Tahadhari ya Wizara kuhusu wanaojitambulisha kama viongozi wa kielimu



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

Tanzanian Government National Emblem Logo ngao uhuru na umoja

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MATAPELI WANAOOMBA RUSHWA KWA KUJITAMBULISHA KAMA VIONGOZI WA ELIMU

Kumejitokeza kundi la watu ambao ni matapeli wanaoomba rushwa kwa kujitambulisha kama viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kutumia namba za simu zilizoandikishwa kwa kutumia majina ya viongozi hao. Namba hizo hutumika kwa muda na baada ya kufanikisha lengo lao, watu hao huzifunga na hivyo kutokupatikana tena hewani.

Majina ya viongozi yanayotumika katika utapeli huo ni ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Katibu Mkuu, Kamishna wa Elimu na ya baadhi ya Wakurugenzi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Namba hizo za simu hutumika na matapeli hao kwa kuwapigia watu wanaohitaji huduma katika ofisi za elimu na kuwaomba wawatumie fedha kupitia namba hizo ili kufanikisha upatikanaji wa huduma wanazozihitaji kutoka katika ofisi hizo. Huduma zinazotajwa ni pamoja na kufanikisha usajili wa shule na vyuo.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inawatahadharisha wananchi kujiepusha na kundi hili la matapeli na ifahamike kuwa huduma zote zinazotolewa katika ofisi za elimu zikiwemo za usajili wa shule hazitolewi kwa rushwa au malipo ya aina yoyote.

Maelezo kamili kuhusu usajili wa shule yanapatikana katika ofisi za Ukaguzi wa Shule za Wilaya na Kanda na ofisi za Makao Makuu ya Wizara, au chumba namba 21 na 36 hapa wizarani. Tafadhali wasiliana na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu au Kamishna wa Elimu endapo utapigiwa simu na mtu usiyemfahamu atakayejitambulisha kwako na kudai fedha ili afanikishe usajili wa shule au kupata huduma zingine wizarani. Usikubali kudanganywa na kutoa fedha kwa huduma inayopatikana bure.
Imetolewa na:

Katibu Mkuu,
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
02 Julai, 2015

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA