Miraba Minne ya Chipukizi

Mwaka 2011 ulikuwa mzuri katika nyanja kadhaa za TZhiphop na miradi mingine, ingawa, kama kawaida,  changamoto za hapa na pale hazikosekani. Kwa upande wa wasanii, kwa ujumla wale chipukizi walioanza kusikika mwaka 2010 waliweza kujikita kwenye masikio na nyoyo za wengi. Mwamko wa mashabiki wanaoongezeka ni ushahidi thabiti.
Kwa upande mwingine, tunapenda kuwaasa mashabiki pamoja na wasanii waendelee kujifunza kuhusu historia na misingi ya Hip Hop.
Mwaka 2012 bila shaka unaonekana utakuwa mzuri zaidi. Wale waliochomoza mwaka 2010 na kufanya vizuri mwaka 2011 wanapevuka. Vivyo hivyo, wale walioanza kusikika mwaka 2011 wanaelekea kuzuri!
Wasanii wanne chipukizi wanaojitegemea wameamua kuunganisha vichwa na kuunda Miraba Minne, chini ya uongozi wa mtayarishaji wa ala, Ray.  Ndani ya Miraba Minne kuna Maalim Nash (alikuwa anatumia jina ‘Nash MC’), P The MC, msanii mpya ndani ya M-Lab, Songa, na ZAiiDKaa tayari kupokea mixtape yao kwa mikono miwili.
Tunatambulisha nyimbo zao kwa mpigo, tukianza na miradi binafsi.
 1. Songa — Songa
Songa anajitambulisha kwa wimbo unaobeba jina lake. Mitaani wanasema Songa ana ngoma kwa sababu muda wote hukohoa mistari.
2. Songa & Ghetto Ambassador — Mathematrix
Wote wawili ni wasanii wapya ndani ya  M-Lab. Kama kina Nikki Mbishi, One na Stereo walijivyojitambulisha na ‘The Element Mixtape’, utapata nafasi ya kuwasikia kina Songa na Ghetto Ambassador ndani ya ‘Mathematrix Mixtape’ inayosukwa na Duke Tachez. Mwaka huu.
3. ZAiiD ft. Dk. Remmy Ongala — Muziki Asili Yake Wapi
Baada ya kutoka na Mwanzo Mwisho, ZAiiD anarudi na Dk. Remmy Ongala katika harakati zake za kuwasha ‘Mwenge wa Uhuru’. Kama ilivyokuwa kwenye Mwanzo wa Mwisho, AK 47  aka Pallah amefanya kazi ya maana sana kwa kuenzi sauti na ujumbe wa mkongwe Remmy.
4. Maalim Nash — Maalim
Ukipewa nafasi ya kusimama mbele ya hadhira, kama Maalim, unapaswa kusema unachopigania na kuamini. Sikiliza itikadi za Nash ndani ya utamaduni wa Hip Hop.
5. Maalim Nash — Mzimu wa Shaaban Robert
Nash ana mixtape inayosambaa mitaani, inaitwa Mzimu wa Shaaban Robert Vol 1. Vol 2 inakaribia kukamilika; kuendeleza harakati za kupigania, kuheshimu na kutunza lugha yetu ya Kiswahili. Sikiliza Kionjo vya Mzimu wa Shaaban Robert, kisha mtafute Nash ili ujipatie nakala zako.
6. Miraba Minne — Vina Mpaka Uchina
Vijana waliotambulishwa hapo juu wana mitindo tofauti ya kughani na aina pekee za uandishi. Je, wakisimama kwenye wimbo mmoja, inakuwaje?
Kikosi cha TZhiphop kinawatakia wasanii wote kila la heri kwenye kazi na maisha yao binafsi. Kama vipaji wanavyo, ila wasikache kujifunza kuhusu mambo mbalimbali yanayowazunguka ili wazidi kujiendeleza. Kwa kuwa, huu ni mwanzo tu.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA