Taarifa kuhusu kuanzishwa kwa rajisi kuu ya namba tambulishi za mikononi

ISO 9001:2008 CERTIFIED


Ndugu Waandishi wa Habari;

Tumewaita hapa leo ili tuwapatieni taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kuzuia simu bandia za kiganjani zisitumike kwenye mitandao ya simu hapa nchini.

Kama ambavyo mnakumbuka, usiku wa tarehe 16 Juni 2016 simu bandia zilizuiwa kutumika katika mitandao ya simu. Maagizo ya Serikali kuzuia matumizi ya simu bandia kwenye mitandao ni sehemu ya mpango wa kuanzishwa kwa rajisi kuu ya Namba Tambulishi za simu za mkononi, kwa kifupi CEIR ambayo ni Central Equipment Identification Register.

Uthibiti wa matumuzi ya simu katika mitandao ya mawasiliano kunatokana na kuongezeka kwa umuhimu wa simu na vifaa vya mkononi vya mawasiliano kama nyenzo muhimu kimaisha, kijamii, kiuchumi, na kiusalama.

Vifaa vya mkononi vya mawasiliano ambavyo vinatumia laini ya simu, yaani SIM card kuwasiliana vina namba maalum inayoitambulisha, ambayo inaitwa IMEI – kifupisho cha International Mobile Equipment Identity.

Mfumo wa Rajisi kuu ya Namba Tambulishi ni wa kielektroniki na unahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi (IMEI). Lengo la Rajisi ni kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango (bandia) vya matumizi katika soko la mawasiliano.

Kuanzishwa kwa Mfumo wa Rajisi kuu ya Namba Tambulishi kunatokana na matakwa ya kisheria, ikiwemo masharti ya vifungu vifungu vya 84 hadi 90 vya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010 na Kanuni za Namba Tambulishi (Central Equipment Identity Register) za mwaka 2011. Sheria na Kanuni vinaipa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania nguvu ya kusimamia kwa karibu vifaa vya kielektroniki vya mawasiliano vyenye namba tambulishi.

Sheria na Kanuni hizi zinawataka watoa huduma za simu za kiganjani kuwa na Mfumo wa ndani wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa simu za kiganjani yaani ‘Equipment Identity Register’ kwa kifupi EIR katika mitandao yao. Mifumo hii imeunganishwa na Rajisi Kuu iliyoko hapa TCRA.

Aidha Sheria inawataka watumiaji kusajili IMEI za vifaa wanavyotumia.

Mfumo huu una faida zifuatazo:-

  • Kuongeza usalama mtandaoni kwa watumiaji wa simu, kwani simu zote za kiganjani zitakuwa zinajulikana;
  • Kuzuia matumizi ya simu zisizokuwa na viwango hivyo kuepuka madhara yatokanayo na simu zisizokuwa na ubora stahiki;
  • Kuthibiti wizi wa simu. Iwapo mtu atapoteza au ataibiwa simu ya kiganjani na akatoa taarifa kwa mtoa huduma, simu hiyo tafungiwa isiweze kutumika kwenye mtandao mwingine wowote wa simu za kiganjani;
  • Kuhimiza utii wa sheria: Kifungu cha 128 cha EPOCA kinamtaka mtumiaji wa simu kutoa taarifa ya kupotea au kuibiwa kwa simu au laini ya simu. Kifungu cha 134 kinayataka makampuni ya simu kutokutoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa kama ilivyoelezwa hapo juu. 
  • Kujenga misingi ya matumizi ya simu halisi, zisizo bandia. Mtumiaji ataweza kutambua iwapo simu aliyo nayo inakidhi viwango, ni halisi na sio bandia.Hii pia itatoa fursa kwa wateja wa simu za kiganjani kupata bidhaa inayolingana na pesa walizotoa kununulia simu hizo. 
Uzimaji wa Simu

Usiku wa manane tarehe 16 Juni, 2016 simu ambazo zilikuwa hazina viwango (bandia) zilizimwa kwa kuzingatia uchambuzi wa kina uliofanyika ili kubaini namba tambulishi ambazo hazikuwa na viwango. Namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango ilikuwa ni asilimia 2.96 ya simu zilizokuwa zinatumika kwenye mitandao ya makampuni ya simu hapa nchini. Simu zilizokuwa na namba tambulishi ambazo zimenakiliwa, yaani duplicates zilikuwa asilimia 0.09 na asilimia 96.95 ilikuwa ni idadi ya namba tambulishi za simu halisi (genuine).

Hadi kufikia sasa idadi ya namba tambulishi ambazo hazikidhi viwango zimefikia 1,713,337.

Baada ya kukamilika kwa zoezi la kuzimwa kwa simu zenye namba tambulishi ambazo hazikuwa za viwango (invalid IMEIS) na namba tambulishi zilizonakiliwa (Duplicate IMEIs) hadi sasa idadi ya namba tambulishi zilizonakiliwa ambazo zimezimwa imefikia 117,389.

Uelewa wa wananchi umechangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha mpango huu.

Kama mnavyokumbuka, Mamlaka ya Mawasiliano iliratibu na kuendesha mpango wa elimu kwa umma kuhusu rajisi kuu ya namba tambulishi nchini kote na kupitia vyombo vya habari kati ya 17 Desemba 2015 na 16 Juni 2016.

Katika kutelekeza mpango huu, tumekumbana na changamoto zifuatazo:-
  • Uaminifu mdogo kwa baadhi ya wauzaji wa simu kwa kutoa punguzo kwa wananchi ili kuwashawishi kuzinunua simu bandia kwa bei nafuu. Hata hivyo ni jambo la kutia moyo kwamba wananchi wengi hawakubali kudanganywa.
  • Gharama zinazohitajika katika kuwafikia wananchi na kuelimisha ili waweze kuelewa zaidi juu ya mpango mzima wa kuhakiki simu zao. Tanzania ni kubwa na hatukuweza kufika kila mahali kutokana na ufinyu wa bajeti. 
  • Baadhi ya watumiaji kutokufuata maelekezo ya namna ya kuhakiki simu zao katika kipindi cha mpito. Kwa mfano, wengi walikuwa wanakosea kutuma ujumbe wenye Namba tambulishi kwenda 15090.
  • Baadhi ya watumiaji kuamini kwamba simu bandia ni zile za bei rahisi au ambazo zimenunuliwa hapa nchini na hivyo kulalamika walipofungiwa simu walizonunua kwa bei kubwa na ambazo ni bandia.
  • Baadhi ya watoa huduma kushindwa kushughulikia malalamiko ya wateja waliofungiwa simu zao kwa wakati.
  • Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inaendelea kuwakumbusha watanzania wote kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa simu yake ni halisi na sio bandia. Pia wananchi wanakumbushwa kutoshikilia simu zilizozimwa majumbani na kuzipeleka mahali husika kwa ajili ya ukusanyaji (disposal).
Vilevile Mamlaka inawakumbusha wauzaji wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi na mafundi simu kuwa ni kosa kubadilisha namba tambulishi za vifaa vya simu za mkononi (mobile devices). Kwa mujibu wa kifungu cha 127 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA), mtu yeyote ambaye anachakachua simu au lani ya simu kwa lengo la kubadilisha uhalisia wake anatenda kosa ambalo adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi millioni 30 au kifungo kisichozidi miaka kumi (10) au vyote kwa pamoja.

Aidha, kifungu cha 135 cha EPOCA kimeweka adhabu ya faini ya shilingi 1,500,000 au kifungo cha miaka mitano au vyote kwa pamoja kwa matu ambaye anachakachua simu iliyofungiwa.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inatoa wito kwa wale wote wote wanaofanya biashara za kuingingiza simu hapa nchini kutoka nje wahakikishe kuwa simu wanazoleta zinakidhi viwango, zimehakikiwa kwa mujibu wa wa Shirika la Viwango Tanzania.

Aidha Mamlaka inawakumbusha kwa mara nyingine kuwa wanapaswa kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano kwa mujibu wa Sheria. Hii pia ni kwa mafundi wote wa simu nchini, wanatakiwa kuanza mchakato wa kupata leseni ya kutengeneza simu, ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuwaorodhesha wanaoleta simu zao kutengenezwa ili kuepuka kuwa sehemu ya mtandao wa wizi wa simu.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inawashukuru wadau wote walioshiriki katika kufanikisha Mpango huu. Hao ni pamoja na makampuni ya simu za mkononi, jeshi la Polisi, Viongozi wa mikoa ambako elimu kwa umma ilitolewa, vyombo vya habari Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Asanteni.

IMETOLEWA NA KAIMU MKURUGENZI MKUU, MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

4 JULAI, 2016

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA