MAJALIWA:WANAVYUO WAFUATE TARATIBU NA SHERIA ZILIZOPO VYUONI
SERIKALI imekanusha madai ya kutoa maelekezo kwa Uongozi wa vyuo vya elimu ya juu ya kuwanyanyasa wanafunzi wa vyuo hivyo wanaojihusisha na masuala ya siasa na badala yake imewataka wafuate kanuni na taratibu zilizowekwa sehemu husika.
Hata hivyo imesema itaendelea kuwahudumia Watanzania wote ikiwemo kutoa elimu kuanzia ngazi awali hadi elimu ya juu bila kujali ya itikadi za dini wala vyama vyao vya siasa.
Waziri Mkuu,Kassm Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi, Mei 5, 2016) wakati akijibu swali la papo kwa papo la Mheshimiwa Ester Matiko (Viti maalum Chadema) aliyetaka kujua kama Serikali imetoa maelekezo kwa uongozi wa vyuo vikuu kunyanyasa wanafunzi wanaojihusisha na masuala ya siasa.
“Nakanusha si kweli kwamba kuna maelekezo kwenye vyuo vyote vya elimu ya juu na pia hakuna unyanyasaji wowote wa vyuo na Watanzania wote wanao uhuru wa kujiunga na vyama vyote wanavyovitaka, lakini kila eneo limeweka utaratibu wake hivyo wafuate taratibu na sheria katika sehemu husika,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeondoa tozo ya asilimia 15 ya eneo la manunuzi ya vifungashio katika zao la korosho ili kumfanya mkulima kupata tija zaidi.
Akijibu swali la papo kwa papo la Mheshimiwa Katani Katani (Tandahimba-CUF) aliyetaka kujua ni lini tozo hiyo itaondolewa, Waziri Mkuu Majaliwa amesema tayari tozo hiyo imeshaondolewa na gharama hizo kwa sasa zipo katika mfuko wa wakfu ulioundwa na wadau wa zao hilo na unachangiwa na asilimia 65 ya tozo za korosho zinazouzwa nje.
Amesema mfuko huo wa wakfu unatakiwa kusimamia upatikanaji wa masoko ya zao la korosho, kununua pembejeo, kusimamia uboreshaji na upanuzi wa mashamba na kugharamia tatifi mbalimbali kwa ajili ya kupata ubora wa zao hilo.
Akijibu kuhusu suala la madai ya wakulima ambao korosho zao zimepotea ghallani, amesema mfumo wa uuzwaji wa zao hilo wa stakabadhi ghalani ni wa kiushirika na unasimamiwa na Mrajisi ni vema wakulima wakadai haki yao katika mikutano ya ushirika wao na kama hawaridhiki na majibu waende mahakamani ili kupata haki yao.
Amesema kwa sasa Serikali itahamishia nguvu zake katika kusimamia mazao mengine ya pamba, tumbaku na kahawa kama walivyofanya kwenye zao la korosho ili wakulima wa mazao hayo nao wapate tija.
Akijibu swali la Mheshimiwa Joseph Kekunda (Sikonge-CCM) aliyetaka kujua Serikali inampango gani wa kutatua migogoro ya wakulima na wakulima ,Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha inakomesha migogoro hiyo ambazo ni pamoja na kupima maeneo na kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi.
Pia kuweka mipaka katika maeneo mapya na kutumia ranchi zilizopo kwa ajili ya wafugaji wakubwa na kwamba itatenga maeneo ya kilimo na kuyabainisha kwa wananchi ili kuepuka muingiliano uliopo hivi sasa
Comments
Post a Comment