Poulsen awatema Tegete, Yondani, wengine watano

KOCHA wa Taifa Stars, Jan Poulsen amewaacha wachezaji saba mahiri kwenye safari ya Algeria kwa sababu ambazo ameziita kuwa za kiufundi na ushindani mkubwa kwenye kikosi chake.

Kikosi hicho cha wachezaji 20 kitakachoondoka Jumanne kwenda Algeria kwa mchezo huo wa kwanza za kusaka tiketi ya kufuzu kwa fainali za Afrika mwaka 2012.

Timu hiyo itaondoka kwa ndege ya Shirikika la Ndege la Qatar Airways kuelekea Algiers.

Wachezaji walioachwa ni pamoja na Uhuru Seleman, Kelvin Yondani, Juma Jabu, Abdulhalim Humoud , Jerryson Tegete, Athuman Idd 'Chuji' na kipa Juma Kaseja.

Poulsen alisema wachezaji hao wameachwa kwa sababu mbalimbali za kiufundi. Alisema Chuji na Kaseja bado ni majeruhi.

“Chuji amepata nafuu , lakini hajakuwa na mazoezi kwa muda mrefu, siwezi kusafiri naye kwani hawezi kucheza, hali ambayo ni sawa kwa Kaseja ambaye nimempa muda zaidi wa kupona,” alisema Poulsen.

Aliongeza kuwa Abdulhalim Humud, ambaye anaichezea Simba ameachwa kwa sababu ya timu yake kuwa na viungo wanne wenye nguvu ambao wanaweza kuziba nafasi hiyo.

“Ninao Nurdin Bakari, Henry Joseph, Abdi Kassim na Shaaban Nditi kwenye nafasi hiyo, wote wanaweza kucheza vizuri na ni viungo wakabaji ,” alisema.

Kulingana na maelezo yake, wengine wameachwa kutokana na ushindani wa namba kwenye kikosi chake.

Hicho ndicho kilichomkumba beki Kelvin Yondani, pia wa Simba ambaye ameshindwa kumudu kasi ya Aggrey Morris huku Juma Jabu akiachwa kwa sababu katika nafasi yake ya beki wa kushoto wapo pia Stephano Mwasika kutoka Yanga na Idrissa Rajab anayecheza soka ya kulipwa kwenye klabu ya Sofapaka ya Kenya.

Tatizo hilo, ndilo limempata pia Uhuru ambaye amekuwa akichuana na Jabir Aziz ambaye anao uwezo wa kucheza kama kiungo wa kushoto au kulia au pengine mkabaji.

Kuhusu mshambuliaji ambaye amekuwa tegemeo Stars, Tegete, kocha huyo ameeleza kuwa ameshindwa kukabiliana na changamoto kutoka kwa kina John Bocco, Mussa Hassan ‘Mgosi” na Danny Mrwanda anayecheza soka kwenye klabu ya Dong Tam Long ya Vietnam.

Lakini, Poulsen alieleza kuridhishwa na viwango vya wachezaji wa Tanzania wanaocheza soka ya kulipwa nje na ana imani kuwa wataisaidia timu yake kwenye mchezo huo wa awali na mingine inayofuata ya michuano hiyo.

“Wana uwezo, viwango vya kimataifa, nimawaamini kuwa wataisaidia timu yetu inayokabilwia na mchezo mgumu wa ugenini,,” alisema.

Kikosi kamili.

Makipa : Shabani Kado (Mtibwa) na Jackson Chove (Azam ).

Mabeki : Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub, Stephano Mwasika (Yanga), Salum Kanoni,(Simba), Idrissa Rajab (Sofapaka), Aggrey Morris nad Erasto Nyoni (Azam).

Viungo : Jabir Aziz, Selemani Kassim (Azam), Shaaban Nditi (Mtibwa), Nurdin Bakari, Abdi Kassim (Yanga ), Henry Joseph (Kongsving).

Washambuliaji: Danny Mrwanda (DT Long), Nizar Khalfan (Whitecaps), John Bocco, Mrisho Ngasa (Azam), Mussa Hassan Mgosi (Simba).

Akizungumzia mchezo huo, Poulsen alisema anaamini kikosi chake kitaiwakilisha vyema Tanzania katika michuano hiyo, hivyo ni matumaini yake kuwa watashinda mchezo huo wa awali na hatimaye kufanikiwa kusonga mbele katika michuano hiyo.

"Tumefanya maandalizi ya kutosha na kila mmoja wetu anafahamu nini anakwenda kufanya kikubwa tunahitaji ushirikiano baina yetu na tunaomba sapoti ya Watanzania ili tuweze kuiwakilisha nchi vyema,"alisema Nsajigwa.
Wakati huo huo; Mwamuzi wa kati kutoka Togo, Djobi Kokou ameteuliwa kuchezesha mechi ya kwanza ya michuano ya awali ya Mataifa ya Afrika baina ya Tanzania na Algeria itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mustapha-Tchaker mjini Bilda.

Mwamuzi huyo atasaidiwa na Watogo wdenzake, Djoukere Biagui na Ayena Mathias, ambao wote walichezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baina ya JSK na Al-Ahly iliyofanyika mjini Cairo ambako wageni walishinda kwa bao 1-0.

Katika mechi nyingine ya Kundi D siku hiyo, Morroco itakuwa aikivaana na Afrika ya Kati.
Kocha wa Algeria, Rabah Saadane amekuwa akifuatilia wachezaji wake wanaosakata soka barani Ulaya wakati akijiandaa kusuka kikosi kitakachokaribisha Stars katika mechi hiyo ya Septemba 3.

Katika kikosi chake alichokiteua nkwa ajili ya mechi hiyo, Saadane ameita wachezaji wawili wapya ambao ni Amri Chadli anayechezea klabu ya Kaiserslautern ya Ujerumani ambaye amerejeshwa kuziba nafasi ya Medhi Lacen, na Mohamed Chakouri anayechezea Charleroi ya Ubelgiji.

Kikosi kamili ni kama ifuatavyo
Makipa: Lounes Gaouaoui (USM Blida), Rais Mbolhi (Slavia Sofia, Bulgaria), Mohamed Amine Zemmamouche (MC Alger)
Mabeki: Mohamed Chakouri (Charleroi, Ubelgiji), Habib Bellaid (Eintracht Francfort, Ujerumani), Madjid Bougherra (Glasgow Rangers, Scotland), Rafik Halliche (Benfica, Ureno), Abdelkader Laïfaoui (ES Setif), Carl Medjani (AC Ajaccio), Nadir Belhadj (Al-Sadd), Djamel Mesbah (Lecce, Ufaransa).
Viungo: Adlene Guedioura (Wolverhampton, England), Hassan Yebda (Benfica, Ureno), Fouad Kadir (Valenciennes, Ufaransa), Karim Ziani (VfL Wolfsburg, Ujerumani), Chadli Amri (Kaiserslautern, Ujerumani), Djamel Abdoun (FC Nantes, Ufaransa), Ryad Boudebouz (FC Sochaux, Ufaransa)
Washambuliaji: Karim Matmour (Borussia Mönchengladbach, Ujerumani), Rafik Djebbour (AEK Athens, Ugiriki), Abdelkader Ghezzal (AS Bari, Italia), Abdelmalek Ziaya (Al-Ittihad)

habari kutoka gazeti la mwananchi.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA