Wanachuo DSJ wabakwa kwa zamu

Kundi la vibaka zaidi ya 15 limevamia wanachuo wa kike wanaolala katika hosteli ya Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ) iliyoko Ilala, Dar es Salaam na kuwabaka kwa zamu.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotaja majina yao, baadhi ya wanachuo waliovamiwa walisema kuwa, vibaka hao waliwavamia juzi majira ya saa nane usiku.

“Sisi tulikuwa tumelala kama kawaida, ilipotimia majira ya saa nane za usiku, tukasikia kelele nje ya geti ambazo zilionyesha kuwa mlinzi wetu Mmasai alikuwa ametekwa na hao vibaka.

“Baada ya vurugu za muda mrefu kidogo, inaonekana mlinzi alizidiwa nguvu, akafungwa kamba miguuni na mikononi na kulazwa chini. Walipomalizika zoezi hilo, wakaja chumbani kwetu, mimi nilikuwa nilelala na mwenzangu, wakagonga mlango kwa nguvu wakitutaka tufungue.

“Sisi tukakataa kufungua, wakaanza kututishia kwamba kama tumegoma kufungua mlango basi watauvunja na wakiingia ndani watatuua ama watatufanyia kitendo kibaya sana ambacho hatutasahau maishani.

“Tuliposikia hivyo, tukaamua kufungua, wakaingia ndani, wakaanza kutupiga na kutwambia tuwape pesa, simu na ‘laptop’ na kama hatuna vitu hivyo, watubake. Tukaogopa, tukawapa vyote walivyotaka, wakatuacha wakahamia vyumba vingine ambapo kazi yao ilikuwa ni ile ile ya kutaka pesa na wale ambao hawakuwa na pesa za kutosha waliwabaka kwa zamu.

“Hapa inaonekana waliobakwa ni wengi, ila wengine wanaficha, lakini aliyeweka ukweli wazi ni mmoja na hivi tunavyozungumza, amepelekwa Hospitali ya Amana kwa ajili ya uchunguzi,” alisema mmoja wa wanachuo hao.

Mkuu wa chuo hicho, Joakim Lupepo, alipoulizwa juu ya tukio hilo, alikiri wanachuo hao kuvamiwa na kumtaka Mwandishi Wetu awasiliane na Makamu Mkuu wa Chuo, Yusto Satipa, ambaye ndiye alikuwa akishughulikia suala hilo.

Satipa alikataa kuzungumzia tukio hilo kwa kile alichoeleza kuwa, hana mamlaka yoyote, badala yake akamtaka Mwandishi Wetu arudi tena kwa mkuu wa chuo kwa kuwa ndiye msemaji wa chuo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Faustine Shilogile, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea.

“Ni kweli wanachuo hao wamevamiwa na mmoja ndiye aliyethibitika kubakwa kwa mujibu wa ripoti niliyoletewa na maofisa wangu. Lakini katika hosteli hiyo kuna mazingira mabovu, kwa sababu geti halifungwi kama ilivyo vyuo vingine, hapo geti linaachwa wazi masaa yote na wanachuo wanaruhusiwa kutoka na kuingia muda wowote wanaotaka,” alisema Kamanda Shilogile.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA