Hawaruhusiwi kutumia rasilimali za umma kwenye kampeni za kisiasa isipokuwa...


Katika ukurasa wa mbele na wa tano wa Gazeti la Nipashe, toleo 0578604 la tarehe 12 Septemba, 2015 kumechapishwa taarifa kwamba “Sefue; Marufuku kutumia magari ya serikali kwenye kampeni”

Katika taarifa hiyo, imeelezwa kwamba Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema “Ni kosa kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutumia rasilimali za serikali yakiwemo magari katika mikutano ya kampeni ya Chama cha Mapinduzi (CCM).”


Alichosema Katibu Mkuu Kiongozi ni kwamba Watumishi wa Umma wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Wilaya hawaruhusiwi kutumia rasilimali za umma yakiwemo magari kwenye kampeni za kisiasa isipokuwa wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao kiserikali.


Aidha, watumishi wa Umma wanaotaka kushiriki katika katika kampeni za kisiasa ama kugombea nafasi yoyote ya kisiasa sharti wajiudhulu nyazifa zao za utumishi wa umma.


Kupitia taarifa hii, Watumishi wa Umma na wa Kisiasa wanaombwa kuzipuuza taarifa hizo potofu zilizoandikwa na gazeti la Nipashe na wanashauliwa kufuata maelekezo yaliyomo kwenye Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Namba 1 wa Mwaka 2015. Walaka huu unaeleza bayana utaratibu na jinsi Watumishi wa Umma wanavyoweza kushiriki katika kugombea ama kufanya kampeni za kisiasa na utaratibu pindi mtumishi wa umma anataka kugombea nafasi ya kisiasa.


Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo

13 Septemba, 2015

Habari iliyochapishwa katika gazeti la NIPASHE "Sefue: Marufuku kutumia magari ya serikali kwenye kampeni."


Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue amesema ni kosa kwa wakuu wa mikoa na wilaya kutumia rasilimali za serikali yakiwamo magari katika mikutano ya kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kadhalika, Sefue amesema walimu katika vyuo vikuu vya umma wanaruhusiwa kufanya ama kujihusisha na masuala ya siasa kwa kuwa baadhi yao wanakuwa wanafanya utafiti.

Hata hivyo, kuhusu viongozi hao kutumia magari yao ambayo ni ya serikali katika mikutano ya CCM, Sefue alisema hajapata ushahidi kamili, lakini alisema ni kosa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma.

Alitoa kauli hiyo baada ya baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa kuonekana katika misafara ya wagombea wa CCM wakifanya kampeni huku wakitumia magari ya serikali.
Pamoja na gazeti hili kumtajia baadhi ya mikoa na wilaya ambayo viongozi hao walionekana kutumia magari ya serikali kwenye kampeni za CCM, Sefue alisisitiza kwamba hajapata ushahidi.

Katika maeneo mbalimbali viongozi hao ambao kwa mujibu wa katiba ya CCM ni wajumbe wa kamati za siasa katika wilaya na mikoa yao, wameonekana katika mikutano ya kampeni za CCM, wakiwa na magari ya serikali yakiwa na nembo ya DC ama RC.

Akizungumza na Nipashe Ikulu juzi muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete kupokea tuzo mbili kutoka taasisi ya East Africa Book of Records ya nchini Uganda, Sefue alisema walimu katika vyuo vikuu ambao ni madokta na maprofesa, hawafungwi kushiriki siasa.

Hata hivyo, wakati Sefue akitoa ufafanuzi huo, Profesa Mwesiga Baregu aliwahi kusimamishwa kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kile kichodaiwa kujihusisha na siasa ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwa mjumbe wa kamati kuu.

Alisema watumishi wa serikali wameganyika katika makundi mbalimbali wapo wanaoruhusiwa kushiriki siasa na ambao hawaruhusiwi wakiwamo makatibu wakuu wa wilaya, yeye mwenyewe, lakini wapo ambao hawafungwi na kanuni hizo utumishi wa umma.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA