BOKO HARAM WAMEUA WATU 380 CAMEROON
Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International limesema
raia 380 wameuawa na wapiganaji wa Boko Haram kaskazini mwa Cameroon
mwaka huu.
Wanajeshi na polisi wa Cameroon nao wanadaiwa kujibu mashambulio ya kundi hilo kwa kuwakamata watu zaidi ya 1,000, wengi wao vijana.
Shirika hilo linasema watu 200 waliokamatwa na maafisa wa usalama kwenye operesheni Desemba kwa sasa hawajulikani waliko.
Amnesty wanaamini Cameroon inaweza kujifunza mengi kutokana na makosa yaliyofanywa na taifa jirani la Nigeria ambako wanajeshi wametuhumiwa kutekeleza dhuluma dhidi ya raia kwa muda mrefu.
Kundi hilo linasema yaliyotokea Nigeria yanaonyesha kukosa kuheshimu haki za kibinadamu na sheria za kimataifa kuhudu ubinadamu katika vita dhidi ya Boko Haram kuna madhara makubwa.
Katika kisa kimoja kaskazini mwa Cameroon, shirika hilo la haki za kibinadamu linasema maafisa wa usalama walishambulia shule za kutoa mafunzo ya Kiislamu ambazo waliamini zilikuwa kambi za mafunzo za Boko Haram.
Watoto 84 na wanaume zaidi ya 43, wakiwemo walimu wengi, walizuiliwa kwa miezi sita bila kufunguliwa mashtaka, shirika hilo linasema.
Katika visa vingine, wanajeshi wa Cameroon wanadaiwa kupora mali na kuteketeza nyumba za watu.
Comments
Post a Comment