Mbatia amchambua Dk. Slaa
Umoja huo ulioundwa na vyama vinne wakati wa Bunge Maalum la Katiba, 2013, una kazi kubwa ya kuwaeleza wananchi umuhimu wa kukinyima kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho badala ya kujisafisha kinatumia mbinu ya kueneza propaganda kuwa kimebadilika.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya New Africa, kuhusu tuhuma alizozitoa Dk. Willibrod Slaa ambaye amelaumu viongozi aliokuwa nao Chadema kwa alichosema kimepokea viongozi waovu kutoka CCM.
Mbatia amesema mambo yanayofanywa na CCM kwa wananchi ni ya kutaka kuivuruga amani ya Watanzania, lakini dhamira yao inashindwa.
Lawama za Dk. Slaa zililenga kumshambulia Edward Lowassa, ambaye ndiye aliyejiunga Chadema akitokea CCM baada ya jina lake kukatwa kwenye orodha ya waliojadiliwa kugombea urais.
Lowassa ambaye ameteuliwa kuwa mgombea urais wa jamhuri ya Muungano kupitia Chadema, akiwakilisha UKAWA, anaendelea kuzunguka nchi akifanya kampeni ya kuomba ridhaa ya wananchi ya kuongoza taifa.
Mgombea mwenza wake ni Juma Duni Haji kutoka Zanzibar ambaye naye alikaribishwa Chadema akitokea Chama cha Wananchui (CUF). Dk. Slaa pia amemshambulia Frederick Sumaye, waziri mkuu mstaafu ambaye alihama CCM na kujiunga na kampeni ya Lowassa kuchukua uongozi wa dola. Akijibu tuhuma alizotoa Dk. Slaa kwamba viongozi wa dini walihongwa fedha na Lowassa ili kumuunga mkono, Mbatia amesema alichokifanya daktari huyo ni mipango iliyosukwa maalumu ili kuwagombanisha viongozi hao wa dini na waumini wao na kusababisha kutoaminika tena.
“Uongo uliosemwa jana ulinisikitisha… anajaribu kuivuruga amani ya Watanzania kwa kuzungumza uongo huku akiwahusisha viongozi wa dini halafu anajiita Padri wakati anajihusisha na siasa chafu tena za mitaroni,” amesema Mbatia.
Mbatia amesema tuhuma dhidi ya Lowassa zilianza tangu mwaka 2008, kama ni kweli mbona hakushitakiwa hadi sasa? Kwanini wasimfungulie mashitaka tangu alipojiuzulu katika hatua ya uwajibikaji ili kuifichia aibu serikali ya rais Kikwete… alifcha kombe mwanaharamu apite lakini yeye hakushiriki bali alibebeshwa mzigo,” amesema.
Mbatia amesema Januari 4, 2009 alimwandikia barua Rais Kikwete akiutafsiri kwa undani ufisadi. “Nilipata kumshauri akitaka kukomesha tatizo hili ni lazma aanze ngazi za chini lakini pia ilishindikana kwani mfumo mzima wa uongozi chini ya CCM ni mbovu na taasisi za kushughulikia rushwa ndio zinahusika.
“Nikianza kuuchambua ufisadi unaofanywa na viongozi wa CCM hapa hakuna atakayepon, kila mtu ataenda jela kuanzia mgombea wao wa urais, Rais Mstaafu Mkapa, Samuel Sitta na wengine kibao.”
Amesihi wananchi na viongozi wa dini kuwa watulivu wakisubiri kupiga kura ya maamuzi na kuomba wachague wagombea wanaosimamishwa na vyama vilivyojiunga katika UKAWA.
Chanzo: Mwanahalisi Online
Comments
Post a Comment