Anatafutwa kwa kutokomea na fedha za michango ya harusi

Maisha magumu, ukapa mifukoni umekolea kweli kweli kwa wananchi, hadi kulazimika kuiba michango ya harusi? Eh! Jeshi la Polisi Mkoani Singida linamtafuta mhasibu wa kitengo cha mishahara wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Imani Abduli, anayetuhumiwa kutoweka na sh milioni sita zilizochangwa kwa kwa ajili ya harusi ya mmoja wa askari wake. Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya watumishi wa ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo zinasema kwamba alitoweka na kiasi hicho cha fedha siku mbili baada ya kikao cha mwisho cha maandalizi ya harusi hiyo kilichofanyika siku mbili kabla ya harusi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kamati teule ya harusi hiyo ya askari polisi mmoja, Meja Christopher Mungumaji na Martha Shaka na kwamba, lakini licha ya kuamiwa na kukabidhiwa wadhifa wa kuwa mhasibu mwenye mamlaka ya kupokea na kuhifadhi michango yote ya harusi hiyo ndipo ghafla aliamua kutoweka nayo. Hata hivyo kwa mujibu wa habarai hizo ilidaiwa pia kuwa baada ya Abduli au maarufu kwa jina la 'Pedejee', kutoweka mjini hapa vile vile simu zake zote za mkononi hazipatikani tena hewani tangu wakati huo hadi hivi sasa. Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya ofisi za halmashauri hiyo, zinadai kwamba kwa kutofahamu tatizo hilo lililojitokeza, Abduli alipewa kazi ya kupeleka Dar es Salaam nyaraka mbali mbali za madai ya watumishi wa halmashauri hiyo na kwamba alitakiwa awepo ofisini kwake Jumatatu, Januari 9, 2012 lakini hadi jana alikuwa hajaonekana ofisini. Habari zaidi kutoka ofisini kwake zinadai kwamba Januari 10, Abduli akiwa mafichoni aliagiza nyumba yake iuzwe ili aweze kupata fedha za kutosha kutatua matatizo yake ikiwemo kulipa madeni mbalimbali. Habari hizo zinaendelea kudai kwamba hilo ni tukio la tatu kwa mhasibu huyo ‘kuchakachua’ fedha za michango ya harusi tofauti tofauti na kwamba hata wafanyakazi wenzake wamekuwa wakifanya naye kazi kwa woga sana kwa madai kuwa amekithiri kwa matukio ya kutokuaminika linapofika suala ya fedha, “Wakati akiingia mitini Abduli, mfanyakazi mwenzetu alikuwa ana laptop ya halmashauri, polisi wameinusuru laptop hiyo ambayo Abduli alikuwa tayari ameshatangaza kuiuza kwa bei poa ya shilingi laki tano tu,” aliweka bayana mmoja wa watumishi wa halmashauri hiyo ambaye amekataa jina lake kutajwa gazetini. Akizungumza na waandishi wa habari kwa upande wake, mwenyekiti wa kamati ya harusi hiyo aliyetambulika kwa jina moja tu la Madeje ambaye pia ni mfanyakazi wa TTCL mjini hapa alisema kwamba ili kufanikisha sherehe za harusi hiyo, waliweza kubanana kwa kuchangishana upya na kufanikisha harusi hiyo ya meja wa polisi na mmoja wa wafanyakazi wa Bohari mkoani Singida, Bi Martha Peter Shaka. Licha ya gharika hilo lililojitokeza lakini sherehe hizo zilifanikiwa kwa harusi hiyo kufanyika kwenye Kanisa Katoliki, na sherehe za harusi hiyo zilifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mjini hapa. Naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Illuminata Mwenda alikiri kupokea taarifa za mtumishi huyo kukumbwa na tuhuma hiyo nzito, “Mimi ninawashauri tu watumishi wa serikali, taasisi mbalimbali na wananchi kwa ujumla wawe makini sana na kuhakikisha hawawapi kazi za kupokea fedha watu wasiowafahamu vizuri tabia zao. “Utampaje mtu nafasi nyeti ya kukusanya michango ya fedha mikubwa kiasi hicho kwa kumfahamu tu barabarani?”alihoji mkurugenzi huyo. Mkurugenzi huyo alidai mhasibu huyo ameidhalilisha halmashauri hiyo na kuahidi kukutana na uongozi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa ili kulitaka radhi kwa kitendo hicho cha aibu. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Celina Kaluba licha ya kukiri kufunguliwa kwa tuhuma za mhasibu huyo, lakini hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kwamba atamharibia kazi. Alisema hivi sasa wameanzisha msako mkali wa kumsaka mhasibu ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya dola. via Tanzania Daima

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA