Serikali yawaonya wenye 'blogs'

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Clement Mshana amewataka wamiliki wa mitandao ya habari maarufu kama 'Blogs' na wale wa magazeti ya udaku kuacha mara moja kuweka picha na habari zinazodhalilisha jamii.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa wanahabari mjini Morogoro, Mshana alisema Tanzania imekuwa na ongezeko kubwa la vyombo vya habari tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi.

"Hilo ni jambo zuri katika kutoa habari za kuwaelimisha, kuwaburudisha na kuwahabarisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali yakiwamo ya afya, siasa, maendeleo na ustawi wa jamii kwa ujumla hasa pale habari hizo zinapokuwa zimeandikwa kwa ufasaha bila udhalilishaji. "Lakini utakuta katika blog, badala ya kuwekwa habari na picha za kuelimisha jamii, zinawekwa picha za watu wakiwa uchi! Huku ni kuwadhalilisha watu. Ijulikane kuwa mitandao hiyo husomwa pia na watoto wadogo, hii inawafundisha nini?" alihoji Mshana.

Hata hivyo, alisema si magazeti yote ya udaku yanayokiuka maadili ya Mtanzania kwani yapo baadhi yanayoandika habari nzuri na za kuelimisha jamii na ndiyo yanayopaswa kuendelea kuwapo katika jamii hii.

Alibainisha kuwa tayari wahariri kadhaa wa vyombo vya habari vya aina hiyo wamekwishaitwa na kuelekezwa kuwa kuna baadhi ya mambo wanayoyafanya hayakubaliki na wasipojirekebisha, watafungiwa.

"Na amri hii inakwenda hata kwa wale wanaodhani kuwa wanamiliki blogs binafsi na hata wanaochangia blogs hizo kwa kutuma maoni, wanapaswa kujirekebisha," alisema.



Habari hii nimeichukua katika gazeti la Mtanzania, toleo la leo, ikiwa imeandikwa na Rose Chapewa wa Morogoro.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA