CHADEMA YAFUNGUA MILANGO:RATIBA YA KUCHUKUA FOMU, VIKAO VYA MCHUJO NA UTEUZI WA WAGOMBEA


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetoa ratiba kwa wanachama wake wanaotaka kugombea udiwani, ubunge na urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015 kujitokeza kuchukua fomu. 

Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alitangaza ratiba hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam kuhusiana na maazimio yaliyofikiwa na Kamati Kuu ya chama hicho katika mkutano wake wa siku mbili.

Mkutano huo ulifanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Jumapili hadi juzi.

UDIWANI

Alisema uchukuaji na urejeshaji wa fomu za udiwani katika kata ambazo CHADEMA hakina madiwani utaanza Mei 18 hadi Juni 25, mwaka huu wakati kwa kata ambazo chama hicho kina madiwani utaanza Julai Mosi hadi Julai 20 mwaka huu.

Mbowe alisema uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani wa kata pamoja na viti maalum ambao utafanywa na Kamati Tendaji za Majimbo, utafanyika Julai 15 hadi 20 mwaka huu.

UBUNGE

Mbowe alisema kuchukua na kurejesha fomu za ubunge wa majimbo na ubunge wa viti maalum katika majimbo ambayo CHADEMA hawana wabunge uchukuaji fomu na urejeshaji fomu utaanza Mei 18, hadi Juni 25, mwaka huu.

Kwa upande wa majimbo ambayo CHADEMA ina wabunge kwa sasa utafanyika Julai 6 hadi 10, mwaka huu na uteuzi wa awali wa wagombea ubunge utafanyika kati ya Julai 20 na 25, mwaka huu.

Mwenyekiti huyo alisema uteuzi wa mwisho utakuwa kati ya Agosti 1 na 2, mwaka huu.

URAIS

Kuhusu urais, Mbowe alisema kuchukua na kurejesha fomu kutafanyika kati ya Julai 20 na 25, mwaka huu na Agosti 3 na 4, mwaka huu vikao vya Baraza Kuu la Taifa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CHADEMA vitakutana.

Alisema wanachama watakaochukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania urais mwaka huu, watapelekwa kwenye mchujo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kupatikana mgombea mmoja atakayesimama kwa niaba ya vyama vinavyounda Ukawa.

Vyama vinavyounda UKAWA ni CHADEMA, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA