Taarifa ya NEC kuhusu ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi 2015
TAARIFA KWA UMMA
KUHUSU VYAMA NA WAGOMBEA KUZINGATIA MAADILI YA UCHAGUZI WA RAIS, WABUNGE NA MADIWANI YA MWAKA 2015
Kama
mnavyofahamu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani
zimeanza tangu tarehe 22 Agosti, 2015 na zinaendelea hadi tarehe 24
Oktoba, 2015.
Ni
jambo linaloeleweka kwamba mchakato wa Kampeni na wa Upigaji Kura
unatawaliwa au kuongozwa na Sheria, Katiba na Maadili ya Uchaguzi wa
Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.
Katika
kipindi hiki tangu Kampeni zianze, nafurahi kusema kwa niaba ya Tume
kuwa kwa ujumla, Kampeni zimeenda vizuri. Karibu mikutano yote
imefanyika katika hali ya utulivu na amani. Hatujapata taarifa ya
mkutano wa Kampeni ambao umevurugwa kwa fujo zozote. Kwa hilo napongeza
Vyama vyote vya Siasa.
Hata
hivyo, kutokana na mikutano hiyo nchini ya Kampeni, ngazi ya Urais,
Ubunge na Udiwani yamejitokeza mambo ambayo ni kinyume kabisa na
Mwongozo wa Maadili ya Uchaguzi wa Rais Wabunge na Madiwani wa mwaka
2015 uliotiwa saini na Vyama vyote vya Siasa tarehe 27 Julai, 2015.
Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yamejitokeza katika Kampeni hizo:-
(i) Kutozingatia muda wa kumaliza Mikutano ya Kampeni
Kuna
baadhi ya Vyama ambavyo katika mikutano yao vimekiuka Kipengele hiki
kwa kufanya mikutano zaidi ya saa 12.00 jioni. Kuendelea kufanya
Mkutano wa Kampeni zaidi ya muda huo ni ukiukwaji wa Kipengele cha 2.1 (c) cha
Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015
kinafafanua kuwa Mikutano yote ya Kampeni itafanyika kuanzia saa 2.00
asubuhi hadi saa 12.00 jioni.
(ii) Kubandika mabango ya Kampeni, matangazo au Mchoro wowote kwenye maeneo yasiyoruhusiwa au bila idhini ya wahusika
Baadhi
ya Vyama vimeanza kubandika mabango, michoro na picha za Wagombea wao
katika majengo au vyombo vya usafiri vya watu binafsi au Taasisi
mbalimbali bila idhini ya wamiliki husika.
Napenda kuwakumbusha kuwa, kwa mujibu wa Kipengele cha 2.2. (g) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, hairuhusiwi kufanya hayo bila idhini ya wamiliki husika.
(iii) Kuchafua, kubandua au kuharibu matangazo au picha za Kampeni za Vyama vingine
Tume
imeanza kupokea malalamiko kutoka baadhi ya Vyama kuwa, mabango au
picha za Kampeni za Vyama vyao yanabanduliwa au kuchafuliwa na wafuasi
wa Vyama vingine.
Ni vema Vyama vya Siasa na Wagombea wakumbuke kuwa Kipengele cha 2.2 (f) cha
Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015,
kinapiga marufuku Chama kingine kuchafua, kubandua au kuharibu matangazo
au picha za Kampeni za Vyama vingine.
(iv) Matumizi ya lugha zisizo za staha
Tume
imepokea malalamiko kuwa, katika Mikutano mbalimbali ya Kampeni katika
ngazi zote, kumeanza kujitokeza baadhi ya viongozi wa Vyama, Wagombea au
wafuasi wao kutumia lugha zisizo za staha wakati wa Mikutano ya Kampeni
katika ngazi mbalimbali.
Lugha zisizo za staha zinajumuisha matusi, kejeli, kashfa n.k. Kipengele cha 2.2 (b) cha
Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015,
kinakataza Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wao kutumia lugha
zisizo za staha katika harakati zote za Kampeni hadi upigaji Kura.
Wajibu wa Vyama vya Siasa na Wagombea
Viongozi
wa Vyama vya Siasa na Wagombea wana wajibu wa Kisheria wa kuyaheshimu,
kuyasimamia na kuyatekeleza Maadili hayo kwa mujibu wa Kipengele cha
2.1. (b) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka
2015. Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wana jukumu la
kuwaelimisha, kuwahamasisha na kuwasisitiza wanachama wao kutekeleza
Sheria ya Uchaguzi (ikumbukwe kuwa Maadili ya Uchaguzi yametungwa chini
ya Kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343)
Adhabu za ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi
Napenda
kuwakumbusha Vyama vya Siasa na Wagombea kuwa, ukiukwaji wa aina yoyote
wa Maadili unaweza kusababisha Chama au mgombea kupewa adhabu kama
zilivyoainishwa katikaKipengele cha 5.10 (a-f). Adhabu hizo ni pamoja na:
1. Chama au Mgombea aliyekiuka maadili kuelekezwa kuomba msamaha hadharani.
2. Kupewa onyo au karipio.
3. Kumtangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari na taarifa kwa Umma mgombea au Chama kilichokiuka Maadili.
4. Chama au Mgombea kusimamishwa kuendelea kufanya Kampeni.
5. Chama au Mgombea kuzuiliwa kutumia vyombo vya habari.
6. Chama au Mgombea kulipa faini kuanzia kiwango cha 100,000/- 500,000/- na 1,000,000/- kutegemea ngazi ya Kamati husika.
Katika
kipindi hiki cha Kampeni, Chama au Mgombea akipewa mojawapo ya adhabu
hiyo kunaweza kuathiri Kampeni zake za kuelekea Uchaguzi wa Rais,
Wabunge au Madiwani.
Hitimisho.
Napenda kunukuu Kipengele cha 1.4 cha
Maadili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 ili
kila Chama kione umuhimu wa kuwahimiza wagombea na wanachama wao
kuzingatia Maadili katika harakati zao za kujinadi. Nanukuu:
“[……]
kila mgombea atajaza Fomu Na. 10 kuthibitisha kuwa ataheshimu na
kutekeleza Maadili ya Uchaguzi. [….] Mgombea atakayekataa kusaini
Maadili haya atakataliwa au kuondolewa kushiriki katika Uchaguzi kama
Mgombea.”
Maana
yake ni kwamba kila Chama, Mgombea na Wanachama kwa ujumla wana wajibu
kuheshimu taratibu zote za Kampeni hadi kupiga Kura.
Yote
yaliyokatazwa katika Maadili yazingatiwe na Vyama vyote. Kama
nilivyosema hapo awali Tume imepata malalamiko kuwa baadhi ya Vyama na
Wagombea wamekiuka Maadili ama kwa kuzidisha muda wa Kampeni, au kuchana
na kuharibu mabango, au kutumia lugha chafu isiyo na staha; Haya yote Tume inakemea kwa nguvu sana na kusihi Vyama vyote na Wanachama wao wote kuheshimiana, waeleze sera zao bila kukashifiana.
Lengo
na matumaini ya Tume ni kuwa na Kampeni za utulivu na hatimaye wananchi
kuwa na hali ya utulivu na amani ili Uchaguzi ufanyike kwa amani na
utulivu. Kwenye hali ya utulivu na amani wananchi wataweza kupiga Kura
ya utulivu ili kuamua viongozi wanaowataka. Hiyo ndiyo Demokrasia.
Nimalizie
kwa kuwakumbusha Vyama vyote kuzingatia Maadili ya 2015. Tume
isilazimishwe kuchukua hatua za kutoaadhabu kwa Vyama na
Wagombea. Busara itumike katika mikutano yote ya Kampeni.
Inawezekana, wote tukidhamiria, “Play your Part”.
Jaji (Mst.) Damian Z. Lubuva
MWENYEKITI
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
Comments
Post a Comment