. UKAWA yataja zitakakotoka fedha za elimu bure, bajeti, punguzo la kodi ya mshahara




BAADA ya ahadi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ya kutoa elimu bure kwenye ngazi zote na kupunguza kodi ya mishahara kutoka asilimia 18 hadi tisa, kubezwa kwamba haitekelezeki, umoja huo umeeleza ilipopata jeuri ya ahadi hiyo baada ya kuainisha vyanzo vya mapato watakavyotumia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, amesema wamefanya utafiti wa kina na kubaini ahadi hizo zinatekelezeka tofauti na ambavyo wapinzani wanawakejeli.

Alisema utafiti uliofanyika umebaini kuwa iwapo watadhibiti mapato yanayopotea katika ulipaji kodi, kupunguza misamaha ya kodi hadi asilimia 1, kuboresha ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam, sekta ya utalii na uvuvi, mapato ya Serikali yataongezeka maradufu kuliko ya sasa.

“Wameanza kutukebehi kwamba ilani yetu haitatekelezeka, eti hizo fedha za kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu itatoka wapi,” alisema.

Alisema takwimu za Serikali sasa hivi zinaonyesha mapato ya ndani yatokanayo na kodi na yasiyotokana na kodi ni Sh trilioni 13.47 ambayo ni asilimia 14.3.

“Hivyo kutokana na takwimu hizo, asilimia 100 ya pato la taifa ni zaidi ya Sh trilioni 90,” alisema.

Mbatia alitaja mambo yatakoyoweza kusaidia kwenye ukusanyaji kodi ni kuwekwa mazingira mazuri kwa mlipakodi na wigo wa kodi kutanuliwa, kuwapo viwango vya kodi vinavyotabirika na tegemezi na Mamlaka ya Mapato (TRA) kupambana na ukwepaji wa kodi.

Alitaja njia nyingine kuwa ni kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia asilimia moja ya pato la taifa, kuongeza ufanisi Bandari ya Dar es Salaam, kuweka mazingira mazuri na endelevu kwenye sekta ya utalii na kukusanya kwa ufanisi mapato kwenye sekta ya uvuvi.

“Kwenye sekta ya uvuvi pekee tunaweza kupata zaidi ya Sh trilioni moja kwa mwaka. Lakini pia kwa sasa mapato yanayotokana na kodi ya nyumba kubwa kubwa ni asilimia tatu tu ya makusanyo yote,” alisema.

ZITAKAKOTOKA FEDHA ZA ELIMU

Mbatia alisema wakati Serikali ina uwezo wa kukusanya asilimia 25 pekee ya pato la taifa kwa sasa, wao wataweza kukusanya na ongezeko la zaidi ya Sh trilioni 10.

“Chukua asilimia 25 ya pato la taifa leo ambalo kwa takwimu za Wizara ya Fedha ni zaidi ya trilioni 23.55 wakati wao wanakusanya Sh trilioni 14.3, niwahakikishie Watanzania tuna uwezo wa kuleta ufanisi tukifanya uamuzi, na Lowassa anaweza kufanya uamuzi mgumu,” alisema Mbatia.

Alisema wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu ni 300,000 na ada yao ni inafikia sh trilioni 1.55, hivyo hata kama wataongezeka mara mbili bado Serikali ya Ukawa itaweza kumudu gharama hizo kutokana na makusanyo ya kodi.

KODI YA MSHAHARA

Mbatia alisema kwa sasa kodi ya wafanyakazi wa Tanzania ni kubwa ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Alisema licha ya kwamba Serikali inasema kodi ni asilimia 11, ukweli ni kuwa kiasi hicho kinakatwa kwa watu wenye mshahara wa kima cha chini, huku wale wa juu wakikatwa hadi asilimia 18.

“Wafanyakazi wa Tanzania ndio wanalipa kodi kubwa ya mshahara ambayo ni takribani asilimia 18, na hizo ni takwimu za Benki ya Dunia tukifuatiwa na Uganda wanaolipa asilimia 11, Burundi asilimia 10, Kenya asilimia 6.8 na Rwanda asilimia 5.6.

“Tunavyosema tutapunguza kodi kutoka asilimia 18 mpaka tisa ambayo ni punguzo la Sh bilioni 704, hilo punguzo tutalipata kwenye sekta ya utalii, uvuvi, ndiyo maana tunasema tutaipunguza kodi kwa mfanyakazi, tunawaambia Watanzania watuamini, haya tutayafanya na yanawezekana kabisa,” alisema Mbatia.

SAFARI ZA VIONGOZI

Mbatia alisema mbali na kuangalia mambo makubwa, safari za viongozi ni eneo jingine watakaloweza kulitumia kupata fedha zitakazoweza kufidia pengo litakalosababishwa na kupunguza kodi ya mishahara na kutoa elimu bure.

“Viongozi walioko madarakani, hususani rais, ameshasafiri nje ya Tanzania takribani mara 409 na wastani wa kila safari ya siku tatu mpaka tano ni dola milioni 3 na milioni 5, hivyo mpaka sasa tayari wametumia takribani sh trilioni 4 katika safari hizo,” alisema.

Alisema fedha hizo zingeweza kujenga vyuo vya kisasa vya veta zaidi ya 200 nchi nzima ambapo kila kimoja kingegharimu Sh bilioni 20, pia zingeweza kujenga hospitali zaidi ya 100, kila moja ikigharimu Sh bilioni 30 na kujenga vyuo vikuu zaidi ya 80, kila kimoja kikigharimu Sh bilioni 50.

Mbatia alisema si kwamba Serikali ya Ukawa itaishi kama kisiwa bila kushirikiana na wengine bali watapunguza safari zote zisizo za lazima.

“Kwa mfano rais anataka kutunukiwa shahada ya heshima, hakuna sababu ya yeye kwenda nje ya nchi na kutumia mabilioni ya fedha za walipakodi, kwanini hao wanaotaka kumtunuku wasije pale Ikulu? Lakini hata mikutano mingine siyo lazima aende, anaweza kushiriki kwa kutumia teknolojia (teleconference),” alisema.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA