Safari ya kuelekea Dodoma: Jambo 1 muhimu na 8 ya kuzingatia


Kuna mambo ambayo ni lazima yaangaliwe katika uamuzi wa kuhamia Dodoma.
  • Kuna masuala ya kuangalia kama idadi ya watumishi watakaohama na hawa wana familia ngapi, ikiwamo watoto wa shule. Lazima athari za kuhamisha watu wa namna hii hazina budi zitathminiwe na kupatiwa mwelekeo endelevu. Lazima kuangalia gharama za kuhama ghafla ni Sh ngapi na watakaolengwa ni watumishi wapi, yaani kada ipi na fedha zimetengwa kwenye kasma ipi!
Aidha, hatua ziangaliwe za kuzuia bei ya viwanja kupanda bei ovyo kwa sababu idadi ya watu watakaotafuta viwanja itaongezeka kwani tayari kuna taarifa kuwa mamia ya wananchi wameanza kupeleka maombi yao ya kupata viwanja katika ofisi za Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA). Hali hiyo imetokea baada ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza nia ya Serikali kuhamia mjini Dodoma kwa kuwa ndiko yaliko makao makuu ya nchi.
  1. Kwamba kuna idadi kubwa ya watu wanaofika katika ofisi za Idara ya Ardhi katika mamlaka hiyo, na kwamba Jeshi la Polisi tayari linalazimika kuimarisha ulinzi ili kukabiliana na hali hiyo.
  2. Kwamba kuna watu waliokuwa hawalipii viwanja vyao siku za nyuma, lakini sasa wanahangaika kulipia viwanja hivyo. Kwa bahati CDA inasema ardhi mjini Dodoma itauzwa kwa bei ya kawaida ili watu wengi waweze kumiliki viwanja.
  3. Kwamba ‘square’ mita moja ya kiwanja cha makazi Sh 5,500 hadi Sh 10,000 katika maeneo ambayo kitaalamu tunayaita ‘medium density’. Viwanja kwa uwekezaji mkubwa ‘square’ mita moja itauzwa kwa Sh 13,300 na maeneo hayo kitaalamu tunayaita ‘low density’. Tunawahimiza watu wasinunue viwanja kienyeji ili wawakwepe wapigaji wa dili watakaowaumiza.
  4. Kwamba pamoja na uwepo wa mahitaji makubwa, ardhi ipo ya kutosha, yaani hata kama watakuja wananchi wote wa Dar es Salaam watapata ardhi ya kutosha; hata baada ya miaka 30 ardhi itatosha kwa sababu hata Mwalimu Nyerere alipoamua Dodoma iwe makao makuu, alijua kuna ardhi ya kutosha kwa idadi yoyote ya watu.
  5. Kwamba mpangilio wa mji utaanzia katika Kijiji cha Mtumba hadi eneo la Ikulu ndogo ya Chamwino ambako kutakuwa na ofisi za wizara na mabalozi. Mji wa kibiashara utakuwa ni eneo lote la mji wa Dodoma kwa sababu hii iko katika ‘master plan’ ya mwaka 2010-2030 ya kuhakikisha makao makuu ya nchi yanakuwa vizuri kuanzia kwenye barabara za kuingia na kutoka ili kusiwe na msongamano wa aina yoyote.
  6. Kwamba CDA imetenga maeneo maalumu kwa kujenga mahoteli makubwa na nyumba mbalimbali za kupanga. Zaidi ya ekari 1,500 kwa uwekezaji mkubwa zimetengwa na miundombinu iliishafika mapema kwani kuna maji, umeme pamoja na barabara za lami.
  7. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, tayari amesema kuwa TANESCO itazalisha umeme wa megawati 60 ili kuondoa tatizo la kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Dodoma.
  8. Aidha, maeneo yote yatakayopimwa yatapata maji safi na salama; na Wakala wa Barabara Tanzania (TanRoads) amejipanga kukabiliana na ongezeko la magari.
Tunasema kuhamia Dodoma iwe chagizo cha maendeleo badala ya kuleta mambo hasi kwa Watanzania, wakiwamo wafanyakazi.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA