Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) jana aligoma kuwekewa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, hivyo kulazimika kwenda rumande katika Gereza la Kisongo kwa siku 14.
Wakati washtakiwa wenzake 18 wakiachiwa kwa dhamana, Lema alikataa kudhaminiwa hata baada ya kujitokeza kwa wadhamini kutimiza masharti yaliyotolewa na mahakama.
Badala yake mbunge huyo alisambaza waraka ulioeleza msimamo wake wa kukataa dhamana na kuwa tayari kwenda rumande akidai hivyo ni vita dhidi ya uonevu na ukandamizaji wa haki na utu wa binadamu.
Lema katika waraka huo alisema amechoka kuishi kwa vitisho vya kila siku kutoka kwa polisi hao, na sasa hawezi tena kuogopa lolote linalotokana na msimamo wake wa kuwatetea wanyonge na maskini wanaoishi kwa kukandamizwa na utawala.
‘Leo nitakwenda jela kwa hiyari yangu binafsi kwa siku kadhaa na si kwa nia ya kutafuta utukufu wangu bali kwa kupinga ukandamizaji wa haki za binadamu.
‘Sioni ugumu kuchukua maamuzi haya ninayotoa leo ; upendo huu nilionao kwa watu wa Arusha na nchi yangu ni sababu ya msingi ya kufikia maamuzi haya. Nimetishwa mara nyingi, rafiki zangu wametishwa, jamii ya watu duni imeendelea kuishi katika hali duni kwa mashaka na vitisho kwa muda mrefu,’ alisema katika waraka huo.
Mbunge huyo ambaye jana alikaririwa na Tanzania Daima akielezea hofu ya usalama wa maisha yake, alisema, ‘Wala sintoogopa jela yoyote katika kupigania haki, utu wa kweli katika jamii yangu na wasifikiri wataendelea kutuogopesha kwa sababu wana jela na silaha, wanafikiri tutaendelea kuabudu uogo na wanafikiri wataendelea kutunyanyasa bila sababu za msingi, lakini sisi tunajua tutashinda kwa sababu haki tunayoipigania ni makusudi ya Mwenyezi Mungu,’ alisisitiza.
Lema aliongeza katika waraka huo kuwa wapinzani wanaojaribu kutetea haki za wanyonge wanakamatwa hovyo kwa makosa ya kutunga ili kuwanyamazisha. Aliongeza kuwa Watanzania wengi wamefungwa kwa uonevu na serikali imeacha kuhangaika kwa ajili ya maskini waliokosa huduma za msingi kama chakula, malazi, huduma za afya, ajira na wengi kukimbia familia zao kwa kukosa matumaini ya maisha.
Ameongeza kuwa badala yake imewakumbatia watu wachache waliopora utajiri wa nchi kwa manufaa yao binafsi, huku wakinunua haki na sheria dhidi ya wajane na wanyonge na wengine kuwapora mashamba na raslimali za wananchi.
Alisema serikali imeamua kutumia polisi kuwakandamiza, ili kuwatisha wasitetee haki za watu, jambo ambalo alisema kamwe hatafumba mdomo hata ikimlazimu kufa.
‘Na sasa siwezi kukaa kimya tena, ni afadhali vita inayotafuta haki na usawa kuliko amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mwanadamu na katika msingi huu, hofu na mashaka umekosa thamani kwangu, sintamwogopa mtu yeyote, mwenye silaha na mwenye cheo chochote,’ alisema.
Lema pamoja na wafuasi 18 wa CHADEMA jana walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya mjini Arusha Judith Kamara wakikabiliwa na mashtaka manne, ya njama za kufanya kosa mahakamani, kufanya maandamano yasiyo ya halali, kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri halali ya polisi iliyowataka kutawanyika.
Mara baada ya kukana mashtaka hayo, Hakimu Mkazi Judith Kamala alisema dhamana ipo wazi kwa washtakiwa na kutoa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye barua toka kwa mtendaji wa kata na sh 500,000.
Baada ya kukataa kudhaminiwa licha ya kubembelezwa na viongozi wenzake, Lema aliondolewa mahakamani hapo majira ya saa 9 alasiri chini ya ulinzi mkali akiwa ndani ya gari la polisi aina ya Land Rover ya polisi yenye namba za Usajili T 422 AGK lililosindikizwa na gari jingine lililosheheni askari wenye silaha za moto.
Umati mkubwa wa wafuasi wa CHADEMA ulifurika katika mahakama hiyo, huku polisi wengi wakiwa wamevalia nguo za kiraia wakiwa wametapaa kila kona ya mahakama hiyo.
Washtakiwa walitimiza masharti ya dhamana ni pamoja na Diana Anthony, Gerald Majengo, Hassan Mdigo, Lomaiyan Nassi, Rashidi Shumbeti, Daudi Hamza na Bahati Daudi.
Washtakiwa wengine ni Kelvin Simon, Amendeus Chami, Meshack Betuel, Hamadi Shabani, Richard Mollel, Frank Daniel, Leonard Kiologo, Juliana Lukumay, Jafarry Samwel, Mussa Mwakilema, Dina Kamtoni na Joseph Simon, ambapo kesi hiyo itatajwa tena Novemba 14 mwaka huu katika mahakama hiyo.
habari hii ni kutoka Tanzania Daima
Comments
Post a Comment