Viwango vya tozo za kuvuka daraja la Nyerere / Toll rates for Nyerere bridge crossing


Katibu Mkuu wa Wizara  ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga
SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imetangaza rasmi tozo zitakazotumika katika Daraja la Nyerere jijini Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga, amesema kuwa tozo hizo zitaanza kutumika rasmi Jumamosi wiki hii na zitahusisha vyombo vyote vya usafiri.

“Tumeanza kutoza tozo hii mara baada ya kufunguliwa kwa daraja hili na kuanza kutumika kwa kupita bila kulipa kwa vyombo vya usafiri tangu Aprili 19 mwaka huu na sasa tunaanza rasmi kutoza tozo kwa ajili ya kukusanya gharama za usimamizi, utunzaji na uendeshaji wa daraja hili.

“Hakikisheni mnazifahamu tozo zote zitazotumika katika daraja hili kwa magari ya aina zote ili kuondoa usumbufu wakati wa utekelezaji wa zoezi la malipo”, Amesema Eng. Nyamhanga.

Nyamhanga amefafanua kwamba watembea kwa miguu watapita bure katika daraja hilo huku wenye baiskeli wakilipia Sh. 300, pikipiki Sh. 600,  mikoteteni, guta, bajaj na magari madogo (salon cars, sedan) yatatozwa shilingi 1500, wakati magari aina ya ‘pick up’ yatakayozidi tani mbili na mashangingi yatatozwa shilingi 2000.

Amefafanua kuwa mabasi yanayobeba abiria wasiozidi 15 (mini bus) yatatozwa shilingi 3000, mabasi yanayobeba abiria kuanzia 15 hadi 29 yatatozwa shilingi 5000 huku mabasi yanayobeba abiria zaidi ya 29 yatatozwa shilingi 7000.

Aidha trekta na magari yenye tani 2 hadi 7 yatalipia Sh. 7,000, tani 7 hadi 15 watalipa Sh.10,000, tani 15 mpaka 20 watalipa Sh.15,000 na yale yenye tani 20 mpaka 30 yatalipia Sh. 20,000.

Ameongeza kuwa matrekta yenye matrela, magari makubwa yenye uzito wa tani saba hadi 15 yatatozwa shilingi 10,000 wakati magari yenye uzito wa tani 15 hadi 20 yatatozwa shilingi 15,000.

Katibu Mkuu Nyamhanga ameongeza kuwa magari yenye uzito usio wa kawaida (abnormal load) yatapita kwa vibali maalum vinavyotolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Amesisitiza kuwa tozo zote zimezingatia maoni ya wadau na hali ya uchumi wa wananchi ili kumudu gharama za matumizi ya daraja hilo.

“Magari yote ya Serikali na taasisi za umma yatatakiwa kulipa tozo kama ilivyobainishwa isipokuwa yale yenye namba za jeshi (Magereza - MT, Polisi - PT, JWTZ, Zimamoto) na magari ya wagonjwa”, na magari yenye vibali maalum, amesisitiza Eng. Nyamhanga.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Uwekezaji kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (N.S.S.F), Yacoub Kidula, amewataka wananchi kuchangia gharama za uendeshaji wa daraja hilo ili kuongeza mapato ya Serikali.

Takribani wiki tatu magari yamekuwa yakivuka katika Daraja la Nyerere bila tozo ambalo lilifunguliwa katikati ya mwezi Aprili mwaka huu na Rais wa awamu ya Tano Mhe. John Pombe Magufuli.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA