TUJIKUMBUSHE: BOMU LINALOMWANDAMA SAMIA SULUHU HASSAN


Samia Suluhu Hassan
Samia Suluhu Hassan

Kisiwa cha utalii cha Changuu, kilikodishwa kwa ‘ bei chee’ na kampuni ya Leizure Hotel Limited, ripoti ya Kamati ya Baraza la Wawakilishi (BLW) imebaini.

Ripoti ya Kamati ya BLW iliyoundwa kuchunguza ubadhirifu wa mali za serikali , imebaini kuwa kilikodishwa kwa kodi ya Dola 1,000 kwa mwezi na kumtaja aliyehusika na ukodishwaji huo kuwa ni aliyekuwa Waziri wa Utalii Biashara na Uwekezaji Zanzibar, Samia Suluhu Hassan.

Waziri huyo wa zamani anatajwa kuwa alishirikiana na Kitengo cha Uwekezaji Zanzibar, (ZIPA) kufanikisha suala hilo Desemba 2002.

Katika Baraza la Mawaziri la sasa Samia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kisiwa hicho chenye ukubwa wa hekta 11.27 kimekodishwa mwaka 2002 kwa malipo ya Dola za Marekani 1,000 kwa mwezi katika kipindi cha miaka 30. (Dola moja ni karibu sawa na Sh. 1,580)

Hata hivyo kodi hiyo imerekebishwa na kufikia Dola 3,500 licha ya kwamba kabla ya kuwamilikisha wageni kisiwa hicho kilikuwa kinavuna zaidi ya Dola 5,500 kwa mwezi,

Kabla ya kukodishwa kisiwa hicho Shirika la Utalii Zanzibar, (ZTC) lilikuwa likikusanya zaidi ya Dola za Marekani 5,500 kwa mwezi kupitia watalii waliokuwa wakitembelea kisiwa hicho.

“ZTC lililipwa Sh.milioni 40 ili kuondoa mkono wao kwenye kisiwa hicho,” imeeleza ripoti hiyo ambayo imeibuwa mjadala mkubwa visiwani Zanzibar.

Kamati hiyo ya uchunguzi imesema kiwango hicho cha kodi kiliendelea kulipwa na mwekezaji huyo hadi mwaka 2004 kabla ya kufanyiwa mabadiliko baada ya kulalamikiwa kuwa mkataba huo hauna maslahi kwa serikali.

“Kamati ya Baraza haikuridhika na kiwango cha kodi ambacho kilikuwa kinalipwa na wakodishwaji na baada ya hapo kodi iliongezeka kufikia Dola 3,500 kwa mwezi kiasi ambacho kinaendelea kulipwa hadi sasa.”ilisema ripoti hiyo.

Akihojiwa na Kamati ya Uchunguzi ya Baraza hilo Meneja wa Shirika la Utalii Zanzibar, Sabaha Salum, alisema wakati kisiwa hicho kinasimamiwa na shirika lake walikuwa wakikusanya Dola 5,500 kwa mwezi. Hata hivyo alisema ZTC katika kitega uchumi hicho walihusika kukodisha biashara tu, lakini ukodishwaji wa ardhi ya kisiwa ulifanywa na Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na ZIPA.

Kuhusu kobe ambao wamehifadhiwa katika kisiwa hicho alisema pia wamekodishwa kwa mwekezaji huyo kwa mkataba maalum ulioidhinishwa na Idara ya Uhakiki wa Mali za Serikali.

Hata hivyo alisema shirika lilikuwa na mpango wa kukodisha kobe hao katika hifadhi ya wanyama ya ‘Zanzibar Park’ lakini serikali iliahirisha kutokan na wananchi wengi kujitokeza kupiga mpango huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya ZIPA kuhusu mradi huo, kampuni hiyo ilikabidhiwa rasmi kisiwa hicho Agosti mwaka 2003 na mradi huo ulitarajia kuwa na thamani Dola za Marekani milioni 1.1 ambapo hadi sasa kampuni hiyo imejenga vyumba 27 vya kulala wageni katika kisiwa hicho.

Wakihojiwa na kamati hiyo ZIPA walieleza kuwa kampuni hiyo imekuwa na tatizo kubwa la kuficha taarifa za mapato na takwimu za wageni wanaotembelea kisiwa hicho tangu kukabidhiwa mradi huo , hali waliyosema ni kinyume na sheria za uwekezaji Zanzibar.

‘Haieleweki ni kiasi gani cha mapato ambacho mwekezaji anaingiza kutokana na biashara anazofanya kisiwani Chaguu.”

Aidha alisema kamati hiyo ilipokea taarifa kuwa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na SMZ wala taarifa yoyote inayopatikana ya kiulinzi na usalama kutoka kwa wawekezaji hao.

ZIPA iliieleza kamati kuwa mwekezaji huyo kwa mujibu wa sheria anatakiwa kutoa taarifa za shughuli zake kila baada ya miezi mitatu jambo ambalo halifanyiki.

Pia ilisema baada ya kuhojiwa na Kamati ya BLW Mkurugenzi wa Ardhi Zanzibar kuhusu utaratibu uliotumika kutoa kisiwa hicho, alisema “Wakati kodi inapagwa kwa mara ya kwanza ya ukodishwaji wa kisiwa hicho hapakuwa na tathimini yoyote ya kitaalamu iliyokuwa imefanyika hadi sasa kuhusiana na ardhi ya kisiwa hicho.”alikaririwa mkurugenzi wa Ardhi wa Zanzibar.

Kamati imeitaka SMZ kuchukuwa hatua ikiwemo kumtaka mwekezaji huyo kutoa taarifa za mapato na wageni wanaoingia na kutoka katika kisiwa hicho ndani ya miezi mitatu tangu kutolewa kwa ripoti hiyo ya uchunguzi mwezi uliopita.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa tathimini ya ardhi ifanywe pamoja na kuangalia upya sheria ya ukodishaji ardhi kifungu cha 46(6) namba 12 ya mwaka 1992 ili ongezeko la kodi lisiwekewe kikomo cha asilimia 10 ya kodi ya awali ya mkataba wa mradi.

Kamati ilieleza kufurahishwa na hatua zinazochukuliwa na kampuni hiyo ya uhifadhi wa mazingira katika kisiwa hicho tangu kufanyika ukodishwaji.

Kisiwa cha Chaguu kina daiwa kukodishwa kwa mwekezaji huyo kwa zaidi ya miaka 30 na kimekuwa kivutio kikubwa cha watalii kutokana na historia kubwa ikiwemo kuwahi kutumika kama gereza kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 yaliyowaondoa Waarabu visiwani hapa.

Kisiwa cha Changuu Z`bar chakodishwa kwa `bei chee`

MWINYI SADALLAH
NIPASHE JUMAPILI
Mei 13, 2012

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA