Kocha Stars aja leo, kuanzia kibarua

KOCHA mpya wa Taifa Stars, Jan Poulsen anatua nchini leo kuanza kibarua chake kipya ambacho kitaanzia rasmi Cairo, Misri dhidi ya mabingwa wa Afrika, Mafarao, Agosti 11.

Poulsen, raia wa Denmark atawasili nchini leo usiku kuinoa Stars iliyoachwa na Marcio Maximo aliyemaliza muda wake mwanzoni mwa mwezi.

Kulingana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mechi hiyo ambayo ni ya kirafiki ya kimataifa ilipangwa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa,Fifa.

Ofisa Habari waTFF, Florian Kaijage, alisema jana kuwa baada ya kuwasili nchini Poulsen atakuwa na jukumu la kuanza mchakato wa kuteua wachezaji wa Stars na kuwaandaa kwa mechi hiyo siku kumi baadaye.

Kaijage alisema kuwa ni matarajio ya shirikisho hilo kuwa mechi hiyo itakuwa sehemu muhimu ya matayarisho ya Stars kuanza harakati za kusaka tiketi ya kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika za mwaka 2012 zitakazoandaliwa kwa pamoja na Gabon na Guinea ya Ikweta.

"TFF imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuhakikisha Stars inapata mchezo wa kujipima nguvu ambao unaendana na aina ya mashindano ambayo yanaikabili timu hiyo ya taifa.

"Jitihada hizo sasa zimefanikiwa kwa kupata mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Misri ambao Stars itacheza ugenini mjini Cairo," alisema Kaijage.

Harakati za Stars kufuzu zitaanza mwanzoni mwa Septemba ambapo Tanzania itavaana na Algeria ugenini katika mchezo wa kwanza wa Kundi D barani Afrika.

Baada ya hapo, Stars itarejea nyumbani mwezi Oktoba kupambana na Morocco.
Nchi nyingine iliyo kundi moja na Tanzania ni Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kuhusu ujio huo wa Poulsen, Kaijage, alisema atakuwa na mazungumzo mafupi na wanahabari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

"Ni matarajio yetu (TFF) kwamba Poulsen atapata ushirikiano kutoka kwa wadau wa mpira wa miguu ikiwemo wadhamini, vyombo vya habari na mashabiki ili aweze kufanya kazi yake kwa utaalam na hatimaye kuiwezesha nchi yetu kupiga hatua katika maendeleo ya soka.

"Kama ambavyo iliwahi kuelezwa awali, Poulsen ni kocha wa kiwango cha kimataifa na mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25", alisema Kaijage.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA