MAMBO 10 ALIYOZUNGUMZA LOWASSA NA WAANDISHI WA HABARI KWA MARA YA KWANZA




Mhe. Edward Lowassa amefanya mkutano maalum leo nyumbani kwake mjini Dodoma ambapo ananukuliwa kusema yafuatayo kwa muhtasari:



1. Hahusiki lolote na sakata la Richmond na ndio sababu hata kamati ya Mwakyembe haikuona sababu ya kumhoji. Amesisitiza kuwa cheo cha uwaziri mkuu ndio ilikuwa lengo la kamati ya mwakyembe na spika wa bunge kipindi hicho Samwel Sitta. Amesisitiza hicho sio kikwazo kwake katika kuingia Ikulu kwani sakata la Richmond lilipikwa kumchafua. Amechukua muda mrefu kuzungumzia hili la Richmond na amesema atalisema zaidi Arusha wikendi hii.

2. Anaamini kila mtangaza nia ana makundi ya kumuunga mkono. Yeye katika mkutano huu na wahariri leo ameambatana na Nazir Karamagi, Peter serukamba, Diana chilolo, Hussein Bashe na wengineo huku wengi wakiwa ni waliojeruhiwa katika serikali ya awamu ya nne akiwemo Aliekuwa DC Igunga Elibariki Kingu. Pia aliyekuwa mkurugenzi wa HakiElimu Elizabeti Misoki naye alikuwepo. Amehoji kwani akina Karamagi wana tatizo gani na kwani wao sio binadamu?

3. Lengo kuu atakaloanza nalo ni Elimu na siyo Kilimo Kwanza cha serikali ya Rais Jakaya Kikwete. Amesema serikali ya JK ilikosea kuanza na kilimo na kuweka kando elimu. Ametangaza kuwa sera yake ni Elimu Kwanza.

4. Kuhusu pesa anasema anapata michango ya rafiki zake na ataendelea kupokea michango hii wakati wote wa harakati zake na haina madhara yotote.

5. Anasema hatahama CCM na asiyemtaka yeye CCM ndie aondoke ndani ya chama kwani yeye ana uhakika wa kupata nafasi kuwania Urais.

6. Hatalipa kisasi kwa lolote lililomtokea katika siasa. Amemwachia Mungu kwani yeye ni mcha Mungu.

7. Arusha itawaka moto tarehe 30 mwezi huu na kuwataka watanzania kutega sikio kwani ataanika kila jambo kuhusu mustakabali wa nchi hii na mipango yake ya kuiinua nchi kiuchumi katika miaka kumi ijayo. Lowassa: Nimeingia CCM tangu mwaka 1977. Maisha yangu yapo CCM; Mafanikio ilyopata CCM yasiifanye ikabweteka mwaka 2015; upinzani umeimarika.

8. Toka nimetoka Serikalini; tumekuwa wagumu wa kufanya maamuzi. Kila kitu ni legelege! Waganda, Wakenya na Wanyarwanda wanatupita!

9. Afya ni neema toka kwa Mungu: Nawahakikishia watanzania kuwa “am fit and kicking” nashauri watangaza nia wote tupimwe wote afya

10. Arusha itawaka moto tarehe 30 Mei 2015; Watanzania tegeni sikio kwani nitaanika kila kitu kuhusu mustakabali wa nchi hii!

Wahariri wakuu katika media zote kupitia Jukwaa la Wahariri walikuwepo. Absalom Kibanda (New Habari) na Nevil Meena (Free Media) ndio walikuwa waratibu wakuu wa mkutano huu.

  • Taarifa hii imetumwa na "Mwana Mpotevu" kwenye ukumbi wa majadiliano JamiiForums





HABARI KWA KINA

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amezungumzia kwa mara ya kwanza sakata la Richmond lililosababisha ajiuzulu wadhifa huo, akisema alichukua tahadhari katika suala hilo na kuwa ubishi umeligharimu Taifa kulipa Dola za Marekani bilioni 120.

Mbali na hilo, Lowassa ametaka watu waache kumchonganisha na Rais Jakaya Kikwete, huku akimsifu kwa kutekeleza kwa mafanikio Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Aidha, amesema hana mpango wa kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM), na pia ametoa changamoto kwa wanaCCM wanaotaka kuwania urais wapimwe afya zao.

Lowassa aliyasema hayo jana katika mkutano wake na wahariri wa nyombo mbalimbali vya habari nchini uliofanyika nyumbani kwake Area C mjini hapa.

Lowassa aliyejiuzulu wadhifa wake huo Februari 2008, akihusishwa na sakata la Richmond – kampuni ya kufua umeme iliyoletwa nchini mwaka 2006 baada ya kuwapo kwa matatizo makubwa ya nishati ya umeme, alitoa sababu nne za kukaa kimya tangu wakati huo.

Alizitaja kuwa kwa mwanasiasa kukaa kimya pia ni silaha, hivyo aliamua kukaa kimya; kuogopa upotoshaji wa vyombo vya habari, siasa kuwa za uhasama, kusingiziana na kuogopa kuanzisha malumbano zaidi katika jamii.

Kuhusu Richmond alisema ‘zengwe’ hilo limeeleweka nchini kwani limeandikwa sana na kuzungumzwa sana.
“Lakini tunajifunza nini? Walikuja wakubwa wawili hapa Hillary Clinton na Rais Obama (Barack) wa Marekani…wote hawa walisema kuwa mtambo ule ulikuwa state of the art (wa kisasa sana),”
“Kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbowe bungeni hivi karibuni, ubishi ule umegharimu bilioni 120 (Dola za Marekani), tulitaka kuvunja mkataba wa Richmond.
“Nikasema wataalamu wasituingize mkenge, nikamwita Mwanasheria Mkuu wa Serikali nikamwambia kuna story hii, be careful. (Anasema iliandikwa na gazeti la The Guardian).
“Baadaye nikaandika kwa maandishi kwa Mwanasheria Mkuu. Halafu kulikuwa na timu ya makatibu wakuu inaongozwa na Bwana Mgonja (Gray). Lakini ubishi wa kisiasa umetugharimu bilioni 120.”

Alisema pia Waziri wa Fedha wakati huo, Zakia Meghji hakutoa fedha zozote kwa kampuni hiyo na kwamba hata Rais alimwambia aliyekuwa Waziri wa Nishati, Ibrahim Msabaha “kuwa makini, vinginevyo utakwenda kujinyonga kwenu Msoga.”

Lowassa aliongeza kuwa asingependa kulijadili suala hilo zaidi, lakini akatolea mfano alipokuwa Waziri wa Maji na Mifugo, alivyoweza kuvunja mkataba wa City Water.
“Chini ya Rais Mkapa tuliweza kuvunja mkataba ule. Tukafanya vikao saa tisa mchana, tukafanya timing ya benki, kisha ili mzungu yule asipate muda, tukampa warrant, saa tisa akampanda KLM kurudi kwao.
“Tulihofia kuwa kama tusingewahi angekwenda kuweka court injections, kwa uzoefu ule wa 1995, tulitaka kuvunja mkataba, lakini nakumbuka rafiki yangu mmoja, Lipumba akasema tutalipa mabilioni, si kweli. Kwa hiyo, wakati ule sikuweza kwa sababu mamlaka hayakuwa kwangu,” 
alifafanua Lowassa.

Alisema imewachukua Hillary Clinton na Rais Obama kuja nchini kueleza kuwa mitambo ile ni ya kisasa, na ndiyo maana alibainisha kuwa alipojiuzulu alisema ajenda ilikuwa ni Uwaziri Mkuu.

Alipoulizwa nani alikuwa anautaka Waziri Mkuu, Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli, alisema hilo anamuachia muuliza swali.

Kuhusu uhusiano wake na Rais Kikwete, Lowassa ambaye alisema Jumamosi atatangaza nia yake ya kuwania urais akiwa Arusha, aliwataka watu waache kumchonganisha na mkuu huyo wa nchi.
“Kwa nini urafiki wetu uwe ajenda? Kwa nini mnapandikiza hilo, yeye ni rafiki yangu, achene maneno yasiyo na maana,” 
alisema Lowassa na kuongeza kuwa hata kama walichukua fomu pamoja mwaka 1995, lakini miaka mingi imepita na muhimu ni kuangalia kama urafiki wao umeshawishi kitu fulani.

Akizungumzia utajiri wake, mwanasiasa huyo alikiri kumiliki nyumba kadhaa (hakuzitaja idadi) na pia anazo ng’ombe kati ya 800 hadi 1,000, lakini akaongeza kuwa anauchukia umasikini na anatamani utajiri.

“Hili ni swali zuri sana, lakini mtashangaa majibu yangu. Namiliki nyumba kadhaa na nina ng’ombe kati ya 800 na 1,000. Na kule kwetu ninakotoka, ili uwe kiongozi lazima uwe na mifugo ya kutosha,”
“Lakini kama watu wanataka kufahamu utajiri wangu waende Sekretarieti ya Maadili, unalipa kidogo utasoma kila kitu. Lakini ngoja niseme kidogo, natamani utajiri.
“Tuache kuwabeza matajiri, kuwa na matajiri kama Mzee Mengi, Bakhresa, kina Karamagi, ni jambo zuri sana na hawa ni role model, tungekuwa nao 20,000.
“I hate (nachukia) umasikini. Nataka uongozi ili kuwaondoa Watanzania katika umasikini. Kama mtu amepata utajiri kwa njia za uhalali, amejinyima, ni nzuri sana. Nachukia watu wanaopata fedha na kuishia katika ulevi na wanawake. Kina mama mnisamehe. Sitaki kupata uongozi kwa kudanganya, nachukia umasikini.”

Alipoulizwa kuhusu harambee mbalimbali anazozifanya misikitini, makanisani na kwingineko na kuchangia mamilioni ya fedha, Lowassa alizitetea harambee hizo na kueleza kuwa fedha zinachangwa na marafiki zake.
“Zile sio fedha zangu, kwa mfano kule Arusha juzi, zilichangwa milioni 200, watu wamesema nimechangia shilingi milioni 200, hapana. Mimi na marafiki zangu wa Arusha, Dar na kwingineko tumechanga shilingi milioni 100, Makamu wa Rais amechangia shilingi milioni 10,”
“Kuchangia misikitini, makanisani na katika maendeleo ni jambo zuri, kwa wenzetu wa Kenya harambee ndio kila kitu. Nawashauri viongozi na wabunge kwenda vijijini kusaidia maendeleo kwa njia ya harambee.
“Hili la shule za kata ambalo ni mawazo ya CCM na maelekezo ya Rais, limefanikiwa kwa nguvu za Serikali na wananchi, kwa hiyo harambee zinafaa.”

Kuhusu afya yake, alisema yuko fiti na ni upuuzi kusema kuwa ni mgonjwa, na akatoa changamoto kwa wanaCCM watakaojitokeza kuwania urais, wakapimwe afya zao.
“Nimetembea pale Dar kilometa tano, wakasema siwezi kukimbia hata kilometa 100 na kuwa nimepelekwa Ujerumani kutibiwa. Huu ni upuuzi, ni chuki kutakiana mabaya. Niko fit and kicking. Fit kwa chochote kile.
“Tukapimwe afya zetu kujua nani mgonjwa, tutakutana kwenye uwanja wa mapambano, na I will beat them by far (nitawashinda kwa mbali).”

Alipoulizwa kama asipoteuliwa na CCM kuwania urais, atahama chama hicho, tawala, Lowassa alisema hana mpango B katika hilo, na CCM ni haki yake.
“Sina mpango wa kuhama. Nimeingia CCM mwaka 1977 na sijawahi kutoka katika majukumu yake zaidi ya pale nilipokuwa Mkurugenzi Mtendaji wa AICC.
“My right is CCM (haki yangu ni CCM), sio kwa hao kina kadeti. Huyo ambaye hanitaki CCM ndio ahame. Hakuna mpango B, nina mpango A na naamini utafanya kazi.”

Aidha, akizungumzia kuhusu madai kuwa akiwa Rais atalipiza kisasi, Lowassa alisema yeye ni Mkristo, na imani yake inamtaka kusamehe mara 70, hivyo hatalipa kisasi, moyo wake ni mweupe na yaliyopita yamepita.

Akitoa maoni baada ya kuulizwa kuhusu chama chao CCM, Lowassa alisema hakipaswi kubweteka kwani upinzani umepata nguvu sana mijini na vijijini.
“Tusibweteke wenzetu wamejiandaa, na mkiondolewa hamrudi madarakani, angalia KANU, UNIP na vinginevyo. Lakini faida kubwa ya CCM ni kuwa Rais Kikwete ametekeleza vizuri sana Ilani, hii ndio kete yetu, jamaa mmoja alisema mtaji wetu, lakini isitubweteshe, tutatue matatizo ya wananchi na watu wahimizwe kujiandikisha kwa wingi,” 
alibainisha mwanasiasa huyo.

Lowassa ambaye baadhi ya maswali aliyajibu juu juu au kukataa kuyajibu kwa kuwa alisema yapo katika hotuba yake ya Jumamosi mkoani Arusha, alisisitiza suala la elimu kuwa kipaumbele namba moja na pia tatizo la ajira kama bomu lisiposhughulikiwa ipasavyo.

Kuhusu ajira, alisema chama chochote kinachotaka kushika madaraka, lazima kizungumzie ajira na jinsi litakavyotengeza fursa hizo, akitoa mfano wa uchaguzi wa karibuni wa Uingereza kati ya David Cameroun na Ed Milbrand na pia Obama alipoingia madarakani.

Aliwataka Watanzania walifikirie hilo kwa umakini.

Katika elimu, alisisitiza kuwa kwake kipaumbele cha kwanza, cha pili, cha tatu ni elimu, na kwamba nchi ikiwekeza vizuri kielimu, itasonga mbele kiuchumi.

Alisema elimu nchini imeparaganyika na hakuna budi kusakwa jibu la maarifa kwani imefikia mahali watu wanawachukia Wachina kwa sababu wanakuja na kuajiriwa kama walinzi Kariakoo.

Lowassa alipoulizwa kama angekuwapo serikalini hadi sasa na akaomba kuwania urais, alisema: 
“Naamini kwa kasi ile, ningepunga mkono, na kuzoa kura zote. Lakini nasikitika hatufanyi maamuzi, yawe mabaya au mazuri. Rais amefanya kazi nzuri, lakini hatukupaswa kuachwa nyuma na Waganda, Wanyarwanda.”


































































Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA