Chuo cha Garissa kufunguliwa tena
Chuo kikuu cha Garissa, mashariki mwa Kenya, kilichofungwa mwaka uliopita baada ya watu 148 kuuawa kwenye shambulio lililotekelezwa na wanamgambo wa al-Shabab, kitafunguliwa tena Jumatatu.
Serikali imeahidi kwamba usalama umeimarishwa chuoni, na kituo cha polisi kimejengwa ndani ya chuo kikuu hicho kutoa ulinzi.
Msimamizi mkuu wa chuo kikuu hicho Prof Ahmed Warfa ameambia BBC kwamba wanaotarajiwa kufika chuo kesho ni wafanyakazi wote.
Walimu wanatarajiwa kufika chuoni kuanza muhula Jumatatu itakayofuata tarehe 11 Januari. Hakutakuwa na sherehe yoyote ya kuadhimisha kufunguliwa upya kwa chuo hicho.
Wengi wa wanafunzi walionusurika shambulio hilo la mwezi Aprili walihamishiwa vyuo vingine, lakini Prof Warfa anasema baadhi wameelezea nia yao ya kutaka kurejea.
Mwandishi wa BBC Bashkas Jugsodaay anasema kufunguliwa kwa chuo kukuu cha Garissa italeta afueni kwa wakazi na viongozi wa mkoa wa Kaskazini Mashariki ambao wamekuwa wakiisihi serikali kufungua chuo hicho, kwa walikuwa wakikitegemea kwa ajira na wateja. Wengi walikuwa wakinufaika
Wanafunzi zaidi ya 800 walikuwa wakisomea taaluma mbalimbali katika chuo hicho kabla ya kushambuliwa na magaidi.
Chuo kikuu cha Garissa ni chuo kishirikishi cha Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret na wasimamizi wa chuo kikuu hicho cha Eldoret wamekuwa wakisaidia katika juhudi za kufunguliwa upya kwa chuo hicho.
Wengi wa wanafunzi waliokuwa Garissa walijiunga na chuo hicho cha Moi.
Matumaini ya kufunguliwa upya kwa chuo kikuu hicho yaliibuka mapema Desemba baada ya Naibu Rais William Ruto kukutana na viongozi wa kisiasa wa eneo hilo na kutangaza kimefunguliwa katika muda wa wiki mbili.
Hata hivyo, aliachia wasimamizi wa chuo uhuru wa kuamua tarehe kamili ya kufunguliwa upya kwa chuo hicho.
chanzo:BBC
Comments
Post a Comment