma leo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho, Nape Nnauye alipokutana na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya ratiba ya vikao vya mchujo wa wagombea utakaoanza siku mbili zijazo.
Kikao hicho kitaongozwa na Katibu Mkuu CCM Abdulrahaman Kinana pamoja na kikao cha sekretarieti ya chama.
Nape alisema hakutakuwa na nafasi ya kukata rufaa kwasababu, kwanza hakuna kanuni hiyo na pia hakutakuwa na muda wa kutosha kufanya hivyo.
“Tuwe wakweli tu, muda wenyewe siuoni na kanuni haisemi habari ya kukata rufaa...uchujaji wa majini kikao hakitakiwi kutoa sababu, sasa unakataje rufaa,” alisema Nape.
Hata hivyo Nape amewapa matumaini wanachama wa chama hicho kuwa watatoka kwa umoja hata baada ya kupatikana kwa mgombea urais kupitia chama hicho.
Aidha amebainisha kuwa hakuna fujo zozote zitakazotokea, kwa kuwa vyombo vyote vya ulinzi vimejipanga vya kutosha.Kwa mujibu wa ratiba ya kikao,Kamati Kuu itakutana tarehe tisa na kutoa wagombea watano kabla ya Halmashauri Kuu kukutana tarehe 10mwezi huu, ambapo majina matatu ya wagombea yatateuliwa kabla ya kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu tarehe 11 ili kumpata mgombea mmoja atakaepeperusha bendera ya chama hicho.
CHANZO:MWANANCHI

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA