Tanzania, Uganda Kutatua Migogoro Mipakani


SERIKALI za Tanzania na Uganda zimepiga marufuku watu kujenga nyumba katika mipaka inayozitenganisha nchi hizo ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima.

Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki mkoani Kagera na wakuu wa wilaya za Misenyi kutoka Tanzania pamoja na wakuu wa Wilaya za Rakai na Isingiro za nchini Uganda.
 
Wakuu hao wa wilaya walitoa maagizo hayo baada ya kukutana kwenye mkutano wa ujirani mwema uliofanyika eneo la Mutukula, Tanzania.
 
Katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Fadhili Nkurlu, ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo, alisema ajenda kuu katika mkutano wao ilikuwa ni kujadili jinsi ya kutatua kero mbalimbali, zikiwamo mfereji uliochimbwa katikati ya mpaka wa kimataifa katika eneo la Mutukula.
 
“Mfereji huo humwaga maji machafu kutoka upande wa Uganda na kuishia katika makazi ya Watanzania na unasababisha uharibifu wa mali na miundombinu mbalimbali.

“Katika suala hilo, tulikubaliana kuwa, suala hilo lirudishwe kwa wataalamu wa ardhi wa nchi husika ili walitazame kwa makini na kutoa ushauri na mapendekezo yatakayotatua kero hiyo.
 
“Wataalamu hao tumewapa muda wa siku 30 kuanzia Mei 7 mwaka huu ili wakamilishe jambo hili na kupeleka ripoti kwetu ili ufumbuzi upatikane.

“Wataalamu hao watazunguka mpaka mzima kuanzia jiwe namba 27 hadi 41 ili kubaini matatizo madogo madogo yanayosababishwa na jamii au yanayoikumba jamii iliyoko mipakani ili tuyafanyie kazi na kuendeleza amani iliyopo,” alisema Nkurlu.
 
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Rakai, Mubiru Charles na Mkuu wa Wilaya ya Isingiro, Muhangi Herbert, walisema kwa nyakati tofauti kwamba wanasubiri ripoti itakayoletwa na wataalamu hao wa ardhi  ili kuona makosa yamefanyika wapi na yatafutiwe ufumbuzi.
Mpekuzi blog

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA