Watu Watano Wathibitishwa Kufariki Dunia Jijini Dar es Salaam Kutokana na Mafuriko


JAMHURI YA MUUNGANO WATANZANIA
WIZARA YA MAMBO YANDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
PRESS RELEASE
08/05/2015

WATU WATANO WATHIBITISHWA KUFARIKI DUNIA JIJINI DAR ES SALAAM KUTOKANA NA MAFURIKO
Watu watano wameripotiwa kupoteza maisha jijini Dar es Salaam kutokana na athari za mafuriko kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha jiji. Mvua hizo zinazonyesha kwa siku tatu mfululizo zimesababisha vifo vya watanzania hawa katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam kama ifuatavyo:
Mnamo tarehe 06/05/2015 majira ya saa moja kamili usiku huko maeneo ya Magomeni Kinondoni jijini Dar es Salaam mtu mmoja jina SHABAN S/O IDD, Miaka 73, Mkazi wa Manzese alisombwa na maji ya mto ng’ombe alipokuwa akijaribu kuvuka mto huo. Mwili wake ulipatikana siku iliyofuata 07/05/2015 akiwatayari amekwishafariki dunia na umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala.
Kifo kingine kilitokea tarehe 07/05/2015majira ya  saa sita kamili mchana huko maeneo ya Mwananyamala Mbuyuni Kata ya Mwananyamala, OysterBay, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo mtu mmoja aitwaye MASUMBUKO S/O DOUGLASS @ LIMAMU, Miaka kati ya 50-55, mkazi wa Mwananyamala Mbuyuni, alianguka na kufariki dunia ghafla wakati anatoa maji yaliyoingia nyumbani kwake. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alikuwa na tatizo la ugonjwa wa kifafa hivyo wakati akihangaika kutoa maji, ugonjwa huo ulimpata na kuanguka kwenye maji na kufariki dunia baada ya kukosa msaada wa haraka. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi.
Mtu mwingine mwanaume RASHIDI S/O HASSAN, Miaka 36, Mkazi wa maeneo ya Mvuruhani Pemba Mnazi Kigamboni jijini Dar es Salaam alizama katika mkondo wa maji unaoelekea baharini tarehe 06/05/2015. Mwili wake ulipatikana tarehe 07/05/2015 ukiwa unaelea majini umbali wa mita 500 toka eneo alilozama.
Kifo kingine kimetokea tarehe 06/05/2015 huko Yombo Makangarawe ambapo mtoto aitwaye GLORIA D/O MREMA, mwaka mmoja na miezi mitatu alipotea baada ya watoto wenzake kumuacha wakati wakicheza pamoja. Juhudi za kumtafuta zilifanyika bila mafanikio hadi mwili wake ulipopatikana ukiwa unaelea majini katima mto mzinga akiwa tayari ameshapoteza maisha.  Mwili umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke
Kifo kingine kimetokea tarehe 08/05/2015 saa moja kamili asubuhi huko maeneo ya Kinondoni Mkwajuni, Kata ya Mkwajuni Wilaya ya Kinondoni ambapo mtu mmoja mwanaume ambaye jina lake halikufahamika mara moja anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka (40-45) mkazi wa Kinondoni Mkwajuni, alikutwa amefariki dunia. Mwili umehifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi.
Pamoja na vifo hivyo kuripotiwa, pia mtu mmoja ajulikanae kwa jina la MABULA S/O MOSSES, Miaka 65, Mkulima, Mkazi wa Vingunguti,  Buguruni wilaya Ilala amevunjika mguu wake wa kulia sehemu ya chini ya goti baada ya kuangukiwa na ukuta wa Godown la FIDA S/O HUSSEIN lililopakana na nyumba yake. Pia ukuta huo umesababisha uharibifu wa vitu mbalimbali. Majeruhi amepekwa Hospitali ya Amana kwa matibabu.
Katika kata ya Mchikichini, taarifa ya mafuriko inaonyesha takribani nyumba 60 hadi 70 zimefunikwa na maji hadi juu ya mapaa ambapo wakazi wake tayari walikuwa wamehama kufuatia agizo la Serikali kuwa wahame maeneo hayo. Pia takribani watu 30 hadi 35 wamejihifadhi katika shule ya Srkondari Mchikichini.
Katika Kata ya Jangwani, zipo nyumba zinazokadiriwa kufikia 90-100 zimefunikwa na maji hadi juu ya paa. Wakazi takribani 250-300 walihama mapema kufuatia taarifa hiyo ya Serikali. Aidha watu wanaokadiriwa kati ya 25-30 nao wamejihifadhi katika Shule ya Sekondari Mchikichini.  
Aidha, maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha ni Keko, Chang’ombe maduka mawili, Yombo Vituka, Vingunguti, Africana, Msasani Bonde la Mpunga, Eneo la Jangwani, Manzese, Kigogo, Mburahati, Boko Basihaya, na maeneo mengine ambayo taarifa zake bado hazijapokelewa
Barabara zinazounganisha katikati ya Jiji na pembezoni zimeharibika na hivyo kusababisha kutolewa maelekezo barabara hizo kufungwa ili kupunguza madhara ambayo yangeweza kutokea.
Aidha, madaraja mbalimbali yameharibika h
ivyo kukata mawasiliano kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine. Kwa mfano daraja la linalounganisha Mbagala na Mtoni Kijichi maarufu kama njia ya ng’ombe. Daraja lingine ni lile la Kinyerezi ambalo halipitiki baada ya kusombwa na maji.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Serikali limejiandaa kwa hali ya dharura itakayojitokeza. Pia Jeshi la Polisi limejipanga kukabili foleni kwa kuhusisha askari wa vikosi mbalimbali ili kukwamua tatizo hilo ambalo limesababishwa na uharibifu wa miundombinu.
Aidha nawataka wananchi wote kuchukua tahadhari ya hali ya juu hasa wale waishio maeneo ambayo ni mikondo ya maji au watumiaji barabara zinazopitiwa na mikondo hiyo. Wananchi wanaombwa kutoa taarifa za mapema na haraka pindi wanapoona au kugundua kuna maeneo au jambo  linalohatarisha maisha yao na ya watu wengine.
NB: Wakati huo huo zimepokelewa taarifa za kupatikana kwa miili ya watu watatu waliofariki ambayo inafanyiwa uchunguzi katika hospitali mbalimbali jiji Dar es Salaam ili kujua kama vifo hivyo vimetokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha jiji. Taarifa kamili zitatolewa kuhusu wajihi wa watu hao na wako katika hospitali gani
 
S. H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA