Serikali kugawanya kwa uwiano madaktari na mabingwa nchini

1/12/2016 10:23:00 PM
Mheshimiwa Ummy Mwalimu akizungumza na Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Peramiho, Dk Venance Mushi, alipotembelea hospitali hiyo 
SERIKALI imesema itapanga mgawanyo maalumu ili mikoa yote iweze kunufaika na huduma za Madaktari na Madaktari bingwa na kutatua kero za wananchi wanazopata za kufunga safari ndefu kuhangaikia huduma za wataalamu hao.

Aidha itaendelea kushughulikia suala la kuboresha mazingira ya kazi kwa Madaktari na watumishi wa Sekta ya Afya kwa ujumla ikiwa ni pamoja na maslahi yao ili kuwafanya wahamasike kufanya kazi hapa nyumbani badala ya kwenda kufuata maslahi makubwa nje ya nchi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa huduma za madaktari bingwa mkoani Ruvuma jana

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Daktari John Magufuli, imedhamiria kukabiliana na upungufu wa Madaktari kwa kuanzisha utaratibu maalumu wa mgawanyo huku ikiongeza idadi ya wahitimu wa fani hiyo katika vyuo mbali mbali vya Udaktari hapa nchini.

“Kama mtakumbuka hivi sasa kuna mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Muhimbili unaoendelea katika eneo la Mlongazila, vilevile kuna ujenzi wa Hospitali ya kisasa unaoendelea katika Chuo Chuo Kikuu cha Dodoma, kote huko kunatarajiwa kutoa Madaktari wa kutosha ili kuziba pengo la Madaktari na Madaktari Bingwa lililopo hivi sasa.” Alisema waziri ummy.

Alisema mipango hiyo iliyoanza katika Awamu ya Nne itaendelezwa kwa kasi zaidi ili taifa lifikie lengo la kuwa na Madaktari Bingwa karibu zaidi na wananchi wengi kwani imeonekana kuwa kuna mlundikano mkubwa wa Madaktari na Madaktari Bingwa sehemu za mijini kama vile katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza na Arusha.

Katika uzinduzi huo ambapo pia alikabidhi hospitali ya rufaa Songea dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi milioni tano, pamoja na mashuka mia tatu, Waziri Ummy aliuagiza Mfuko wa taifa wa Bima ya Afya, kuongeza kasi ya kusajili wanachama wapya ili kuwapunguzia wananchi adha ya gharama za matibabu.

Aliwataka viongozi mbalimbali kusaidia jitihada hizo ili kuhakikisha kwamba wananchi Tanzania wanapata huduma za afya wanapozihitaji na kwa gharama nafuu kwa kuwa katika mfuko wa NHIF.
Aidha alisema serikali itafanyia kazi uwasilishaji wa muswada wa Sheria ambayo itamtaka kila mwananchi awe mwanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

“Ni matumaini yangu kuwa utekelezaji wa Sheria hii utasaidia kuboresha huduma za matibabu na kuondoa changamoto ya ufinyu wa rasilimali kwa ajili ya kuendeshea huduma za afya kwa wananchi wa Tanzania” alisisistiza waziri Ummy.

Akizungumzia uboreshaji wa huduma za matibabu zinazotolewa kwa wananchi hususan katika maeneo ya vijijini kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) unaosimamiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya alisema amfurahishwa na Kazi ya kuboresha miundo mbinu na kuongeza makundi mbalimbali ambapo hadi Desemba 2015 jumla ya wanufaika 6,677,241 walijiunga katika Halmashauri 144 nchini, hii ni asilimia 15.3 ya Watanzania wote.

Hata hivyo alisema Mkoa wa Ruvuma una changamoto kubwa ya halmashauri zake kuwa na idadi ndogo ya wanufaika waliojiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Hadi kufikia tarehe 31 Disemba 2015 idadi ya wanufaika ilikuwa ni 188,136 kati ya walengwa 1,376,891 ambayo ni sawa na asilimia 14 ya lengo la uandikishaji kimkoa.

Alizihimiza Mamlaka za Halmashauri zote nchini, kuhakikishe zinatumia vyanzo mbalimbali vya mapato vinatokana na uchangiaji wa huduma za matibabu kutumia fedha hizo kuboresha huduma ikiwemo dawa, vitendanishi na vifaa tiba.

Awali katika hotuba yake ya utambulisho Kaimu Mkurugenzi wa NHIF, Michael Mhando aliomba uongozi wa Mkoa na Halmashauri zote, ziandae programu maalum ya uhamasishaji wananchi kwa lengo la kurudisha hadhi ya mkoa wa Ruvuma kwenye CHF ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ndio iliyokuwa ya kupigiwa Mfano ndani na nje ya nchi.

Aidha alisema Mpango wa huduma za madaktari bingwa mkoa wa Ruvuma unatekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watotokwa kuwatumia Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, MOI na Hospitali za Rufaa za Kanda.

Alisema mpango huo umeshatekelezwa katika mikoa kumi na tatu hadi sasa.

Alisema kabla ya kutekeleza mpango huu hapa mkoani Ruvuma, waliwatuma Madaktari wao ambao walishirikiana na Madaktari mkoani Ruvuma kubaini mahitaji halisi ya wananchi katika huduma hizo za Madaktari bingwa na kukubaliana kuwa wanahitaji zaidi huduma za Madaktari bingwa katika maeneo ya magonjwa ya masikio, pua na koo, mfumo wa njia ya mkojo, magonjwa ya watoto, magonjwa ya ndani na moyo, pamoja na bingwa wa dawa za usingizi na wagonjwa mahututi.
mwisho

Baadhi ya wanachama wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), wakiwa sehemu ya mapokezi, tayari kwa kupata huduma
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu ametembelea jengo la zahanati ya Mpingi, wilaya ya Songea Vijijini na kuzungumza na wanakijiji wa eneo hilo.

Ziara hiyo ni moja kati ya kazi anazozifanya mkoani hapa kwa lengo la kuzungumza na wananchi, watoa huduma na watumishi wa sekta ya afya ili kuboresha huduma za matibabu na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za afya ikiwemo uchangiaji katika mfuko wa Bima ya Afya.

Baada ya kufika kijijini hapo na kuona jitihada zilizofanywa na na wananchi katika kujenga zahanati ya kijiji, Waziri Ummy aliwaahidi wananchi hao mabati na misumari ili kuunga mkono ujenzi wa zahanati hiyo.


Mheshimwa Ummy Mwalimu akisaini kitabu cha wagenii kijijini Mpingi


Baadhi ya wananchi wa Mpingi waliohudhuria kumlaki Waziri Ummy Mwalimu alipotembelea majengo ya zahanati yao



Waziri Ummy Mwalimu akiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Benson Mpesya, kutembelea majengo ya zahanati ya Kijiji cha Mpingi


Mzee Mohamed Mussa, mkazi wa kijiji cha Mpingi akimshukuru Waziri Ummy Mwalimu kwa kutembelea kijiji chao na kutoa msaada wa bati na misumari ya kukamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA