UDA-RT kuanza kuuza hisa mwezi Machi

Robert Kisena
Robert Kisena

MWENYEKITI wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena, amesema UDA-RT imewekeza zaidi ya Sh bilioni 90 na kuanzia Machi mwaka huu kuna mpango wa kuanza kuuza hisa kwenye Soko la Hisa.

Pamoja na hali hiyo kampuni hiyo imeweka wazi wamiliki halali wa UDA wanaotambulika kwa mujibu wa sheria.

Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam jana kuhusu tuhuma kwamba Kampuni ya Simon Group ilipata upendeleo kununua Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), pamoja na kutoa ufafanuzi wa wanahisa halali kwa mujibu wa sheria.

Alisema hivi sasa kampuni hiyo imejikita katika kuhakikisha Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi, unaanza kwa wakati sambamba na uuzaji wa hisa.

Kisena alisema kuna mpango wa kuuza asilimia 70 ya hisa zake kwenye soko la hisa.
“Tunatarajia kupata Sh bilioni 600 ambazo zitatumika kujenga maegesho ya magari ambayo yatakuwa na huduma nyingine kama maduka na kadhalika,” 
alisema Kisena. Alisema wamiliki wa mabasi 138 ya dalalala wameshalipwa fidia ya Sh bilioni mbili ambako kila basi limelipiwa Sh milioni nne na katika fedha hizo Sh milioni moja zitabaki kama hisa.

Akizungumzia suala la umiliki wahisa wa familia ya Rais Kikwete katika UDA, alisema ni vema washindani wake wa biashara wamwache Rais mstaafu Jakaya Kikwete apumzike kwa kuwa hahusiki katika biashara zake.

Kisena alisema kuna watu wanataka kumchafua yeye katika biashara huku akiwataka wasimhusishe Rais Kikwete, badala yake wamshambulie yeye bila kuhusisha wala kuumiza watu wengine ambao hawana uhusiano na biashara zake.
“Kama kuna watu wana ugomvi wa siasa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, washambuliane wao kwa wao huko huko, wasitumie kampuni yangu kama jukwaa la mashambulio hayo.
“Mimi niliacha siasa tangu mwaka 2010… nilipongombea nikashindwa nimebaki kuwa mwanachama hai na mwaminifu kwa CCM,” 
alisema na kuongeza:
“Kampuni hii tumeipa jina la marehemu baba yangu, Mzee Simo.
Tangu imeanzishwa imekuwa kampuni ya familia, wamiliki wake ni mimi, mdogo wangu William Simon, mpwa wangu Kulwa Simon, ndugu yangu Ngalula Saguda, mke wangu na watoto wangu, imekuwa hivyo tangu ianzishwe na haijabadilishwa”.
Akizungumzia ununuzi wa hisa katika za UDA, alisema alinunua hisa zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kuuzwa (allotted shares) kwa Sh bilioni saba mwaka 2011.

Alisema baadaye mwaka 2013 alinunua hisa za Halmashuri ya Jiji la Dar es Salaam ambazo zilikuwa ni asilimia 24 ya hisa zote za UDA, kwa Sh bilioni 5.8.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA