Maagizo ya Waziri Mkuu Majaliwa baada ya kusafiri kwa mabasi yaendayo haraka
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
*Ataka watu walipe tiketi rasmi, wafuate taratibu
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekagua utendaji kazi kwenye mabasi ya mwendokasi
yanayotoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam na kubaini changamoto
kadhaa ambazo amesema zitarekebishwa kadri mradi unavyoendelea.
Waziri
Mkuu ambaye alilipa nauli na kupanda basi namba 23 lenye usajili namba
T125 DGW kuanzia kituo cha Ferry, Kivukoni, ametumia muda wa dakika 50
kufika Kimara mwisho kwa kutumia usafiri huo.
Waziri
Mkuu alipanda basi hilo saa 3:30 asubuhi na lilianza safari saa 3:33
baada ya kusubiri wengine wapande. Kwa wastani ililtumia kati ya dakika
mbili hadi tatu kutoka kituo kimoja hadi kingine. Basi hilo liliwasili
Kimara Mwisho saa 4:23 asubuhi.
Akizungumza
na waandishi wa habari akiwa Kimara mwisho mara baada ya kumaliza ziara
hiyo fupi ya ukaguzi jana (Ijumaa, Mei 27, 2016), Waziri Mkuu alisema
aliamua kufanya ziara hiyo ya ghafla ili kuangalia matumizi ya njia za
mabasi yakoje na pia kuona abiria wanaelewa vizuri namna ya kuitumia
huduma hiyo.
Amesema
ameridhishwa na mradi unavyofanya kazi ila ameelezwa kuna usumbufu
kwenye mageti wakati abiria wanapotaka kuthibitisha tiketi zao hasa
wakati wa asubuhi kunapokuwa na msongamano wa abiria. Pia alielezwa
kwamba kuna baadhi ya abiria wanakuja na tiketi za jana yake jambo
ambalo linaleta usumbufu kwa sababu hazitambuliki kwenye mfumo wao.
“Nimeridhishwa
na uharaka wa njia kwa sababu na mimi mwenyewe nimetumia dakika 50
kufika hapa ingawa kuna maeneo nimeona kuna haja ya kuwa na taa maalum
za kuzuia magari (special sensors) wakati mabasi yakipita ili kuepusha
ajali,” alisema.
Aliyataja
maeneo hayo kuwa ni kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na mtaa wa
Samora, Morogoro na Jamhuri na makutano ya Morogoro na Kisutu.
Waziri
Mkuu aliwataka Watanzania waende na tiketi rasmi badala ya kutumia
tiketi za jana kwa sababu kufanya hivyo ni makosa na mtu anakuwa
amedhamiria. “Hawa watachukuliwa hatua za kinidhamu. Mtu akija na tiketi
ya jana akamatwe na kupelekwa polisi, huyu atakuwa amedhamiria,”
alisema Waziri Mkuu wakati akiongea na mhudumu mmoja katika kituo cha
Kimara Mwisho.
“Ninawasihi
wananchi wanaotumia usafiri huu wajifunze kufuata utaratibu na
kuwasisitizia kuwa kila abiria aje na tiketi ambayo ni rasmi,” alisema
na kuongeza: “Haya mabasi nimebaini yako vizuri. Ninatoa msukumo kwa
watumishi wa umma wapande mabasi haya ili kupunguza msongamnao wa magari
barabarani.”
Katika
kupiunguza baadhi ya changamoto, Waziri Mkuu alisema Serikali itasimamia
uboreshaji wa ukataji tiketi ili kuondoa usumbufu kwa abiria. Pia
alivionya vyombo vya moto viache kutumia njia maalum ya mabasi hayo.
Pia
aliwataka polisi wanaofanya doria za usiku kupita kwenye fly-overs na
kuwaondoa watu wanaolala kwenye maeneo kwani wanahatarisha usalama wa
watu wanaotumia njia hizo. “Zile siyo sehemu za kulala, wanaofanya hivyo
wanahatarisha usalama wa watumiaji wa njia hizo, kwa hiyo polisi
wakiwakuta watu wa aina hiyo wawakamate mara moja,” alisema.
Kwa
upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed
Mpinga ambaye alifuatana na Waziri Mkuu kaktika ziara hiyo, alisema
amepiga marufuku magari na pikipiki kutumia njia hiyo hata kama ni
magari ya Serikali.
“Tulishapiga
marufuku magari na pikipiki kutumia njia hiyo hata kama ni magari ya
Serikali, ninawasihi madereva watambue hili na watii,” alisema.
Machi 22,
mwaka huu Waziri Mkuu alitembelea soko la Feri kwa lengo la kuangalia
mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo (kuzuia moshi) na kukagua ujenzi wa
ukuta unaotenganisha soko hilo na mabasi yaendayo kasi.
Aprili
15, mwaka huu, Waziri Mkuu alifanya kikao na kuwaagiza wakuu wa taasisi
zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanatoa elimu kwa
umma ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza pindi majaribio
yakianza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
IJUMAA, MEI 27, 2016.
Comments
Post a Comment