CAG Awasaka Walionufaika na Mikopo ya HESLB


Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeanza kukagua taasisi za umma kuhusu utekelezaji wa sheria inayozitaka kuwatambua waajiriwa walionufaika na mikopo ya elimu ya juu.
Hadi Mei mwaka jana, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ilikuwa imekusanya Sh65.2 bilioni kati ya Sh123.8 bilioni zilizopaswa kuwa zimerejeshwa.
Bodi hiyo iliwakopesha wanafunzi Sh1.8 trilioni tangu mwaka wa masomo 1994/95 hadi Juni 2014 kati ya fedha hizo, Sh51 bilioni zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, George Nyatega alisema ili kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mikopo iliyoiva, CAG ameanza kutekeleza matakwa ya kisheria ya ukaguzi kwenye taasisi za umma ili kuwabaini wanafunzi waliopaswa kuanza kurejesha mikopo yao.
“Ni imani ya HESLB kuwa waajiri katika utumishi wa umma watatoa ushirikiano kwa ofisi ya CAG ili kuondokana na matatizo ya kisheria,” alisema.
Nyatenga alisema sheria iliyoanzisha HESLB inazitaka taasisi zote za umma kuijulisha kwa maandishi kuhusu waajiriwa wapya ndani ya siku 28 na bodi kuthibitisha kama waajiriwa hao ni wanufaika wa mikopo au la.
Mkurugenzi huyo alisema baada ya bodi kupokea taarifa na kuthibitisha kuwa waajiriwa ni wanufaika wa mikopo, mwajiri atapaswa kuijulisha HELSB na kuanza kukata sehemu ya mshahara wa mwajiriwa ndani ya siku 30.

chanzo:global publishers

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA