Maziwa, Chilli, Pipi na Biskuti toka TFDA ambazo zimezuiriwa

Bidhaa za vyakula kama vile maziwa chapa NAN2 na vikolombwezo vya vyakula kama vile pilipili ya chupa (chilli), peremende (pipi) na biskuti vimepigwa marufuku na mamlaka inayohusika na chakula Tanzania, TFDA, kufuatia kugundulika kuwepo bidhaa bandia na hivyo kuwa na athari na hatari kwa afya na mwili.

Hatua hiyo ilitangazwa Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, alipozungumza na waandishi wa habari.

“TFDA inapenda kuutaarifu umma kuwa katika ukaguzi uliofanyika Dar es Salaam na hasa maeneo ya kuuzia vyakula, imebainika kuwepo kwa bidhaa bandia na ambazo hazijasajiliwa na Mamlaka na hivyo usalama na ubora wao kutothibitishwa,” alisema Sillo.

Bidhaa zilizokamatwa ni makopo 2,261 ya maziwa bandia ya watoto wachanga aina ya NAN 2 ambayo yanatofautiana kwa kiasi kikubwa na maziwa halisi, chupa 93 za nyanya na pilipili za chupa na pakiti 149 za peremende na biskuti, ambazo hazikidhi viwango na matakwa ya sheria.

Sillo alisema kutokana na ugumu wa mwananchi wa kawaida kugundua maziwa bandia ya NAN 2 kutokana na makopo yake kufanana sana na maziwa halisi, ndiyo maana TFDA imepiga marufuku uingizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya maziwa yote ya NAN 2, wakati uchunguzi wa kubaini mtengenezaji na athari zitokanazo na maziwa hayo bandia ukifanyika.

Jinsi ya kung'amua HALISI na FEKI

Wakati maziwa halisi ya NAN2 yanaonesha kutengenezwa na Kampuni ya Nestl’e ya Ufaransa, huku maelezo ya matumizi yakiwa katika lugha za Kiswahili na Kiingereza, maziwa bandia ya NAN 2 yanaonesha kutengenezwa na Kampuni ya Nestl’e ya Afrika Kusini na maelezo ya matumizi yameandikwa kwa Kiingereza na lugha nyingine ambayo TFDA wameshindwa kuifahamu.

Lakini pia wakati maziwa halisi ya NAN 2 katika kitambulisho chenye maelezo kuna picha ya ndege watatu weupe ambayo ndiyo nembo sahihi ya Nestl’e, kwenye kopo la maziwa bandia ya NAN 2 kina picha ya ndege watatu weupe ambapo mkubwa anawalisha wawili wadogo kwenye kiota.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, tofauti nyingine ni maandishi. Wakati NAN 2 halisi maandishi yako kwenye kopo, maziwa bandia yana karatasi lililobandikwa.

Kuhusu pilipili bandia, Sillo aliitaja ya Eyakho, ambayo imefungashwa kwenye chupa angavu ya lita mbili ambayo ina rangi nyekundu isiyokolea, ikiwa na kifuniko cha kijani, kitambulisho kinachobanduka kirahisi na anuani iliyoandikwa 5 Henry Nxumalo Street, Nowton na tarehe za kusindikwa na mwisho wa matumizi hazijaoneshwa.

Nyanya na pilipili zenye jina la Al’s Sauces Tomato Sauce na Al’s Sauces Chilli Sauce ambazo zimefungashwa kwenye chupa za ujazo wa lita mbili, bila anuani ya mtengenezaji, zenye rangi nyekundu iliyokolea, kizibo cheupe na bila tarehe ya siku ya kusindikwa na mwisho wa matumizi.

Wananchi wametakiwa kutumia maziwa yaliyosajiliwa, ikiwa ni pamoja na Lactogen 1 Infant Formular, Lactogen 2, Cowbell yanayotengenezwa na Kampuni ya Ufaransa na NAN1 Starter Infant Formular yanayotengenezwa Uholanzi.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA